Radi yaua wanafunzi watatu Shule ya Msingi Msongola Dar

Dar es Salaam. Wanafunzi watatu wa Shule ya Msingi Msongola, iliyopo  Kivule wilayani Ilala jijini Dar es Salaam, wamefariki dunia kutokana na kupigwa na radi.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amethibitisha tukio hilo na amesema tukio hilo limetokea leo Jumatano Machi 18, 2026.

“Ni kweli wanafunzi wetu watano walikuwa wakicheza shuleni wamepigwa na radi watatu wakafariki papo hapo, hawa wengine wanaendeleana matibabu,” amesema Muliro huku akiongeza kuwa wanafunzi wawili wamekimbizwa hospitali kwa ajili ya matibabu.

Awali, ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Kivule, Ojambi Massaburi, ilitoa taarifa hiyo huku ikituma salamu za rambirambi kwa ndugu jamaa na marafiki.

“Mbunge anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, akiwaombea faraja, uvumilivu na nguvu ya moyo katika wakati huu wa huzuni,” imeeleza taarifa hiyo.