Wanne wauawa kwa tuhuma za uhalifu, kufumaniwa Mbeya

Mbeya. Watu watano wamefariki dunia jijini Mbeya, wakiwamo wanne wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu ikiwemo uporaji na upigaji nondo nyakati za usiku, na mmoja ameuawa kwa fumanizi.

Hivi karibuni gazeti la Mwananchi liliripoti uwepo wa makundi ya uhalifu katika maeneo mbalimbali jijini Mbeya, siku chache baada ya mwandishi wa TV Imaan, Rashid Mkwinda, kuvamiwa, kujeruhiwa na kuporwa.

Taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga, imesema matukio yametokea nyakati tofauti katika Uyole Sokoni jijini Mbeya na Madibira wilayani Mbarali. Machi 15, kundi la wananchi waliodaiwa kujichukulia sheria mkononi liliwazingira watu wanaotuhumiwa kujihusisha na uporaji na upigaji nondo, waliokuwa wamejificha ndani ya nyumba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP Benjamin Kuzaga akionesha baadhi ya vitu vilivyokamatwa kufuatia operesheni na doria iliyofanywa na jeshi hilo mkoani humo.

Jeshi la Polisi kupitia kikosi maalumu kilifika na kuwaokoa watuhumiwa sita, lakini wanne walifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu, ambao ni Erick Nassoro, Meshack Joseph, Abdalah Ngoliyan na Asajile Isack. Wawili waliopona ni Raksi Hamis na Paschal Aron, ambao wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi.

Watuhumiwa hao walikiri kuhusika katika matukio kadhaa ya uhalifu ikiwemo mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi maeneo ya Isyesye, Iganzo, Hayanga, Manga Veta, Ilomba na Uyole. Walikutwa pia na mali walizoiba, ikiwemo magodoro, redio, TV, mazulia, pazia, majiko ya gesi na mitungi. Jeshi la Polisi linasisitiza wananchi kufika kituo cha polisi kwa utambuzi wa mali zao.

Kamanda Kuzaga pia amesema Jeshi linashikilia Zakaria Golan mkazi wa Magigiwe kwa tuhuma za mauaji ya Zengo Somola, yaliyotokea Machi 11, 2026 eneo la Madibira jijini hapa, akituhumiwa kufumania na kumshambulia kwa  fimbo kichwani.

Jeshi la Polisi linaendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa kufanya operesheni, misako na doria katika maeneo mbalimbali ili kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu. Wananchi waliotajwa wanatakiwa kuacha mara moja matukio ya uhalifu na kulinda rasilimali za Taifa, pamoja na kufuata utaratibu wa umiliki halali wa silaha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP Benjamin Kuzaga akionesha baadhi ya vitu vilivyokamatwa kufuatia operesheni na doria iliyofanywa na jeshi hilo mkoani humo

Kauli za wenyeviti wa mitaa: Upendo Samuel, Mwenyekiti wa Mtaa wa RRM, amesema Jeshi la Polisi limekuwa likitoa ushirikiano kwa jamii na doria za mara kwa mara, akipongeza jitihada zao bila kujali usiku.

Keneth Mwakambonja, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwantengule Kata ya Isyesye, aliomba kuwepo kliniki ya mahakama kutoa elimu kwa wananchi. Henry Kimkoma, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mapelele Kata ya Ilemi, amesisitiza kuwalea watoto kimaadili na kuwaelekeza nyumba za ibada, huku akipongeza ushirikiano wa Jeshi la Polisi katika kuzuia matukio ya uhalifu.