Nguesso ashinda tena urais Congo-Brazzaville kwa asilimia 95

Kwa ushindi huo ushindi huo Nguesso mwenye umri wa miaka 82 ataendeleza utawala wake ambao umechukua takribani miaka 42 katika taifa hilo la Afrika ya Kati.

Rais wa Jamhuri ya Congo, Denis Sassou Nguesso, ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais kwa kupata asilimia 94.82 ya kura.

Matokeo hayo yametangazwa usiku wa kuamkia leo Jumatano Machi 18, 2026 na televisheni ya taifa hilo. Kwa ushindi huo ushindi huo Nguesso mwenye umri wa miaka 82 ataendeleza utawala wake ambao umechukua takribani miaka 42 katika taifa hilo la Afrika ya Kati.

Katika matokeo hayo, mshindani aliyeshika nafasi ya pili, Mabio Mavoungou Zinga, amepata asilimia 1.48 ya kura.

Vyama vikuu vya upinzani chini humo vilisusia uchaguzi huo, huku baadhi ya vigogo wa upinzani akiwemo Jean-Marie Michel Mokoko na Andre Okombi Salissa wakiwa gerezani kwa takribani muongo mmoja sasa.

Siku ya kupiga kura Jumapili, kuliripotiwa changamoto kadhaa ikiwemo kuchelewa kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura na kukatika kwa huduma ya intaneti nchini kote.

Licha ya hayo, televisheni ya Taifa ilieleza kuwa jumla ya wapiga kura waliojitokeza ilikuwa asilimia 84.65, ingawa katika baadhi ya vituo jijini Brazzaville kulishuhudiwa idadi ndogo ya wapiga kura.

Ushiriki mdogo na mazingira tata

Uchaguzi huo umefanyika katika mazingira yaliyogubikwa na changamoto kadhaa, zikiwemo wito wa kususia uliotolewa na vyama vikubwa vya upinzani.

Vyama viwili vikuu havikushiriki katika uchaguzi huo, huku vikihamasisha wananchi kutojitokeza kupiga kura, jambo lililochangia kupungua kwa mwitikio wa wapiga kura.

Licha ya kuwepo kwa wagombea sita kutoka vyama vidogo, wachambuzi wa siasa wanaeleza kuwa hakuna aliyekuwa na nguvu ya kumpa ushindani wa maana Rais wa sasa.

Hali hiyo imeibua hoja kuhusu ubora wa ushindani wa kisiasa na uhalisia wa demokrasia nchini humo huku kwa upande mwingine, hali ya usalama na hatua zilizochukuliwa na mamlaka wakati wa uchaguzi zimezua mjadala. Mawasiliano ya mtandao yalizimwa katika maeneo mbalimbali ya nchi, huku usafiri wa magari ukidhibitiwa katika mji mkuu wa Brazzaville. Hatua hizo, kwa mujibu wa wachambuzi, zilichangia kuongeza hofu na kupunguza ushiriki wa wananchi katika zoezi la kupiga kura.

Wachambuzi wanaeleza kuwa mabadiliko hayo ya Katiba ni miongoni mwa mambo yanayochangia kupungua kwa imani ya wananchi katika mchakato wa kidemokrasia, kwani yanaonekana kupunguza ushindani wa kisiasa na kufifisha matumaini ya mabadiliko ya uongozi.

Changamoto za uchumi na maisha ya wananchi

Pamoja na mjadala wa kisiasa, hali ya uchumi wa Jamhuri ya Congo Brazzaville imeendelea kuwa kitovu cha wasiwasi kwa wananchi wengi.

Licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali za asili, hususan mafuta na madini, taifa hilo linakabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, deni la taifa hilo limefikia takribani asilimia 94 ya pato la taifa, hali inayozorotesha uwezo wa serikali kutoa huduma muhimu kwa wananchi.

Aidha, kiwango cha umasikini kinaendelea kuwa cha juu, huku vijana wengi wakikosa ajira na fursa za kujikwamua kiuchumi.

Mchambuzi wa masuala ya kijamii na uchumi, Marie Therese Ndziessi, anasema zaidi ya nusu ya wananchi wanaishi katika mazingira magumu ya kiuchumi, hali inayoongeza shinikizo kwa serikali inayotarajiwa kuundwa baada ya uchaguzi. Anabainisha kuwa, ingawa uchaguzi unaweza kuendeleza utulivu wa kisiasa, matarajio ya wananchi yako zaidi katika mageuzi ya kiuchumi yatakayoboresha maisha yao ya kila siku, ikiwemo upatikanaji wa ajira, huduma za kijamii na usimamizi bora wa rasilimali za taifa.