Wadau wataka bajeti zaidi kukabili uhaba wa maabara nchini-3

Rombo/Lushoto. Kuongeza uwekezaji katika elimu na kutengeneza maabara zinazotembea, zimetajwa kuwa miongoni mwa suluhisho linaloweza kumaliza uhaba wa maabara za sayansi katika shule za sekondari za nchini.

Hayo yanatakiwa kwenda sambamba na ushirikishwaji wa jamii na wadau kwa ujumla, kwani ili kumaliza uhaba huo zinahitajika jitihada za pamoja.

Haya yanaelezwa wakati ambapo Tanzania inahitaji asilimia 40.68 zaidi ya maabara ili kufikia kiwango kinachohitajika kwa shule zote za sekondari za Serikali, kwa mujibu wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) 2025/2026.

Bajeti hiyo inaonesha kuwa, katika mwaka wa fedha 2024/2025, kulikuwa na jumla ya shule za sekondari 4,894 zilizohitaji maabara 14,682 ili kufanya kila shule kuwa na maabara tatu za sayansi, yaani kemia, baiolojia na fizikia.

Lakini hadi mwaka husika, kulikuwa na maabara 8,710 pekee, hivyo uhaba kuwa maabara za sayansi 5,972.

Jambo hilo ni matokeo ya utekelezaji na usimamizi duni wa Kanuni ya 15 (1)(c) ya Usajili wa Shule za Sekondari ya mwaka 2016, ambayo inamtaka Ofisa Elimu wa Mkoa au wilaya kuthibitisha uwepo wa maabara zinazofanya kazi kama sehemu ya tathmini ya mazingira ya shule kabla ya usajili kufanyika.

Akizungumzia suala hilo, mdau wa elimu, Dk Luka Mkonongwa, anasema ni ngumu kumaliza uhaba wa maabara kwa sababu si kipaumbele kilichowekwa.

“Ingekuwa ni kipaumbele tungeshamaliza, maana gari moja la Serikali linaweza kupunguza uhaba kwa kiasi kikubwa,” anasema Dk Mkonongwa.

Anasema wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, majengo ya maabara mengi yalijengwa, ilibaki kupeleka vifaa, lakini yameendelea kuwa majengo ambayo hayana vifaa.

“Kama majengo yamejengwa, imebaki kazi ndogo ya kupeleka vifaa vya maabara. Kama wakaguzi wanapokwenda kukagua shule binafsi na wakikuta hakuna maabara haifunguliwi, tufanye hivyo pia kwa shule za Serikali, vinginevyo itabaki kuwa stori za magazeti,” anasema.

Anasema upande wa maabara, mahitaji yake yanajulikana na inawezekana kwa wakaguzi kuhakikisha kila shule ina vifaa vizuri vya maabara kama nchi inahitaji kutengeneza wanasayansi.

Anasema kama ilivyokuwa kwa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja, ni vyema kuhakikisha kuwa kila shule inakuwa na maabara, na hapa tunaweza kushirikisha wadau na jamii husika.

Mdau mwingine wa elimu, Dk Muhanyi Nkoronko, anasema ni vyema upatikane mpango utakaoshirikisha jamii na Serikali, ili kupatikana kwa michango inayoweza kusaidia kuondoa upungufu huo.

Anaiomba Serikali kutenga bajeti zaidi katika kujenga maabara hizo na kuzipatia vifaa stahiki, ili kuwawezesha wanafunzi kufanya mafunzo kwa vitendo.

“Tofauti na sasa, maabara moja wanaingia wengi kwa wakati mmoja, lakini zikiwepo za kutosha, tunaweza kufanya walimu wafundishe kwa kiwango kinachotakiwa,” anasema.

Maabara zinazotembea zatajwa

Katika kukabiliana na hali hiyo kwa hatua za muda mfupi, mwalimu mstaafu wa fizikia, John Philipo, anashauri kwa shule ambazo hazina maabara, ni vyema mkoa kuwa na magari ambayo ni maabara kwa ajili ya wanafunzi ili yawasaidie kufanya vitendo katika masomo lengwa.

Anasema kupitia magari hayo, wanafunzi wa shule mbalimbali wanaweza kukusanywa katika eneo moja na kufundishwa kwa vitendo badala ya kusoma kwa kutumia vitabu pekee.

“Hii inaweza kusaidia kupunguza tatizo (maabara inayotembea), badala ya wanafunzi kusoma kwa kuangalia vifaa katika vitabu, wataona vitendo. Kukosekana kwa maabara hizi hakuwezi kuhamasisha wanafunzi wengi kusoma sayansi,” anasema Philipo.

