Dar es Salaam. Wakati kesho Ijumaa, Machi 20, 2026 dunia ikiungana kuadhimisha Siku ya Afya ya Kinywa, imeelezwa kuwa, baadhi ya watu bado hawalichukulii kwa uzito unaostahili suala la kutunza meno, fizi na ulimi.
Siku hii ilianzishwa mwaka 2013 ikiwa na malengo mbalimbali ikiwamo kuongeza uelewa, kuwa watu wengi duniani walikuwa hawatilii mkazo afya ya kinywa, hivyo kulikuwa na haja ya kuelimisha jamii.
Lengo lingine ni kuzuia magonjwa ya kinywa, kama kuoza kwa meno na ugonjwa wa fizi yanayoathiri mamilioni ya watu, lakini yanaweza kuzuilika kwa urahisi.
Wataalamu wa afya wanaonya kupuuza usafi wa kinywa kunaweza kusababisha madhara makubwa, si tu kwa meno bali pia kwa afya ya mwili mzima.
Magonjwa ya kinywa kama kuoza kwa meno (tundu), ufizi kuvimba na harufu mbaya ya mdomo huanza taratibu bila dalili kubwa.
Kama dalili hizo zikipuuzwa, zinaweza kusababisha maumivu makali, kupoteza meno na hata maambukizi yanayosambaa mwilini.
Kwa mfano, wagonjwa wa meno wengi wao hufika hospitali wakiwa tayari wamechelewa, hali inayolazimu kung’oa badala ya kuyatibu.
Tafiti mbalimbali zinaonesha afya duni ya kinywa inaweza kuhusishwa na magonjwa mengine sugu kama kisukari na matatizo ya moyo. Maambukizi ya bakteria kutoka kinywani yanaweza kuingia kwenye mfumo wa damu na kuathiri viungo vingine muhimu.
Maadhimisho ya mwaka huu kidunia yanakwenda na kauli mbiu ya: “Kinywa chenye afya, maisha yenye furaha.”
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Alhamisi Machi 19, 2026, Daktari wa Meno, Lilian Pesha kutoka Biharamulo amesema utunzaji wa afya ya kinywa unaanzia kwenye upigaji wa mswaki ambao njia sahihi ni kupiga asubuhi na usiku wakati wa kulala.
Dk Pesha amesema unaweza kupiga mswaki kwa kutumia ule wa dukani au wa asili (wa miti) na dawa ya meno yenye madini ya Fluoride.
“Tunapaswa kupiga mswaki asubuhi tukiamka na usiku tukiwa tunataka kulala kwasababu tukipiga wakati huo tunaondoa mabaki ya vyakula na uchafu mwingine. Ukipiga mswaki asubuhi unaondoa uchafu ambao umelala nao na ukipiga usiku unaondoa uchafu wa siku nzima.
“Tena unapopiga mswaki hupaswi kutumia nguvu sana ukaharibu fizi au kuondoa leya yake maana yake meno utayachubua,” ameshauri.
Dk Pesha amesema usipopiga mswaki inavyostahili unawapa bakteria waliopo mdomoni nafasi ya kushambulia ule uchafu unaokuwa umeganda mdomoni.
“Tusipopiga mswaki asubuhi na usiku tunajiweka katika hatari ya kutoboka kwa meno, harufu mbaya kinywani kutokana na bakteria kushambulia mabaki ya vyakula yanayokuwa mdomoni,” amesema.
Daktari huyo ameshauri watu kuzingatia upigaji mswaki hasa nyakati za usiku kwakuwa, itaondoa uchafu unaokuwa mdomoni hivyo bakteria hawatakuwa na nafasi ya kushambulia.
Amesema utunzaji mbaya wa afya ya kinywa unaweza kusababisha kutoboka kwa meno, harufu mbaya kinywani, wakati mwingine vidonda.
Dk Pesha ameshauri kufanya uchunguzi wa afya ya kinywa angalau mara mbili kwa mwaka ili kujiepusha na madhara yanaoweza kujitokeza.
Akielezea kiundani zaidi daktari wa kinywa na meno kutoka jijini Mbeya, Flaviana Nyatu amesema ili upate shida ya meno kutoboka lazima kuwe na sukari na bakteria.
Amesema kukiwa na sukari mdomoni, bakteria watajitengenezea chakula, hivyo watasababisha jino kutoboka ijapokuwa ni mchakato mrefu ukienda hadi miezi 18.
“Sasa hapa tunapunguza bakteria kwa kupiga mswaki, hivyo ukipiga asubuhi na usiku unawapunguza hatari yao ya kuharibu meno. Usipopiga kwa usahihi mfano ukipiga asubuhi tu na unatumia vyakula vya sukari nyingi kama keki au soda, unawapa nafasi ya kuwepo kwa wingi kushambulia meno,” amesema.
Pia, amesema ukilala usiku, mtiririko wa mate unapungua kinywani hivyo kunakuwa na nafasi nzuri ya bakteria kutoboa meno kwakuwa hakuna shughuli yeyote inayowasumbua ukilinganisha na mchana.
“Ila unaweza ukakuta mtu hapigi mswaki usiku na hatoboki meno Mfano watu wa vijijini lakini kilichopo hapa ni mtu huyu anakuwa hatumii sukari mara kwa mara, hivyo inakuwa ngumu kwa bakteria kushambulia,” amesema.
“Ukienda vijijini wanakula vyakula vya asili, huwezi kukuta mtu anaumwa kutoboka kwenye meno kwakuwa hawatumii sana sukari ukilinganisha na mijini watu wanakula sana sukari ya viwandani,”amesema.
Dk Nyatu amesema usipotumia sukari unawaondolea bakteria chakula, hivyo hawawezi kutoboa jino pia kama unakula sukari mfano keki halafu ukaenda kupiga mswaki hapo hapo ni sawa, kwa kuwa huwapi nafasi bakteria.
Amesema mtu yeyote mwenye meno yuko hatarini kupata magonjwa ya fizi au kutoboka kwa meno endapo wasipotunza afya ya kinywa.
“Jinsi ya kuzuia unapaswa kupiga mswaki na usiku kabla ya kulala na tunaelekeza matumizi ya mswaki laini ili kuzuia kuumiza fizi na meno,” amesema Dk Nyatu.
Mambo ya kufanya kulinda kinywa
Kwa mujibu wa utafiti wa Vipeholm Study ili kulinda afya ya kinywa unapaswa kuepuka vyakula na vinywaji vyenye sukari nyingi kama soda, pipi, keki na juisi kwa sababu skari hulisha bakteria wanaosababisha kuoza kwa meno.
Kwa mujibu wa utafiti mwingine wa Revista FT wa mwaka 2025, matumizi ya tumbaku kama kuvuta sigara au kutumia bidhaa za tumbaku husababisha fizi kudhoofika na harufu mbaya ya mdomo.
Utafiti unaeleza kuwa, kulinda afya ya kinywa unapaswa kupiga mswaki angalau mara mbili kwa siku pamoja na kufanya uchunguzi wa meno angalau mara moja kwa mwaka.
Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Kinywa yanatoa fursa ya kujitathmini na kubadili mtazamo kuhusu kinywa. Mwisho
