Dar es Salaam. Katika siku za hivi karibuni Mkoa wa Dar es Salaam umekuwa miongoni wa inayopata mvua za mara kwa mara, maji kujaa barabarani na kuleta usumbufu kwa watumiaji imekuwa ni matokeo hasi yanayoshuhudiwa.
Kujaa maji katika baadhi ya maeneo imekuwa ni jambo linalojirudia licha ya maboresho kufanyika ikiwemo ujenzi wa kisasa.
Hali hiyo imewafanya wananchi kutaka suluhisho la kudumu kutafutwa ili mvua zinaponyesha isiwe sababu ya kusimama kwa baadhi ya shughuli ikiwemo usafirishaji.
Wengine, walitaka udhibiti wa utupaji taka holela ili kulinda mitaro inayopitisha maji wakati wa mvua.
“Tusiangalie watu wakigeuza mitaro kuwa dampo wachukuliwe hatua, inaathiri sana kwani mvua zinaponyesha inasababisha watu kupoteza mali zao kutokana na kuharibika,” amesema Malick Bale, mkazi wa Temeke.
Amesema baadhi ya maeneo ikiwemo Sokota yamekuwa yakijaa maji miaka yote licha ya pembeni kuwa na mitaro ambayo kwa bahati mbaya maji yanayoingia katika mitaro hiyo hutuama.
Mwonekano wa moja barabara ikiwa imejaa maji jijini Dar es Salaam ambapo utupaji taka hovyo kwenye mitaro umetajwa kuwa chanzo cha kadhia hiyo. Picha na Mtandao
“Imeziba, hakuna yanapokwenda, wakati mwingine hali hii husababishwa na ujenzi unaofanyika katika baadhi ya maeneo, wakiziba mitaro hawaweki njia mbadala kwa hiyo haya maji yakifika mbele yanakosa kwa kwenda yanaingia barabarani,” amesema.
Wakati Malick akiyasema hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Petsa International inayojihusisha na ujenzi na ushauri elekezi, Jeremiah Charles amelezea ni kwa namna gani jambo hilo linaweza kuepukika hata baada ya kufanya maboresho ya miundombinu.
Amesema kabla ya kufanya ujenzi wowote wa barabara ni vyema kujua eneo ambalo maji yanaelekea ili imsaidie mkandarasi kufanya uamuzi wakati wa ujenzi.
Hilo linapaswa kufanyika tangu awali mradi unapofanyiwa design (muundo) ili kuhakikisha hakuna athari za baadaye zitakapotokea.
“Ukikuta upanuzi wa barabara unafanyika na mitaro kuzibwa huwa inafanywa vile kwa muda na baadaye wanarudisha katika hali ya kawaida inategemeana na mradi. Lakini kama makandarasi wangekuwa wanaweka mbadala wa mitaro wakati wakijenga hili lisingetokea,” amesema.
“Sasa kama hukupewa fedha ya kuweka mitaro mbadala utalazimika kujenga barabara ndiyo uje kujenga mitaro, sasa mvua ikikukuta uko katika ujenzi huo ndiyo maji yatajaa na kuleta usumbufu kwa watu,” amesema.
Kusafisha mitaro ni moja ya jambo ambalo limependekezwa na Safina Mbarouk huku akiita njia hiyo kama kutengeneza njia ya kuaminika ya maji.
“Siyo tu wakati wa mvua, muda wote ikiwezekana watu ambao mbele yao kuna mitaro wasimamiwe ipasavyo, ukikutwa ni mchafu wawajibishwe, waone mtaro kama sehemu ya nyumba yao, tukipata uwajibikaji wa kila mtu tunamaliza kero hii,” amesema.
Athari mitaro kuzibwa wakati wa ujenzi
Wakati baadhi ya maeneo mitaro ikionekana kufungwa ili kutanua barabara kupisha ujenzi inatajwa kuwa moja ya bomu linaloweza kuleta athari baadaye.
Mhandisi David Sembuyagi kutoka kampuni ya Ujenzi Bulkbuild amesema miongoni mwa athari zinazoweza kutokea ni uharibifu wa barabara yenyewe kwani maji yasipopata njia, huingia chini ya lami.
“Hii husababisha lami kuanza kutoa mashimo na kupasuka haraka. Badala ya barabara kudumu miaka 20, inaweza kuanza kuharibika ndani ya miaka miwili au mitatu jambo ambalo ni hasara kwa kodi za wananchi,” amesema.
Amesema kuwapo kwa hali hiyo kunaweza kuchochea ongezeko la mafuriko ya ghafla kwani kuziba mitaro kunapunguza uwezo wa ardhi kupokea maji ya mvua.
Hii itafanya kwa miaka ijayo, mvua ndogo itakaponyesha kusababisha maji kuingia kwenye nyumba na biashara za watu kwa sababu barabara itakuwa inafanya kazi kama bwawa badala ya njia ya usafiri.
“Lakini maji yanayotuama barabarani kwa muda mrefu yanakuwa mazalia ya mbu na vyanzo vya magonjwa kama kipindupindu na homa ya matumbo. Pia, maji hayo yakichanganyika na mafuta ya magari na takataka, huchafua vyanzo vya maji ya chini ya ardhi ambavyo wakazi wengi wa Dar es Salaam wanategemea kupitia visima,” amesema.
Mwonekano wa moja barabara ikiwa imejaa maji jijini Dar es Salaam ambapo utupaji taka hovyo kwenye mitaro umetajwa kuwa chanzo cha kadhia hiyo. Picha na Mtandao
Amesema hali hiyo huenda mbali zaidi na kusababisha kushuka kwa thamani ya ardhi na majengo kwani mafuriko ya mara kwa mara hupoteza mvuto kwa wawekezaji.
“Ikiwa kiwanja chako kipo jirani na barabara ambayo haina mifereji imara, thamani ya nyumba yako inaweza kushuka kwa sababu wapangaji au wanunuzi wataogopa kero ya maji. Hali hii huweza kuleta migogoro ya kisheria kwani hapo baadaye, Serikali inaweza kulazimika kubomoa baadhi ya miundombinu au nyumba ili kupitisha mifereji mipya,” anasema.
Amesema hatua za muda zinazoweza kutumika wakati wa ujenzi ni kuweka mifereji ya muda ili kutoa maji yanayotuama kutokana na kizuizi cha vifusi au mitaro iliyozibwa kwa ujenzi.
Kuhakikisha usimamizi wa vifusi kuhakikisha mchanga, kokoto, na udongo unaotokana na ujenzi haurundikwi karibu na vituo au njia za maji, kwani mvua inaponyesha huvisukuma na kuziba mifereji iliyopo.
