Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuimarisha safu yake ya utendaji kwa kufanya uteuzi viongozi na kupanga vituo vipya kwa balozi, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa taasisi za umma pamoja na kuimarisha mahusiano ya kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 18,2025 na Katibu Mkuu Kiongozi, Moses Kusiluka, mabadiliko hayo yanagusa maeneo muhimu yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
Katika uteuzi huo, Adam Mrisho ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), taasisi inayosimamia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi nchini.
Balozi Elizabeth Kiondo ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania, akichukua nafasi ya Profesa Rwekaza Mukandala aliyemaliza muda wake.
Katika ngazi ya diplomasia, Balozi Noel Kaganda amepangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Korea, hatua inayokuja wakati Tanzania ikiendelea kupanua wigo wa ushirikiano wa kiuchumi na kimataifa.
