Tangu miaka ya 1990 hadi 2026, Mahakama za Tanzania na ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) zimekuwa zikituonyesha wapi kunavuja katika Katiba na sheria zetu, lakini kukosekana kwa utashi wa kisiasa kumefanya tufumbe macho tusione.
Ukweli una sifa moja tu, kwamba hata ukiukataa haugeuki kuwa uongo, nami nasema kwa uzoefu nilionao wa siasa za Tanzania, nathubutu kusema bila kuwapo utashi wa kisiasa, hata Katiba mpya inayoliliwa tangu miaka ya 90 itabaki kuwa ndoto.
Nasema hivyo kwa sababu hata hukumu hizi zilizotolewa na AfCHPR Machi 6, 2026, hata kama ni nzuri kiasi gani na ni kilio cha muda mrefu cha wadau wa demokrasia na haki, hazitaguswa kama hakutakuwa na utashi wa kisiasa.
AfCHPR imeipa Tanzania miezi 24 kuzifanyia marekebisho Ibara ya 74(12) ya Katiba ya Tanzania na Ibara ya 119(13) ya Katiba ya Zanzibar zinazozuia mahakama kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume za Uchaguzi hapa Tanzania.
Lakini siku hiyo pia AfCHPR iliipa Serikali miezi 24 kuifanyia marekebisho Ibara ya 41(7) ya Katiba ya Tanzania, inayozuia mahakama kuchunguza ushindi wa kiti cha Rais baada ya Tume ya Uchaguzi kumtangaza mshindi wa kiti hicho.
Kumbuka Katiba yetu hii hii katika Ibara ya 107A (1) inasema mamlaka ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa mikononi mwa mhimili wa Mahakama. Sasa tunapotoa kinga hizo tunapeleka ujumbe gani kwa umma?
Kwa akili ya Watanzania wa kawaida kabisa na hisia zilizojengeka tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa mwaka 1992, ni kwamba kuna jambo huwa linafichwa kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi.
Yaani tunakipa kinga ya kutoshitakiwa chombo kinachopaswa kuendesha uchaguzi huru, haki na unaoaminika, kwamba hata baadhi ya watendaji wake wakiboronga namna gani au wakipika data namna gani, wasihojiwe kortini.
Kwamba Tume ya Uchaguzi ikishamtangaza mgombea wa kiti cha urais kuwa ndiye mshindi, basi hakuna mahakama yoyote inayoweza kuchunguza kuchaguliwa kwake hata kama uchaguzi huo unalalamikiwa kuwa haukuwa huru na wa haki.
Ukisoma Ibara ya 13 ya Katiba inasema watu wote ni sawa mbele ya sheria na kwamba ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote hapa nchini kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa athari.
Nchi hii inaongozwa kwa utawala wa sheria na Ibara ya 3 ya Katiba imeeleza wazi kuwa nchi yetu ni ya kidemokrasia na yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa. Sasa unazuiaje Tume au matokeo ya urais yasipingwe kama kuna mtu haridhiki?
Ni kutokana na ukakasi wa Ibara hiyo ya 41(7) ya Katiba ndipo Januari 31, 1995, uliwasukuma Jaji Mkuu wa wakati huo Francis Nyalali pamoja na majaji wenzake Robert Kisanga na Jaji Lameck Mfalila kushauri sheria irekebishwe ili matokeo ya Rais yaweze kuhojiwa kortini.
Wakati huo majaji hao walijadili kifungu cha 108 cha Sheria ya Uchaguzi ambacho kiliruhusu tu matokeo ya ubunge kuhojiwa. Wakasema kuacha matokeo ya Rais bila kuhojiwa katika mfumo wa vyama vingi vya siasa ni kukaribisha machafuko.
Badala ya kusikiliza ushauri huo, sisi tukaenda tukakifunga kabisa kwa kurekebisha Katiba na kuingiza kifungu cha 41(7) kinachozuia kabisa matokeo ya urais kuhojiwa kortini licha ya mahakama kuwa chombo cha mwisho cha utoaji haki.
Sasa leo AfCHPR inatoa hukumu na kutuambia kuwa ibara hizo mbili zinakiuka Itifaki ya Mkataba wa Kimataifa juu ya Haki za Binadamu Afrika ulioanzisha Mahakama hiyo ambayo sisi tumeridhia, lakini bado wala hatutachutama chini.
Mahakama hiyo imekwishatoa maamuzi mengine mazuri tu kwa mustakabali wa demokrasia ya nchi yetu, ikiwamo kuruhusu uwepo wa mgombea binafsi au mgombea huru. Hadi leo kimya, ndiyo maana nasema utashi wa kisiasa unahitajika.
