Zaidi ya asilimia 70 wafanyakazi Muhimbili ni wanawake

Dar es Salaam. Zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ni wanawake, hatua inayodhihirisha nafasi kubwa waliyonayo katika utoaji wa huduma za afya nchini.

Takwimu hii ina ujumbe mpana kwa Tanzania siyo tu kwenye afya, bali maendeleo ya Taifa kwa ujumla, ikionyesha wazi kuwa wanawake ndio uti wa mgongo wa sekta ya afya.

Takwimu hizi pia ni ishara ya maendeleo ya usawa wa kijinsia, pia inaibua hitaji la kuwekeza zaidi kwa wanawake, hasa kwenye afya ya akili, Uongozi, mazingira bora ya kazi, lakini pia inaonyesha kuwa uchumi na maendeleo ya Taifa yanategemea wanawake kwa kiwango kikubwa.

Akizungumza katika hafla ya mafunzo kwa watumishi wanawake wa hospitali hiyo yaliyofanyika leo Jumatano, Machi 18, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Dk Delila Kimambo amesema kati ya wafanyakazi 3,000 waliopo, zaidi ya 2,000 ni wanawake, hali inayoifanya hospitali hiyo kuwa kinara wa ushiriki wa wanawake katika sekta ya afya.

Amesema takwimu hizo zinaonyesha wazi kuwa wanawake si washiriki tu wa maendeleo bali ni nguzo muhimu katika utoaji wa huduma bora za afya.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, MNH Dk Delila Kimambo akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo.

“Wanawake wetu wanafanya kazi katika kada mbalimbali muhimu kama madaktari bingwa bobezi, wauguzi, wafamasia, wataalamu wa maabara, watafiti, wahandisi na hata kushika nafasi za uongozi. Mafanikio ya Muhimbili hayawezekani bila mchango wao mkubwa,” amesema Dk Kimambo.

Ameeleza kaulimbiu ya kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayosisitiza haki na usawa kwa wanawake na wasichana ni mwongozo muhimu unaopaswa kutekelezwa kwa vitendo katika taasisi zote, ikiwemo sekta ya afya.

Kwa mujibu wa Dk Kimambo, hospitali hiyo inaendelea kujenga mazingira jumuishi yanayowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya uongozi, kukuza taaluma zao na kufanya tafiti za kisayansi.

“Haki na usawa siyo jambo la hiari, ni msingi wa maendeleo endelevu ya taifa letu. Tunapaswa kuhakikisha kila mwanamke anapata fursa sawa ya kuonyesha uwezo wake,” amesema.

Hata hivyo, amekiri kuwa bado kuna changamoto zinazohitaji juhudi za pamoja ili kufikia usawa kamili, akisisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo vya kijamii, kiuchumi na kiutawala vinavyoweza kuwazuia wanawake kufikia malengo yao.

Sambamba na hilo, Mtaalamu wa Saikolojia, Sophia Sanga amesema tafiti zinaonyesha kuwa wanawake huathiriwa na msongo wa mawazo karibu mara mbili zaidi kuliko wanaume.

Wafanyakazi wanawake wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wakiwa kwenye matembezi wakiadhimisha siku ya wanawake duniani

“Mwanamke mara nyingi anakuwa na majukumu mengi kwa wakati mmoja akiwa mama, mlezi, mfanyakazi na wakati mwingine kiongozi. Hali hii inaweza kuongeza hatari ya changamoto za afya ya akili,” amesema Sophia.

Ameongeza kuwa mabadiliko ya homoni katika vipindi mbalimbali vya maisha ya mwanamke kama ujauzito, baada ya kujifungua na wakati wa kukoma hedhi pia huathiri hali ya hisia na afya ya akili.

“Wakati mwingine mwanamke anaweza kujikuta akiwa na huzuni, hasira au kukosa usingizi bila sababu kubwa inayoonekana. Hii ni hali inayohitaji uelewa na msaada,” amesema.

Aidha, amesema mitandao ya kijamii imeongeza shinikizo kwa wanawake wengi kujilinganisha na viwango visivyo halisi vya urembo, hali inayoweza kusababisha kutoridhika na miili yao na hata matatizo ya ulaji.

Kutokana na hali hiyo, amesisitiza umuhimu wa jamii kuzungumzia afya ya akili kwa uwazi na kutoa msaada kwa wanawake wanaokumbana na changamoto hizo.

Wafanyakazi wanawake wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wakiwa kwenye matembezi wakiadhimisha siku ya wanawake duniani

Katika hatua ya kukabiliana na changamoto hizo, Dk Kimambo amesema wanawake zaidi ya 1,500 wa Muhimbili wamepatiwa mafunzo ya namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo, kupanga maisha ya familia na kazi pamoja na usimamizi wa fedha.

Amesema pamoja na mchango mkubwa wa wanawake katika hospitali hiyo, bado kuna changamoto za maadili katika utoaji huduma zinazohitaji kuimarishwa.

“Ni muhimu kuwa na kauli nzuri kwa wagonjwa. Wanakuja wakiwa na matatizo, hivyo sisi tunapaswa kuwa sehemu ya faraja yao,” amesema.

Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya wanawake na wanaume ni muhimu katika kujenga mazingira yenye usawa na kuboresha utoaji huduma za afya.

Akihitimisha, Dk Kimambo amewapongeza wanawake wa Muhimbili kwa kujitolea kwao, akisema licha ya changamoto wanazokutana nazo, wameendelea kuwa mstari wa mbele katika kuokoa maisha ya Watanzania.

“Nyinyi ni jeshi kubwa la kuokoa maisha kila siku. Michango yenu inaonekana siyo tu hospitalini hapa bali pia katika maendeleo ya sekta ya afya na Taifa kwa ujumla,” amesema.