Anasema uwepo wa maabara katika shule si kitu kinachoweza kupuuzwa, kwani katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia, mtu hawezi kufanikiwa kwa kufanya majaribio mbadala.

Anakumbusha jitihada zilizofanywa katika uongozi wa awamu ya nne kwa kujenga maabara nyingi, lakini ilipofika awamu ya tano, ambayo walitegemea moja ya juhudi zingekuwa ni kuweka vifaa katika maabara hizo, haikutokea.

“Shule nyingi zimebaki na majengo ambayo yanatambulika kama maabara, lakini hayana vifaa. Ni muda sasa wa kuzimalizia ili tujenge kizazi kilichoiva, na magari haya ya maabara yawe kwa ajili ya shule zisizokuwa na maabara kabisa,” anasema.

Anasema magari hayo pia hufanya kazi kwa kuwekewa ratiba ya kupita katika shule mbalimbali, ili kuwezesha wanafunzi kujifunza inavyotakiwa.

“Pamoja na hili kufanyika, ni vyema kila wilaya ikaweka mkakati wa kujenga maabara katika kila shule, na wakati mwingine si lazima kutumia vifaa vya dukani, wanaweza kutengeneza vifaa vyao wenyewe. Ujenzi wa maabara uende sambamba na kuajiri wataalamu wa maabara na si walimu kutumika katika maabara, wawasaidie walimu kufanya practical mbalimbali.”

Halmashauri zinafanya nini

Ili kukabiliana na suala hilo, Ofisa Taaluma wa Halmashauri ya Rombo, Vanence Mgoma, anasema wanaendelea kutumia vyanzo mbalimbali vya fedha kujenga maabara mpya kwa shule za zamani na mpya.

Vyanzo hivyo ni Serikali Kuu, mapato ya ndani, miradi mbalimbali ya kimaendeleo, wadau na wananchi kwa ujumla, huku halmashauri ikitenga bajeti kila mwisho wa mwaka kwa ajili ya kuboresha ufundishaji wa masomo ya sayansi.

“Pia, tunatenga bajeti ya mafuta kwa ajili ya kuwezesha maofisa elimu wa kata na ngazi ya idara kufanya ufuatiliaji, pamoja na kuratibu usambazaji wa vifaa vya maabara na kemikali kutoka Serikali Kuu, na kuratibu upatikanaji na usambazaji wa vitabu na vifaa vya mtaala shuleni,” anasema.

Hayo yataenda sambamba na kukamilisha ujenzi wa maabara zote na zianze kutumika, pamoja na kuhakikisha wanaratibu uwepo wa vifaa na kemikali za kutosha shuleni.

“Pia, kuongeza idadi ya walimu wa masomo ya sayansi na mafundi sanifu wa maabara, kuhimiza na kuwajengea uwezo wanafunzi kupenda kusoma masomo ya sayansi, sambamba na kutumia madarasa janja na njia za kielektroniki katika ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya sayansi,” anasema.

Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Lushoto, Shahara Shaibu, anasema mbali na kutenga fedha kila mwaka za kumalizia maabara nne, pia wako mbioni kuanzisha mfuko wa elimu utakaosaidia kumaliza tatizo hilo.

“Miongoni mwa vipaumbele vilivyowekwa katika mfuko huu ni uboreshaji wa masomo ya sayansi, kutokana na umuhimu unaoonekana kuanzia ngazi ya taifa hadi jamii kuhusu uhitaji wa wanafunzi kusoma masomo hayo,” anasema.

Anasema kupitia fedha zitakazokusanywa kupitia mfuko huo, ukamilishaji wa maabara umepewa kipaumbele, huku fedha nyingine zikitengwa kwa ajili ya kupata walimu wa sayansi kwenye shule zitakazobainika kuwa na upungufu katika masomo hayo.

Pia watatumia fedha hizo kununua vifaa katika shule zitakazoonekana kuwa na uhaba, jambo litakaloenda sambamba na utoaji wa semina kwa walimu wa sayansi, ili wafundishe vizuri kuanzia Februari mwaka huu kwa kutumia rasilimali zilizopo.

Hilo litafanyika kwa kutumia rasilimali zilizopo ndani ya wilaya husika, ikiwemo walimu wanaofanya vizuri katika ufundishaji wa baadhi ya masomo, ikiwemo fizikia.

