Dar es Salaam. “Mwaka 1980 nilijifungua mtoto ambaye baadaye niligundua hasikuu. Nilipohitaji kumpeleka shule, nilikumbana na changamoto kubwa kwa kuwa mkoani Morogoro hakukuwa na shule iliyoweza kumpokea kutokana na hali yake ua uziwi. Shule pekee niliyoipata ilikuwa ya Buguruni Viziwi, iliyopo Dar es Salaam,” anaanza kusimulia Hellen Nkalang’ango.
Ameyasema hayo baada ya kufanya mahojiano na Mwananchi na kueleza kuwa kutokana na hali hiyo, alilazimika kumpeleka mtoto huyo jijini Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka sita na kumweka bweni, hatua aliyosema ilikuwa ngumu kihisia lakini muhimu kwa mustakabali wa elimu ya mtoto wake.
Simulizi hiyo ndiyo chimbuko la dhamira ya Hellen, ambaye sasa ni mwanzilishi na mkurugenzi wa Shirika la Sawa Wanawake mkoani Morogoro, ili kutafuta suluhisho kwa watoto wengine wenye changamoto kama hiyo.
Akiwa anaendelea kufuatilia masomo ya mwanawe, Hellen anasema alianza kujiuliza kwa kina namna watoto wenye ulemavu wa kusikia na mahitaji maalumu kwa ujumla wanavyoweza kupata elimu kwa usawa bila kubaguliwa.
Anasema wakati huo, watoto hao walilazimika kusoma kwa muda mrefu zaidi hadi miaka 10 katika elimu ya msingi, tofauti na mfumo wa kawaida wa miaka saba, jambo lililompa msukumo wa kutafuta njia ya kubadilisha hali hiyo.
“Nilitamani kuona watoto hawa wanasoma kwa muda sawa na wenzao na wanapata fursa zilezile za kufaulu na kuendelea na masomo,” anasema.
Katika kutekeleza azma hiyo, Hellen alianza kuwashawishi watu mbalimbali, hususan wanawake wajane, kuungana naye ili kuanzisha chombo cha pamoja kitakachosaidia kukabiliana na changamoto hizo.
Mwaka 1996, alianzisha kikundi cha awali kilichokuwa na wanawake watano, ambacho baadaye kilikua na kufikia waanzilishi 12, kisha kusajiliwa rasmi mwaka 1998 kama Shirika la Sawa Wanawake. Lengo kuu lilikuwa kusaidia wajane pamoja na watoto wenye mahitaji maalumu.
Baada ya kupata usajili, shirika lilianza kutafuta suluhisho la changamoto za elimu kwa watoto wanaotoka katika familia maskini na wale wenye mahitaji maalumu, wakiwamo wenye uziwi, wenye changamoto za afya ya akili na ulemavu wa viungo.
Waanzilishi waliamini kuwa haki ya elimu ni ya kila mtoto bila kujali hali yake na kwamba, kwa kuweka mazingira sahihi, kila mtoto ana uwezo wa kujifunza na kufikia ndoto zake.
Hatua ya kwanza ya utekelezaji ilikuwa kuanzisha shule ya msingi itakayotoa elimu jumuishi kuanzia awali hadi darasa la saba, kwa lengo la kuwahudumia watoto wa makundi mbalimbali bila ubaguzi.
Kupitia ufadhili wa wadau mbalimbali, wakiwamo Social Teachers kutoka Korea pamoja na msaada wa kiwanja kutoka serikalini, waliweza kujenga shule hiyo ambayo sasa inapokea watoto wote, wenye mahitaji maalumu na wasio na changamoto hizo.
Hellen anasema mfumo wa elimu jumuishi wanaoutumia, unalenga kuhakikisha watoto wanasoma pamoja badala ya kutengwa, hali inayochangia kuongeza ushirikiano, uelewa na kujiamini kwa wanafunzi.
Kwa sasa, shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 279, kati yao 26 wakiwa na mahitaji maalumu. Kati ya hao, wanafunzi 21 hawalipi ada ili kuwawezesha kupata elimu bila vikwazo vya kifedha.
Kwa wanafunzi wengine, wazazi huchangia ada ya Sh800, 000 kwa mwaka kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, gharama inayojumuisha pia chakula cha mchana. Hata hivyo, wazazi hubeba gharama za vitabu na usafiri.
“Tunahudumia idadi ndogo ya wanafunzi kwa sababu hii ni shule ya mfano na rasilimali zetu ni chache,” anasema Hellen.
Pamoja na mafanikio hayo, shirika bado linakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo uhaba wa wataalamu wa lugha ya alama kwa ajili ya kufundisha wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia.
Kutokana na hali hiyo, wakati mwingine hulazimika kutumia wanafunzi waliomaliza masomo yao kuwasaidia wenzao katika kujifunza lugha ya alama.
