Mahakama yakataa madai dhidi ya Tume ya Jaji Chande -4

Dar es Salaam. Katika sehemu ya mwisho ya mapitio ya uamuzi wa shauri la kupinga Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya ghasia na uvunjifu wa amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Mahakama imetoa uamuzi wake.

Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam katika uamuzi huo uliotolewa na Jaji Awamu Mbagwa baada ya kuchambua hoja za pande zote ilitupilia mbali shauri hilo na kuhalalisha tume hiyo. Hivi ndivyo Jaji Mbagwa alivyosema:

“Katika maombi haya, waombaji wanapinga uteuzi wa makamishna kwa misingi ya kutokuwa halali, kutokuwa na busara, nia mbaya, upendeleo, na matumizi mabaya ya hiari.

“Waombaji wamehoji uhalali wa tume kwa misingi mitatu, yaani jina la tume kuitwa, Tume Huru ya Kufanya Uchunguzi,  kwamba haliko kwa mujibu wa sheria. Na kwamba suala linalotakiwa kuchunguzwa halijabainishwa mahsusi na makamishna hawakuapishwa.

“Kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi, ndicho kinampa Rais mamlaka ya kuunda tume na kuteua makamishna.

“Kinafafanua mamlaka ya Rais na mazingira ambayo anaweza kuunda tume. Kifungu kidogo cha (1) hakibainishi idadi wala sifa za makamishna wanaopaswa kuteuliwa

“Hivyo, kinaacha mamlaka ya hiari kwa Rais kuteua makamishna kulingana na asili na mahitaji ya suala litakavyochunguzwa.

“Pia, kifungu hicho hakitoi majina ya tume ambazo Rais anaweza kuunda chini ya kifungu hicho. Katika muktadha huo, Rais ana wajibu wa kuipa tume jina analoona linafaa.  

“Nimesoma Gazeti la Serikali (kiambatisho cha kwanza kilichowasilishwa na mawakili wa wajibu maombi, kutoka ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali -OSG1) lililoitangaza tume hiyo  linasema:

“Taarifa inatolewa kwa umma kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameunda Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Ghasia na Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2025 na kuwateua wajumbe wafuatao kuwa Makamishna wa Tume hiyo.”

Waombaji hawakuweza kuieleza Mahakama hii walipata wapi jina la Tume Huru ya Kufanya Uchunguzi. 

“Walidai kwamba, suala la kuchunguzwa halijabainishwa mahsus, hivyo ni kinyume na Kifungu cha 3(2) cha Sheria. Bila kuzunguka sana, hoja za waombaji hazina msingi na hazijathibitishwa.

“Kutoka katika Gazeti la Serikali, ni dhahiri kwamba suala la kuchunguzwa limebainishwa vizuri, ni wazi kwamba tume imekusudiwa kuchunguza matukio ya ghasia na uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025.

“Inahitaji muujiza au akili ya ziada kukubaliana na waombaji kwamba suala la kuchunguzwa haliko wazi. Kwa mtizamo wangu, suala (la kuchunguzwa) kama ilivyoelezwa katika Gazeti la Serikali ni mahsusi na linakidhi matakwa ya kifungu cha 3(2) cha Sheria.

“Kuhusu kuapishwa kwa makamishna, sioni umuhimu wowote wa kujadili suala hili kwa sababu maombi haya kimsingi yanapinga uteuzi wa makamishna na uendeshaji wa Tume.

“Kwa mujibu wa Kifungu cha 7 (cha Sheria ya Tume za Uchunguzi), sharti la kula kiapo ni hatua inayofuata baada ya uteuzi. Hivyo, dai hili limewekwa mahali pasipostahili.

“Kwa kuzingatia hayo yaliyoelezwa hapo juu, ninaamua kwamba waombaji wameshindwa kuthibitisha madai ya kutokuwa halali katika uteuzi wa makamishna.

“Waombaji walidai kutokuwapo kwa busara, kufanywa kwa nia mbaya, upendeleo na matumizi mabaya ya mamlaka ya hiari katika uteuzi wa makamishna. Walidai kwamba, makamishna wote ni watumishi wa zamani wa umma wenye wastani wa umri wa zaidi ya miaka sitini.

“Kwa mujibu wa waombaji, mamlaka ya uteuzi ilipaswa kujumuisha wawakilishi kutoka asasi za kiraia na za kidini kama vile Chama cha Madaktari, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).

“Walidai kwamba mamlaka ya uteuzi ilipaswa kujumuisha kizazi cha vijana (Gen Z) ambao hawana ajira na ambao walikuwa wameathirika zaidi na ghasia zinazodaiwa kutokea.

