Dar es Salaam. Serikali imeahidi kuwa katika bajeti ya mwaka huu itazifanyia kazi changamoto za kikodi zinazolalamikiwa na wafanyabiashara na wenye viwanda kama mkakati wa kuendelea kuvutia uwekezaji wa ndani na kutoka nje ya nchi.
Ahadi hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam jana Machi 17, 2026 na Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, wakati wa kikao na wanachama wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), kilichoangalia changamoto za kikodi na mafanikio ya wenye viwanda.
Amesema nia ya Serikali ni kuona wafanyabiashara na wenye viwanda wanafanya kazi kwenye mazingira mazuri zaidi yatakayowafanya wazidi kuongeza uzalishaji.
“Serikali inatambua umuhimu wenu katika ukuaji wa uchumi, kwa hiyo kwenye bajeti ijayo itazingatia sana maombi na ushauri wenu kuhusu masuala mbalimbali ya kikodi. Sote tunajenga nyumba moja.
“Kama mlivyofanya mwaka jana, mwaka huu pia mmetuletea mapendekezo mengine, na yale ya mwaka jana kwa asilimia zaidi ya 60 Serikali iliyafanyia kazi. Hii inaonyesha ni jinsi gani ninyi mlivyo washauri wazuri sana wa Serikali,” amesema.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ana nia ya kukuza uwekezaji kutoka nje na ndani ya nchi kwa kuhakikisha kunakuwa na viwanda vingi zaidi, na ndiyo sababu Serikali inajitahidi kuondoa changamoto zote za kikodi.
“Tumesikia changamoto zenu, nyingi zinahusu kodi za bidhaa na kodi ya Ongezeko la thamani (VAT). Sasa tunakwenda kuwasilisha bajeti ya Serikali ambapo mambo mengi mliyoshauri tutayagusia. Kuna kodi zitaondolewa, kodi nyingine zitapunguzwa. Tutatengeneza bajeti bora kwa ustawi wa viwanda, na ninaamini mtatabasamu,” amesema na kuongeza;
“Tutahakikisha tunafanya kitu kizuri mpaka mtabasamu, kwa sababu Serikali inawapenda. Rais Samia anawapenda wawekezaji na wenye viwanda, ndiyo maana kila siku anatatua changamoto zenu.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa (CTI), Leodegar Tenga, amesema mkutano huo ulikuwa muhimu kwa ajili ya kuzungumza masuala yatakayowasaidia wenye viwanda kuongeza uzalishaji wa bidhaa, hususan masuala ya kikodi.
Amewapongeza manaibu mawaziri walioshiriki mkutano huo wa wenye viwanda, na kuongeza kuwa Serikali siku zote imekuwa sikivu kwa wenye viwanda na imekuwa ikizifanyia kazi changamoto zao na kuweka mazingira bora.
“Tumejadiliana masuala ya kikodi na yale ambayo si ya kikodi. Tumejadili mambo mengi ambayo tunaona dhahiri yatasaidia kupunguza gharama za uzalishaji kwa wenye viwanda na kuviwezesha kufanya vizuri zaidi,” amesema Tenga.
Amesema moja ya changamoto ya kikodi inayolalamikiwa na wafanyabiashara ni kodi ya asilimia tisa iliyoanzishwa karibuni bandarini kwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi, ambayo wanasema ni kubwa sana kulinganisha na uhalisia wa biashara.
“Bandarini wamesema ukileta mzigo wowote ambao ni hatari unapewa siku moja tu ya kuuondoa. Ukikaa siku ya pili na kuendelea wanaanza kukutoza pesa. Sasa haiwezekani mzigo ukaja leo ukaondolewa leo leo, ni ngumu sana kwa wafanyabiashara,” amesema.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Deniss Londo, amesema amefurahi kusikia wafanyabiashara na wenye viwanda wakisifu uwekezaji uliofanywa na Serikali kwenye miundombinu, hali inayowasaidia katika usafirishaji wa bidhaa wanazozalisha.
Amesema Serikali inawatambua wenye viwanda na wafanyabiashara kama wadau wa kimkakati katika kufanikisha Dira ya Taifa ya 2050, na itaendelea kuwasikiliza ili kuwawekea mazingira bora zaidi ya uzalishaji.