Aidha, somo la lugha ya alama linafundishwa kwa wanafunzi wote kuanzia darasa la kwanza, lakini upungufu wa vitabu vya kufundishia bado ni changamoto inayokwamisha jitihada hizo.
Mbali na kuanzisha shule, Sawa pia limejikita katika kuboresha miundombinu ya elimu katika maeneo mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
Shirika hilo limefanya kazi katika wilaya za Morogoro Mjini, Mvomero, maeneo ya Mvuha pamoja na Mufindi mkoani Iringa, ambako limechangia ujenzi wa madarasa na miundombinu mingine ya kujifunzia.
Hellen anasema changamoto nyingine kubwa iliyosukuma juhudi zao ni umbali mrefu wanaotembea wanafunzi, hususan wasichana, kufuata shule.
“Baadhi yao walikuwa wanatembea zaidi ya kilomita saba hadi nane kila siku kwenda na kurudi shuleni, hali iliyowaweka katika hatari na kuathiri mahudhurio yao,” anasema.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Sawa kwa kushirikiana na jamii na halmashauri, lilianzisha ujenzi wa hosteli kwa ajili ya wanafunzi wa kike.
Hadi sasa, hosteli tano zimejengwa, nne zikiwa wilayani Mvomero na moja Mufindi, hatua inayochangia kuboresha upatikanaji wa elimu kwa wasichana na kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kila siku.
Alivyogusa ustawi wa jamii
Mbali na kuwekeza katika miundombinu ya elimu, Hellen anasema taasisi ya Sawa Mwanamke pia imejikita katika kuboresha ustawi wa jamii kwa kuwajengea uwezo wazazi, hususan wanawake.
Anasema kupitia mafunzo ya malezi na makuzi ya watoto pamoja na ujasiriamali, zaidi ya wanawake 550 wamewezeshwa kiuchumi na kujipatia kipato cha kujitegemea.
Wanawake hao wameunganishwa katika vikundi 19 vya kuweka na kukopa (Vicoba) na tangu mwaka 2019, kila kikundi kimekuwa kikipatiwa mtaji wa Sh5 milioni, ili kuwawezesha kuanzisha na kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Katika hatua nyingine, shirika hilo limepanua wigo wa shughuli zake kwa kuwekeza katika ukuzaji wa stadi za maisha kwa watoto, likilenga kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku.
Kupitia uanachama wake katika mtandao wa Regional Education and Learning Initiative (Reli), unaojihusisha na masuala ya elimu, Sawa lilishiriki katika tathmini ya awali iliyochunguza namna stadi za maisha zinavyofundishwa kwa wanafunzi waliopo shuleni na wale walio nje ya mfumo wa elimu.
Ofisa ubora wa elimu wa shirika hilo, Mahamoud Ngamange anasema matokeo ya tathmini hiyo yalitoa mwongozo muhimu uliosaidia kuchochea hatua za vitendo katika kuimarisha ufundishaji wa stadi za maisha.
“Katika utekelezaji wa mpango huu, tumekuwa tukitoa mafunzo kwa walimu na wazazi kuhusu umuhimu wa stadi za maisha katika maendeleo ya mtoto,” anasema.
Anafafanua kuwa mafunzo hayo yanajumuisha masuala muhimu kama ushirikiano, utatuzi wa matatizo, kujitambua, mawasiliano na heshima, ujuzi ambao ni msingi wa mafanikio ya mwanafunzi darasani na nje ya darasa.
Kwa mujibu wa Ngamange, mwanafunzi mwenye stadi hizo ana nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa si tu kitaaluma, bali pia katika maisha yake ya baadaye.
Ili kuhakikisha elimu hiyo inawafikia watu wengi zaidi, Sawa lilianzisha mfumo wa “vinara wa stadi za maisha”, unaowahusisha wazazi na wanajamii waliopata mafunzo maalumu na kisha kuwafundisha wengine katika jamii zao.
Vinara hao hutumia majukwaa mbalimbali ya kijamii, ikiwemo mikutano ya kijamii, vikundi vya akiba, maeneo ya kazi na hata sehemu za burudani, kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa stadi za maisha kwa watoto.
Kwa sasa, shirika linafanya kazi na shule 14 katika maeneo tofauti, nne kati ya hizo zikitekeleza kwa karibu programu ya stadi za maisha.
Hata hivyo, Ngamange anabainisha kuwa bado hawajafikia shule zote kutokana na ukomo wa rasilimali, lakini wana mpango wa kupanua wigo wa huduma hizo katika siku zijazo.
Katika mpango mkakati wa mwaka 2026 hadi 2030, Sawa limeweka ukuzaji wa stadi za maisha kuwa moja ya maeneo yake mapya ya kipaumbele, likilenga kuhakikisha wanafunzi wengi zaidi wanapata ujuzi huo muhimu kwa maendeleo yao ya sasa na ya baadaye.
