Kongole Wizara ya Maji kwa mafanikio ya programu ya WSDP

Na: Dk. Reubeni Lumbagala

Wizara ya Maji inatekeleza programu mbalimbali za kimaendeleo zenye lengo la kuboresha usambazaji wa maji kwa wananchi wake na kufanikisha miradi mingine ya umwagiliaji ambayo ni kichochea muhimu kwa ustawi wa shughuli za kiuchumi kama kilimo, viwanda na huduma nyingine za kijamii.

Miongoni mwa mipango inayosimamiwa na Wizara ya Maji yenye lengo la kuchochea kasi ya usambazaji wa maji kwa wananchi ni Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (Water Sector Development Programme – WSDP) ambayo sasa imetimiza miaka ishirini tangu ilipozinduliwa mwaka 2006. 

Machi 16 hadi Machi 22, 2026, Wizara ya Maji inaadhimisha Wiki ya Maji ambapo kilele chake ni Machi 22 ambayo ni Siku ya Maji Duniani. Katika Wiki ya Maji, Wizara ya Maji inaratibu makongamano, mijadala na maonyesho mbalimbali yenye lengo la kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala mbalimbali ya maji na kuonyesha mafanikio yaliyofikiwa katika usambazaji wa huduma ya maji.

Machi 17, 2026, Waziri wa Fedha, Balozi Khamisi Omar alishiriki ufunguzi wa Mkutano wa Mapitio ya Pamoja ya Sekta ya Maji (Joint Water Sector Review – JWSR) uliofanyika katika Ukumbi wa Mkutano wa Cate Convention Centre, mjini Morogoro ambapo aliipongeza Wizara ya Maji kwa mafanikio ya usambazaji wa maji ikiwemo programu ya WSDP. 

Kwa mujibu wa Balozi Omar, programu ya WSDP imefanikiwa kuboresha upatikanaji wa maji ambapo awali maeneo ya mjini yalikuwa yakipata maji kwa asilimia 74 lakini sasa maji yanapatikana kwa asilimia 92.5. Kwa maeneo ya vijijini, upatikanaji wa maji ulikuwa asilimia 54 lakini sasa upatikanaji wa maji umefikia asilimia 85.2.

Ni jambo la faraja kuona programu ya WSDP imeleta matokeo chanya katika miaka ishirini ya utekelezaji wake ambapo usambazaji wa maji kwa wananchi umeimarika sana. Kimsingi, usambazaji maji kwa wananchi kufikia asilimia 92.5 kwa maeneo ya mjini na asilimia 85.2 kwa vijijini ni mafanikio makubwa ya kupongezwa. Maji ni raslimali yenye mnyororo mkubwa wa thamani ikizingatia maji ni uchumi katika ulimwengu huu wa maendeleo.

Iko hivi: Maji yamefungamanishwa na sekta nyingine za kiuchumi kama kilimo, viwanda, migodi, uvuvi, ufugaji samaki, ambapo mafanikio ya maji yanagusa maendeleo ya sekta nyingine moja kwa moja. Kwa upande wa Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amesema vijiji 10,758 vimeshapata maji ya uhakika huku vijiji 1,575 kati ya 12,333 vikiwa bado havijafikiwa na maji ya uhakika huku akisisitiza kuwa mpango wa serikali ni kufikisha maji kwa asilimia mia moja maeneo yote ya mjini ma vijijini.

Ni faraja kuona serikali ikionyesha utashi mkubwa wa kisiasa kuhakikisha usambazaji wa maji kwa wananchi unafikiwa kikamilifu. Mathalani, kwa mujibu wa Balozi Omar, katika kipindi cha mwezi Januari hadi Disemba 2025, serikali imetumia shilingi bilioni 883.93 katika utekelezaji wa miradi ya maji na usafi wa mazingira. Ikumbukwe kuwa, bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ilikuwa shilingi trilioni 1.01, jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya nchi yetu huku fedha nyingi zikielekezwa katika kugharamia miradi ya maendeleo ya huduma za maji.

Wiki ya Maji inayoendelea inachagizwa na kaulimbiu isemayo “Raslimali za Maji na Usawa wa Kijinsia.” Ni muhimu sana wananchi kushiriki kutunza vyanzo vya maji kwa maendeleo endelevu. Vilevile, ni muhimu kuhakikisha miundombinu ya maji inatunzwa bila kuharibiwa au kuhujumiwa. Pia, taasisi na watu binafsi wanaodaiwa fedha na mamlaka za maji wahakikishe wanalipa madeni hayo ili kuzijengea uwezo mamlaka hizo na Wizara ya Maji kuboresha zaidi usambazaji wa maji kwa wananchi. Maji ni uhai, maji ni afya, maji ni uchumi na maji ni maendeleo. Tafakari.

Maoni: 0620 800 462