“Pia kuna shule zinazofanya vizuri, ikiwemo Mazinde Juu, ambazo zinaweza kusaidia walimu wetu kwa kuwa zina uwezo wa kuambukiza umahiri huo kwa walimu wa shule za Serikali. Aidha, tuna Chuo cha Korogwe ambacho tunaweza kukitumia kuongeza umahiri kwa walimu wetu,” anasema.

Katika kuhakikisha wanafunzi wanapata uelewa wa kutosha wa masomo hayo, mafunzo kwa vitendo yataanza kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza, ili wanapofika kidato cha tatu wawe na umahiri unaotakiwa, na wanapofika kidato cha tatu na nne wasipate changamoto yoyote.

Ushirikiano na shule binafsi

Katika kukabiliana na uhaba huu, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali Tanzania (Tamongosco), Benjamin Nkonya, anasema wameingia makubaliano na Serikali yatakayoruhusu Serikali kutumia miundombinu ya shule binafsi kwa ajili ya kufundisha wanafunzi wake.

Ili kutekeleza hilo, kuanzia Februari 18 mwaka huu, wamekubaliana kuzunguka nchi nzima na Wizara ya Elimu kuwaeleza wamiliki wa shule juu ya ushirikiano huo, ili kupeleka baadhi ya wanafunzi katika shule zao na kuwalipia ada.

“Kama ilivyo KCMC, ni mali ya kanisa lakini madaktari na vifaa tiba vinatolewa na Serikali, na shule itakuwa hivyo hivyo. Serikali itagharamia wanafunzi wake na sisi tutatoa elimu, na hii tumerithi kutoka Netherland,” anasema.

Kupitia ushirikiano huo, anaamini kuwa tatizo la maabara litaondoka kwa sababu maabara nyingi katika shule za binafsi zinatumika kwa asilimia 70 pekee, na hivyo wanafunzi wa Serikali watakapopelekwa, itafanya maabara hizo kutumika kwa asilimia 100.

Baby Massawe kutoka Sekondari ya Makiidi anataka vifaa viongezwe, ili kuruhusu kila mwanafunzi kuwa na kifaa chake badala ya kukaa katika makundi, jambo linalofanya wengine wasielewe vizuri.

Emmanuel Godfrey kutoka Shule ya Sekondari Mraokeryo anasema licha ya kuwapo kwa chumba hicho kimoja cha maabara, matamanio ni kila somo kuwa na maabara yake ili wajifunze vizuri na kuelewa kwa ufanisi.

Yusuph Immam kutoka Shule ya Sekondari Motuburu anasema kusoma kwa vitendo kunawasaidia kuelewa zaidi kile wanachofundishwa, huku akitaka uboreshaji zaidi wa maabara na vifaa vinavyohitajika ili kuongeza wigo wa kujifunza.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Reuben Kwagilwa, anasema Serikali inahakikisha shule zinazojengwa sasa zinakuwa na miundombinu yote inayohitajika, ikiwemo maabara.

Hadi sasa, katika awamu ya sita ya uongozi, shule 1,300 zimejengwa zikiwa na miundombinu yote, ikiwemo maabara tatu za sayansi na moja ya miamba na jiografia, huku baadhi zikiwa na maabara za Tehama.

“Shule hizo si za kawaida, kwani kila moja ina madarasa 22, mabweni 12, nyumba za walimu nane, bwalo kubwa la chakula, chumba cha Tehama, na maabara nne. Shule zote zilizojengwa katika kipindi hiki zina maabara,” anasema.

Anasema hayo wakati bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ya mwaka 2025/2026 inaonesha kuwa Serikali imepanga kufanya umaliziaji wa maboma ya maabara 350 pamoja na ununuzi wa vifaa na kemikali za maabara katika shule mpya 300 za sekondari.

Hilo linakwenda kufanyika wakati ambapo Serikali ilikuwa imenunua na kusambaza kemikali za maabara katika shule za sekondari za kata 231, pamoja na vifaa vya maabara kwa shule 486 vilivyonunuliwa katika awamu mbili.

“Vifaa vya awamu ya kwanza vilisambazwa katika shule 231, zikiwemo shule nane kati ya 26 za mikoa za wasichana. Vifaa vya maabara na kemikali kwa awamu ya pili kwa ajili ya shule 255 zilizobaki vinatarajiwa kupokelewa na kusambazwa kabla ya Juni 30, 2025,” ilieleza bajeti hiyo.