Wanawake watakiwa kurasimisha biashara zao

Dar es Salaam. Katika jitihada za kuinua uchumi wa mwanamke na kufungua milango ya masoko mapya, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Ashura Katunzi, amewataka wanawake wajasiriamali nchini kuzingatia viwango na kurasimisha biashara zao ili kujenga uaminifu na kuongeza ushindani sokoni.

Amesema biashara nyingi ndogondogo zinakwamishwa na ukosefu wa kuzingatia viwango na kutofanya kazi kwa mfumo rasmi, hali inayozifanya zikose fursa za kupenya kwenye masoko makubwa ya ndani na nje ya nchi.

Katunzi ameyasema hayo jana Jumatano, Machi 18, 2026 jijini Dar es Salaam alipomwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga wakati wa kongamano la wanawake viongozi katika biashara 2026 lililoandaliwa na Asasi ya Accelerate Women Tanzania.

“Ni muhimu wanawake wajasiriamali wakatambua kuwa kufuata viwango si gharama bali ni uwekezaji unaolipa. Bidhaa yenye ubora unaotambulika hujenga imani kwa mteja na hupanua wigo wa biashara,” amesema.

Mkurugenzi huyo amebainisha urasimishaji wa biashara unasaidia wajasiriamali kupata fursa mbalimbali ikiwamo mikopo, masoko mapana na ushiriki katika zabuni, jambo linalochochea ukuaji wa uchumi binafsi na taifa kwa ujumla.

Akizungumzia upande wa Serikali amesema itaendelea kuboresha mazingira ya biashara kupitia sera rafiki na taasisi zake, kwa lengo la kuhakikisha wanawake wanapata nafasi stahiki ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

Mkurugenzi wa Asasi ya Accelerate Women, Bernice Fernandes amesema kongamano hilo limelenga kuangazia masuala ya uongozi, ubunifu, ujumuishi wa kifedha, teknolojia na ujenzi wa chapa, huku ukiwa chachu ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

Bernice amesisitiza kuna umuhimu kwa wanawake kujifunza jinsi ya kutumia akili unde na aina nyingine za teknolojia ya kidijitali katika biashara zao.

“Kupitia jukwaa hili wanawake wanapata fursa za ndani na nje ya nchi kujifunza kuhusu biashara, ndiyo maana nasisitiza umuhimu wa kutumia mifumo yote ya kidijitali kujifunza na kuchangamkia fursa za kukuza biashara.

Mtaalamu wa masuala ya teknolojia Michael Genuh ambaye alikuwa mtoa mada kwenye kongamano amesema teknolojia ya akili unde inaweza kuongeza tija katika biashara, kuboresha masoko na kusaidia kufanya maamuzi sahihi kwa kutumia takwimu.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Benki ya Absa aliyeshiriki kwenye kongamano hilo, Emanuel Mwanyiku amewataka wanawake kujifunza na kuendana na mabadiliko ya kidijitali, akibainisha kuwa ujuzi wa teknolojia ni muhimu katika ushindani wa uchumi wa sasa.