Sera ya vijana EAC yatia matumaini, sauti yao bado changamoto

Dar es Salaam. Wakati nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zikiendelea kuboresha sera ya vijana ya 2025–2030, wadau wamesema inaleta matumaini kwa maendeleo ya vijana, lakini bado kuna changamoto ya ushirikishwaji na utekelezaji.

Hayo yameelezwa leo Machi 18, 2026 katika mkutano wa kikanda wa afya ulioandaliwa na Baraza la Wabunge Vijana wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Bunge la Afrika Mashariki na Mtandao wa Vijana wa Afrika Mashariki, ukilenga kuanzisha utekelezaji wa pamoja wa ajenda za afya ya uzazi na haki zake (SRHR) chini ya sera hiyo.

Mkutano huo umewakutanisha wabunge wa EALA, viongozi wa vijana, mashirika ya kiraia, wizara na wadau wa maendeleo, ukilenga kuratibu juhudi zilizopo, kuandaa mwongozo wa utekelezaji wa SRHR na kuanzisha kamati za kitaifa kusimamia utekelezaji.

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Machano Ali Machano.

Mwakilishi wa vijana kutoka EANNASO, Leticia Mswaki, amesema sera hiyo ni nyenzo muhimu ya kuwapa vijana nafasi ya kushiriki katika maamuzi, huku ikilenga kuboresha afya ya uzazi, afya ya akili na fursa za ajira na elimu. Hata hivyo, amesema bado vijana wanakosa sauti, huku mimba za utotoni na ukosefu wa mwelekeo wa maendeleo ukiendelea kuwa changamoto.

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Machano Ali Machano, amesisitiza umuhimu wa vijana kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa sera hiyo, akibainisha kuwa mafanikio yatategemea ushiriki wao katika maamuzi, hasa kwenye bajeti za wizara zinazowahusu.

Mratibu wa Sharp Project kutoka Kenya, Dorothy Okyemo, amesema sera hiyo inaleta fursa ya maendeleo ya kikanda, lakini changamoto kama Virusi vya Ukimwi, mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia bado zinaathiri vijana wengi. Amesisitiza umuhimu wa huduma za afya ya uzazi kupatikana bure kwa wajawazito na upatikanaji wa dawa muhimu.

Mbunge wa Kenya, Naomi Wako, amesema sera hiyo inaweza kuwa kinga dhidi ya changamoto hizo, hususan kwa wasichana, huku mwakilishi kutoka Uganda, Jarc Tusiime, akisisitiza umuhimu wa serikali kuweka bajeti maalumu kwa vijana na kuondoa vikwazo kama kodi kwenye taulo za kike.

Mwakilishi wa vijana Amina Boru amesema sera hiyo itawasaidia vijana kudai haki zao na kushiriki maendeleo, akisisitiza kuwa vijana wanahitaji kushirikishwa sasa, si baadaye.

Kwa ujumla, wadau wanakubaliana kuwa sera ya vijana ya EAC ina uwezo mkubwa wa kuleta mageuzi, lakini mafanikio yake yatategemea utekelezaji wake na ushiriki wa vijana.