Ajali yaua wanne Rombo wakitokea matembezini

Rombo. Vijana wanne ambao ni mafundi ujenzi wamefariki dunia baada ya pikipiki waliyokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na gari aina ya Noah eneo la Shimbi, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.

Vijana hao wenye umri kati ya miaka 19-20 ni wakazi wa Kijiji cha Shimbi Masho, Kata ya Kwa Ndele, walikuwa wanatokea matembezini.

Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na ajali hiyo leo Machi 18,2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema imetokea  saa tisa usiku wa kuamkia leo.

Amewataja waliofariki duni kuwa ni pamoja na Pascal Kisheo, Devis Kitali, Nobet Mrema na Emmanuel Kitali, wote wakazi wa Kijiji cha Shimbi Masho.

Aidha, Kamanda Maigwa amesema wanamshikilia dereva wa gari kwa hatua zaidi za kisheria.

Akizungumzia ajali hiyo, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Peter Kimario amesema ilitokea usiku baada ya pikipiki waliyokuwa wanasafiria kugongana uso kwa uso na Toyota Noah na kusababisha vifo vya vijana hao.

“Hawa vijana walikuwa wanapata kinywaji kwenye moja ya baa iliyopo hapa kijijini, baada ya kumaliza kunywa waliondoka katika ile baa wakiwa wamelewa na walibebana mshikaki wote wanne kwenye pikipiki moja,” amedai Mwenyekiti huyo na kuongeza;

“Inadaiwa kabla ya kufika barabara ya Shimbi, waliona gari mbele yao aina ya Noah na inaonekana kwa sababu walikuwa wamekunywa na pombe ipo kichwani, walikuwa upande ambao sio wao, dereva wa  Noah alivyoona wapo kwenye upande wake alijaribu kuwakwepa kurudi upande mwingine nao wakamfuata kulekule wakajigonga kwenye ile Noah,” amedai Kimario.

Amesema miili ya vijana hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Huruma, iliyopo wilayani humo.

Aidha, amewataka vijana kutotumia vyombo vya moto wakiwa katika hali ya ulevi kwa sababu ni hatari na inagharimu maisha yao na kuwaachia mzigo familia ambayo inawategemea.