“Zaidi waombaji walidai kwamba, uwepo wa waziri wa zamani wa ulinzi, ambaye ni mlalamikiwa wa tisa (Tax) , unaashiria uwepo wa upendeleo kwa upande wa Tume.

“Katika maelezo yao yote hakuna mahali popote walipodai kutokuwa na uaminifu au kuwa na upendeleo kwa kamishna yeyote. Kinyume chake, wanakiri kwamba, makamishna wote wametumikia umma kwa heshima katika nyadhifa mbalimbali.

“Kama nilivyoeleza hapo awali, kifungu cha 3 cha sheria hakijaweka sifa za makamishna. Ni muhimu pia kubainisha kwamba, wajibu wa tume si kuhukumu nani anapaswa kulaumiwa, bali kukusanya ushahidi ili kubaini ukweli.

“Tume kuundwa na wajumbe wenye umri wa zaidi ya miaka 60 haimaanishi kwamba hawawezi kusikiliza na kupokea maoni au mapendekezo kutoka kwa makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwamo kizazi cha vijana ambacho waombaji wanadai ndicho kilichoathirika zaidi.

“Hoja kwamba mamlaka ya uteuzi ilipaswa kujumuisha vijana wasio na ajira haina msingi, Tume haikuundwa ili kutoa fursa za ajira bali kuchunguza ukweli wa matukio yanayodaiwa kutokea.

“Hivyo, mtu yeyote mwenye busara angemteua mtu anayeweza kuchunguza suala hilo kwa ufanisi na kwa weledi.

“Waombaji wanakiri kwamba, baadhi ya makamishna walihusika katika Tume ya awali iliyojulikana kama Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai,  na hakukuwa na madai yoyote ya upendeleo dhidi ya mmoja wao.

“Isitoshe hawakutoa madai ya rekodi mbaya dhidi ya kamishna yeyote.

“Kwa hiyo, kinyume na mtazamo wa waombaji, ni hitimisho la Mahakama hii kwamba, kwa kuzingatia uzoefu mkubwa na upeo mpana wa makamishna katika nyanja mbalimbali za utumishi wa umma, mtu mwenye busara angepongeza uteuzi wa makamishna hao. 

“Ni muhimu pia kubainisha kwamba, wakati wa kutekeleza majukumu yao, makamishna wanaongozwa na masharti ya sheria. Kwa mujibu wa vifungu vya 7 na 9 vya sheria husika, kila kamishna anatakiwa kula kiapo cha kutekeleza majukumu yake kwa uaminifu na bila upendeleo.

“Hivyo basi, mpaka ithibitishwe vinginevyo, madai ya waombaji dhidi ya makamishna yanabaki kuwa dhana tu ambazo Mahakama hii haiwezi kuzifanyia kazi.

“Kwa kuzingatia yote yaliyoelezwa hapo juu, ninabaini kwamba, madai ya waombaji ni dhana na mawazo tu kuliko kuwa na uhalisia. Ninatupilia mbali maombi haya kwa kukosa msingi, kwa kuwa hili ni suala la masilahi ya umma, sitoi amri yoyote kuhusu gharama.”

Hata hivyo,  waombaji Rosemary Mwakitwange, mawakili Edward Heche na Deogratius Mahinyila na wakili wao Hekima Mwasipu walieleza kutokuridhishwa na uamuzi huo.

Mbali na kutokuridhishwa na uchambuzi na uamuzi  katika hoja zao nyingine, pia walieleza kuwa, kuna hoja Mahakama haikuziamua kabisa ambazo ni  wajibu maombi kutokuwasilisha uthibitisho wa wajibu maombi kula kiapo na uhalali wa Tangazo la Serikali kuitangaza tume hiyo, lililowasilishwa mahakamani

Hivyo, walisema kuwa wanakata rufaa Mahakama ya Rufani kufupinga uamuzi huo.

Pamoja na hatua nyingine wanazokusudia kuzichukua Mahinyila alisema kuwa, kwa kuwa Mahakama imekataa hoja zao, sasa wanasubiri hiyo tume ije iwaeleze Watanzania kuwa ni nani aliyefanya mauaji na kwa amri ya nani.

“Tunaamini tume hii kwa jinsi ilivyoundwa na kwa aina ya wajumbe wake haiwezi kuja kusema hayo. Lakini, kama tume itafanya kazi ambazo tuliona kuwa haiwezi kuzifanya basi sisi tutakuwa waungwana tutaiomba radhi,” alisema Mahinyila na kusisitiza kuwa, hawatarajii kabisa kupata uhalisia wa matukio hayo kutoka kwa tume hiyo.