Dk Tulia agusa wahitaji 204, misikiti 17 wagawiwa futari, masheikh watoa neno

Mbeya. Mbunge wa Uyole mkoani hapa, Dk Tulia Ackson, amerejesha kicheko kwa waumini 204 wa dini ya Kiislamu, wakiwemo wazee waishio katika mazingira magumu, kwa kutoa futari katika misikiti 17 iliyopo katika kata 13 jimboni kwake.

Hatua hiyo ni sehemu ya sadaka katika kuhitimisha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuelekea kuungana na Watanzania wengine kusherehekea Sikukuu ya Eid El Fitr.

Sadaka hiyo imekabidhiwa leo Jumatano, Machi 18, 2026, kwa Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Alhaji Sheikh Msafiri Njalambaha na Meneja wa Taasisi ya Tulia Trust, Jackline Boaz, kwa niaba ya Mbunge wa Uyole.

Jackline amesema futari hiyo imelenga makundi hayo kwa lengo la kurejesha tabasamu, lakini pia kuikumbusha jamii kuwatazama kwa jicho la upendo katika kuelekea kusherehekea Sikukuu ya Eid El Fitr.

“Tumeleta futari kidogo kwa niaba ya mbunge wenu Dk Tulia kwa ajili ya ndugu zetu walio kwenye mfungo wanaoishi katika mazingira magumu, ikiwemo mchele, unga wa sembe, maandazi, tende na sukari kwa ujazo tofauti tofauti,” amesema.

Amesema wanufaika ni walengwa walioteuliwa na mashekhe wa misikiti 17 kutoka Bonde la Uyole, huku kila msikiti ukitoa waumini 12 na kufanya idadi ya wahitaji kufikia 204.

“Tumekabidhi sadaka kwa Sheikh wa Mkoa, Msafiri Njalambaha, kwa niaba ya Dk Tulia. Tunaomba kwa dua zenu muendelee kumuombea kwani kwa sasa ana majukumu mengi ya kikazi na ameahidi akirejea atakuja kuwaona,” amesema.

Kauli ya viongozi wa dini

Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Msafiri Njalambaha amesema kwa niaba ya Waislamu wa kata 13 za Bonde la Uyole anashukuru Taasisi ya Tulia Trust kwa niaba ya Dk Tulia kwa hatua hiyo ya kugusa watu wenye maisha magumu.

“Dk Tulia si leo tu amefanya hilo, ni mwenendo wake tangu akiwa Mbunge wa Mbeya Mjini kugawa futari katika Msikiti Mkuu wa Mkoa, jambo ambalo ni mwenendo mzuri katika dini ya Kiislamu,” amesema.

Baashi ya waumini wa dini ya kiislamu walio nufaika na mgao wa futari iliyo tolewa na mbunge wa Uyoke Dk Tulia Ackson. Picha na Hawa Mathias

Amesema hana shaka kuwa Dk Tulia kwa hayo anayoyafanya atapata thawabu kubwa mbele za Mwenyezi Mungu na pia ametuma salamu kuwa wale watakaomuiga watapata thawabu pia.

“Hilo lipo wazi, Dk Tulia ndiye kinara wa kufuturisha Waislamu kila mwaka katika Mkoa wa Mbeya. Ndiye mwanzilishi, lakini leo kuna misururu ya mialiko ya futari,” amesema.

Sheikh Njalambaha amesema kitendo hicho cha kukutanisha makundi mbalimbali, wakiwemo Waislamu, kinajenga mshikamano na amani kwa wananchi wa Mbeya mbali na kuwa yeye ni kiongozi wa juu.

“Dk Tulia ni championi wa mambo hayo. Amekuwa mwanamke kinara, jasiri na anayejishusha kwa watu wa chini kabisa pasipo kujali nafasi yake, na ninawasihi wananchi wa Uyole kuitunza tunu hiyo,” amesema.

Naye Sheikh Ibrahim Bombo, Mjumbe wa Baraza la Masheikh Mkoa wa Mbeya, amesema wamepokea sadaka ambayo itagusa wahitaji 204 kutoka misikiti 17 katika kata 13 za jimbo hilo.

“Sasa ninyi Waislamu wa Uyole mwezi huu mtukufu wa Ramadhani mtakuwa wanufaika wakubwa, lakini pia kumshukuru huu ni mwanzo mzuri. Mtumieni vizuri Dk Tulia ili muweze kunufaika zaidi,” amesema.

Mmoja wa wanufaika, Salma Issa amesema kimsingi walijua ni wapweke kwa kukosa misaada mbalimbali, na kwamba wanamuombea kwa Mungu Dk Tulia katika kutekeleza majukumu yake kwa Watanzania.