Najua unanisikia hata kama hutanijibu. Katika kumbukizi hili, mafyatu wenzako tunakukumbuka kinamna. Wapo wanaokulilia na wanaoshangilia kutegemea na hali. Leo, sitachonga sana bali kufyatuka.
Kwanza, wasalimiwa na mafyatu wako wote na wananzengo. Tunakumiss kifyatu.
Pili, pole kwa sababu, kama ulivyokuwa ukisema, kuna mafyatu utawashangaa. Ungerudi, ungejinyotoa roho namna mambo yalivyovurugika. Mfano, mafyatu na majipu uliyokuwa ukiyatumbua yalisharejeshwa na yanazidi kutanuka na kutanua. Juzi, wapigaji wa mwendofasta waliachiwa.
Tatu, unaweza kufyatua vibao mafyatu, tena uliowaamini na kutengeza. Si ulisema kuwa watakaofyatua Bwagamoyo ni mataahira na mazwazwa. Kumbe uliwajua! Ungekuwepo, nadhani eheee, kingeleweka. Hata hivyo, ujue. Simba akifariki, panya hutafuna ngozi yake. Ndviyo ilivyotokea. Yale ambayo hukuwahi kudhani yangetokea, yeshatokea zamani. Mafyatu waliogoma kufyatuka wakafyatua sasa wanafyatuliwa kama hawana akili nzuri.
Nne, ungerejea, kabla ya kujinyotoa na kufyatua watu mbanta, ugepata kichaa. Maana, wengi uliodhania wafuasi wako sasa wanaimba ngonjera na nyimbo za kukukandia na kukukana. Juzi, nilisikia mmoja uliyemtoa mikoani na kumpa kipaza sauti akisema eti wewe hukukusanya gold! Si alirambishwa asali, wengi siyo walikusaliti tu, bali wanapmbana kulihalli usahaurike kana kwamba hukuwahi kuwapo na kutisha.
Tano, mwaka jana kuna mafyatu waitwao ‘mamluki’ walikinukisha wote tukanuka hadi kufyatuana shaba. Wengine walifanyiwa kale ka mchezo ulikoacha. Wasiojulikana bado wapo. Waliwafyatua, kuwapoteza na wengine kuwanyotoa roho. Shaba zilitembea mitaani usipime.
Sita, walitokea mabeberu wakatuma mamluki wakatuonea wivu na kuja kuvuruga amani yetu. Walitutaimu siku ya uchaguzi wa amani na mshikamano. Walitaka kuuvuruga tukawavuruga ile mbaya tena kifyatufyatu. Siku hiyo, amani ilivugika hadi shaba zikageuka lugha pekee. Mwaka jana mwezi wa kumi tarehe 29 haitasahaulika kwa mafyatu siku walipokinukisha hawa mamluki hadi kisiwa cha amani kikageuka kisiwa cha vita na umwagaji damu ambavyo havikuwahi kutokea.
Saba, pamoja hila na wivu wao, tunamshukuru Mungu, rahis wetu alishinda kwa asilimia 98. Mbili zilizobaki ziliibiwa na wapingaji wachoyo wa madaraka. Baada ya kukinukisha na kufyatuana, sorry, kuwafyatua mamluki, tuliunda tume ya kujichunguza lau tujue nani alizembea hadi kikanuka. Wapo mabeberu waliotucheka na kutuzodoa kuwa tunawezaje kujichunguza. Hebo! Bila kujichunguza, utawezaje kujisuta. Hawa walitaka tuite wengine watuchunguze halafu watusute wakati tunaweza kufyatua vyote viwili, yaani kujichunguza na kujisuta na kuwatuliza mafyatu waliofyatuliwa tokana na uzwazwa wao wa kukataa kufyatuka wakafyatua hadi wakafyatuliwa.
Nane, nadhani unakumbuka wale mafyatu wa akina yero kule Ngolongolo. Walishafyatuliwa zamani gani. siku hizi wako ugosini wakijifunza kukata vikalio na kuacha na ngoma zao za kurukaruka. Ilibidi tuwafyatue ili kupisha uwekaji ili kujiongezea kipato.
Tisa, kabla sijasahau, ule uwanja wako wa home ulishadoda. Sikujua kuwa wewe ndo ulikuwa bidhaa kuu iliiyokuwa ikiupa shavu! Baada ya kuondoka si kila kitu kiliondoka. Naomba unisamehe. Usidhani nilikufyatua ua kukusaliti. Hapana. Hata ile biashara yangu ya hoteli niliyokuwa nimefungua Chato niliishafunga baada ya kukosa wateja. Napanga kuihamishia kule Kizinkazi ambako siku hizi ndiko kunatesa. You know what I mean.
Kumi, japo ulizuia watoi wako kushiriki siasa, siku hizi Jessie ni mheshi wa viti maalum. Tangu ulipoondoka aligeuka maalum kiasi cha kupewa kiti maalum tokana umaalum wake utokanao na wako.
Kumi na moja, unakumbuka ile kauli mbiu yako ya kutetea wanyonge? Tangu uondoke na unyonge ulikufuata hadi unatendewa kinyonge. Siku hizi, hakuna mnyonge hata mmoja. Ila wanyongaji bado wapo hasa wale maadui wa amani na mshimano wetu kama wale tuliowafyatua walipotaka kuvuruga uchaguzi wetu kwa vurugu badala ya kufanya hivyo kwa amani na mshikamano. Tuliwashika kwa mshikamano na kuwatia adabu kwa amani.
Baada ya kuondoa unyonge, wapo waliopagawa hadi wakageuka machawa. Zamani chawa walikuwa wadudu. Siku hizi uchawa au kuwa chawa ni sawa na kuwa superstaa. Tuna machawa kila aina. Wako wa maza, wa faza, hata chawa wa machawa. Kabla sijasahau, nadhani swahiba yako Rao aka Jaduong Maduong yule wa kaya ya jirani wakimuita baba mshaonana au hajafika. Si naye aliwageuka Gen Ziro w akule walipokinukisha akajiunga na Kasongeyeye mobali nangai. Acha afyatuliwe kuwa alijigeuza msaliti. Alisononeka hadi akarejesha namba akiwa amechafuka. Kuna mafyatu wanaodai kuwa alifyatuka kwa sababu ya usaliti uliosababisha umwagaji damu.
Kabla ya kusahau, wajua? Si kwa Joji kichaka walimchagua chizi aitwaye Donnie Tarampu. We, acha ainyooshe dunia. Ninavyochonga, yupo anazipiga na waajemi kiasi cha kupandisha wese. Ila anazidi kuzidiwa pumzi hadi anaomba nimpe tafu.
Mwisho, kuna busara ambayo sikuielewa ila leo naielewe. Kumbe asikuwepo na lake halipo! Kumbe hata kupe anaweza kuwa mkubwa na mwenye maguvu kuliko tembo aliyemnenepesha hadi akawa hivyo huku tembo akigeuzwa mdogo kuliko inzi. Du! Kumbe naota mchana!
