Morogoro. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko, amemuagiza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kuwasilisha maelezo ya kina kwa maandishi kuhusu kusuasua kwa ujenzi wa vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi (Veta) vinavyojengwa katika wilaya 64 nchini.
Agizo hilo limetolewa leo Jumatano Machi 18, 2026, wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi wa ujenzi wa chuo cha Veta katika Wilaya ya Gairo na imeelezwa kuwa kasi ya ujenzi bado hairidhishi.
Sekiboko amesema kamati inahitaji taarifa ya kina kuhusu maendeleo ya miradi hiyo pamoja na matumizi ya fedha zilizotengwa, kabla ya kuanza kwa Bunge la Bajeti la mwaka 2026/2027.
Amebainisha kuwa zaidi ya Sh100 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa vyuo hivyo katika wilaya mbalimbali.
“Kama kamati tunahitaji kupata taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa chuo hiki na vyuo vingine 64 vinavyojengwa nchini, pamoja na maelezo ya matumizi ya fedha zake kabla ya Bunge la Bajeti,” amesema Sekiboko.
Amesisitiza kuwa kukamilika kwa vyuo hivyo ni muhimu kwa wananchi wa maeneo ya pembezoni, wengi wao wakiwa hawana uwezo wa kugharamia elimu ya juu. Alieleza kuwa vyuo hivyo vitakuwa suluhisho kwa vijana wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari kwa kuwapatia ujuzi wa kujiajiri.
Muonekano wa majengo ya chuo cha mafunzo ya ufundi stadi VETA kinachojengwa katika wilaya ya Gairo mkoani Morogoro. Picha Hamida Shariff
Sekiboko ameongeza kuwa kamati yake haitakuwa tayari kuona ahadi ya Samia Suluhu Hassan ya kujenga chuo cha Veta katika kila wilaya ikikwama, akitaka hatua madhubuti zichukuliwe kuharakisha miradi hiyo.
“Tunataka kujua changamoto zilizopo na namna ya kuzitatua ili kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati. Ni lazima fedha zipatikane na kusimamiwa ipasavyo,” amesisitiza.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, mshauri elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM-BICO), Denis Msumba amesema ujenzi wa chuo cha Veta Gairo unahusisha majengo tisa katika awamu ya kwanza, huku maendeleo ya ujenzi yakiwa chini ya asilimia 45.
Ametaja majengo hayo kuwa ni pamoja na jengo la utawala, maktaba, karakana, madarasa, nyumba ya mkuu wa chuo, nyumba ya mlinzi na ukumbi wa mikutano.
Amesema mradi umezingatia pia mahitaji ya watu wenye ulemavu kwa kuweka miundombinu rafiki, hususan vyoo na maeneo mengine muhimu.
Mshauri elekezi kutoka chuo kikuu Dar es Salaam (UDSM – BICO) Denis Msumba akitoa taarifa Kwa kamati ya kudumu ya bunge ya elimu, utamaduni na michezo kuhusu ujenzi wa chuo cha mafunzo ya ufundi stadi VETA kinachojengwa katika wilaya ya Gairo, kamati hiyo imetembelea mradi huo leo macho 18. Picha Hamida Shariff
Kwa upande wake, Profesa Mkenda amesema amepokea maelekezo yote yaliyotolewa na kamati hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi pamoja na kutoa mrejesho katika vikao vya Bunge vitakavyofanyika Dodoma.
Naye mmoja wa wananchi wa Gairo, Amani Kobadi ameiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa chuo hicho akisema kitakuwa mkombozi kwa vijana wengi wanaokosa fursa ya kuendelea na masomo ya juu.