Lakini niwakumbushe tu, Mei 16, 1991, jopo la majaji watatu hapa nchini wakiongozwa na Jaji Mkuu Francis Nyalali na majaji Lewis Makame na Augustino Ramadhan aliyekuja kuwa Jaji Mkuu, walitoa hukumu ya kihistoria hapa nchini.
Majaji hao walikuwa wakitoa hukumu ya rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) dhidi ya Daud Pete aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya wizi wa kutumia silaha, ambapo aliwasilisha ombi la dhamana mahakamani na akapewa.
Mahakama ya chini ilimpa dhamana kwa maelezo kuwa kuzuia dhamana yake kunakiuka Katiba. DPP hakuridhika akakata rufaa Mahakama Kuu ambayo ilibariki maamuzi yale, ndipo DPP akakimbilia Mahakama ya Rufani kukata rufaa.
Katika hukumu yao walisema: “Kwa ufupi, kwa sababu hiyo, ingawa kwa sababu tofauti, tunakubaliana na Jaji Mwalusanya kwamba kifungu cha 148(5)(e) ni kinyume cha Katiba na hivyo kinaondolewa katika vitabu vya sheria vya nchi.”
Wakaendelea kusema kuwa hii ina maana kwamba mahakama zina mamlaka ya kutoa dhamana kwa watu wanaotuhumiwa kwa makosa yaliyoainishwa chini ya kifungu cha 148(5)(e) kwa mujibu wa sheria kama ilivyokuwa kabla ya kutungwa.
“Mamlaka haya yanapaswa kila wakati kutumiwa na mahakama kwa kuzingatia haki, yakizingatia maslahi ya mtu binafsi na jamii ambayo mtu ni sehemu yake,” walisisitiza. Lakini bahati mbaya sana msimamo huo haukusimama kama ulivyo.
Tumeendelea kushuhudia washukiwa wa mauaji, wizi wa kutumia silaha, uhaini, utakatishaji fedha na usafirishaji wa dawa za kulevya wakinyimwa dhamana kwa kuegemea kifungu hicho ambacho awali kilitakiwa kuwa kinakiuka Katiba ya nchi.
Ndiyo maana nimesema bila utashi wa kisiasa tutaendelea kutwanga maji kwenye kinu, kwani Juni 13, 2023 jopo la majaji 10 wa AfCHPR walitoa hukumu ya kihistoria wakiungana na Jaji Mkuu Nyalali na wenzake juu ya kifungu hicho.
Majaji hao walikuwa wametoa hukumu ya maombi namba 039/2020 yaliyofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) waliokuwa wakipinga kifungu hicho.
Katika hukumu yao majaji hao walisema kifungu hicho cha 148(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kinakiuka vifungu mbalimbali vya Itifaki iliyoanzisha Mahakama hiyo na kutoa miezi 24 kwa Serikali kukirekebisha.
Yapo maamuzi mengine katika Mahakama hiyo na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki yaliyotamka baadhi ya vifungu vya sheria au Katiba kukiuka Itifaki za mikataba iliyoanzisha taasisi hizo, ikiwamo ile ya wakurugenzi kuwa wasimamizi wa uchaguzi.
Machi 25, 2022, Mahakama ya Afrika Mashariki ilimpa ushindi Freeman Mbowe na wenzake watatu, Seif Sharif Hamad (marehemu), Zitto Kabwe, Hashim Rungwe, Salum Mwalimu na LHRC juu ya mamlaka ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Mamlaka hayo yapo katika Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019 inayompa mamlaka makubwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia shughuli za kisiasa za vyama, ambapo mahakama ilibaini baadhi ya vifungu vinakiuka Mkataba wa EAC.
Juni 14, 2013 AfCHPR ilitoa hukumu ya kihistoria katika shauri lililokuwa limefunguliwa na Tanganyika Law Society (TLS), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) na Mchungaji Christopher Mtikila (marehemu).
Mifano ya maamuzi ya majaji juu ya sheria za Tanzania ni mingi, lakini tumeyafanyia kazi kiasi gani kuyarekebisha? Jibu ni hakuna, ukiacha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ambayo bado ina mapungufu.
Ndiyo maana nimetangulia kusema tunahitaji utashi wa kisiasa ili kutekeleza hukumu na maamuzi ya mahakama ambayo watawala wanaona yanagusa maslahi yao ya kisiasa. Tofauti na hivyo tutaendelea kutwanga maji kwenye kinu.
Nimalizie kwa kusema hukumu hizo zinatupa somo moja tu, kwamba tunahitaji kuandika Katiba mpya ambayo ni sheria mama, itakayokwenda kurekebisha sheria nyingi hapa Tanzania ambazo zinalalamikiwa kuminya haki.
Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Anapatikana kwenye namba 0656600900
