Vikwazo kwa zao la tende vyawekwa hadharani, wanaume wakitajwa kuongeza thamani

Dodoma. Changamoto ya upatikanaji wa miche bora ya tende pamoja na masharti yanayowekwa na nchi zinazolima zao hilo zimetajwa kuwa miongoni mwa vikwazo vinavyokwamisha ukuaji wa kilimo cha tende nchini.

Kutokana na vikwazo hivyo, wakulima wengi wameendelea kutumia mbegu za zamani, ambazo zinaelezwa kuwa hazina tija katika kipindi hiki.

Hali hii inajitokeza wakati mahitaji ya tende yakiongezeka kufuatia imani ya baadhi ya watu kuwa husaidia kuongeza nguvu na hamu ya tendo la ndoa, hivyo kuifanya zao hilo kuwa na soko kubwa la ndani.

Hayo yameelezwa na mtaalamu wa kilimo cha tende kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Nicholas Kuboja, leo Alhamisi, Machi 19, 2026, wakati wa mafunzo ya siku tatu kwa wakulima 57 waliochaguliwa kushiriki katika mashamba ya mfano.

Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wakulima wa tende na yanatekelezwa kwa ufadhili wa Serikali ya Saudi Arabia kupitia King Salman Humanitarian Aid and Relief Centre.

Tayari zaidi ya miche 3,700 imepandwa mashambani, huku wakulima wengine wakiendelea kusubiri kupatiwa miche hiyo.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Dk Nicholas Kuboja amesema baadhi ya mikoa ya kati imechaguliwa kwa ajili ya mradi huo kutokana na mwamko mkubwa wa wakulima.

Hata hivyo, amebainisha kuwa juhudi hizo zinakwamishwa na taratibu za nchi zinazozalisha miche ya mbegu, ambazo zina masharti mengi kuhusu ununuzi na usafirishaji wake.

“Sisi tumekuja na utaalamu kuhusu zao hili jipya nchini, lakini ikumbukwe mitende ilikuwepo tangu siku nyingi katika maeneo tofauti. Hawa wakulima wametupa ujuzi na mbinu ambazo hatukutegemea. Kikwazo ni namna ya kupata mbegu,” amesema Dk Kuboja.

Mtaalamu huyo amesema mwitikio wa wakulima kwa zao la tende katika mikoa ya kati umekuwa mkubwa kuliko kiwango cha mbegu zilizotengwa kwa awamu ya kwanza, jambo linalowalazimu kujipanga kwa namna nyingine.

Mkulima wa zao la tende kutoka Kijiji cha Mvumi, Wilaya ya Chamwino, Dk Aman Daniel, amesema hata kabla ya Serikali kuanza uhamasishaji wa zao hilo, yeye alishaona mafanikio ndiyo maana aliendelea kupanua mashamba.

Dk Daniel amesema mbali na mitende kutumika kama chakula, mti wake hakuna kinachotupwa, na ndiyo maana aliamua kuwekeza akijua itamjengea uwezo wa kiuchumi.

“Mvumi tunalima zabibu, hata nami nimelima, lakini najitahidi kuwekeza zaidi kwenye tende kwani mafanikio nilishayaona. Pia naitazama mitende itakuwa dhahabu kwa siku za usoni,” amesema Dk Daniel.

Akizungumzia utaalamu, amesema kuna baadhi ya taratibu wakizifuata moja kwa moja kuna maeneo watakwama kwani haiko hivyo uwandani, hivyo inapaswa uzoefu na historia pia iangaliwe kwa maeneo yanayozalisha.

Katika hatua nyingine, mkulima huyo ametaja alichosema kinaongeza thamani kwenye zao hilo na bei yake kuwa ni imani kwamba wanaume wanaotumia tende kula au kunywa juisi yake huongeza nguvu katika tendo la ndoa.

Mratibu wa mradi huo kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Fadhir Mtengela, amesema lengo la mradi huo lilikuwa kuwafikia wakulima 250, ingawa katika hatua ya kwanza ya ugawaji wa miche wakulima 57 ndiyo watanufaika.

Mtengela ameeleza kuwa changamoto kubwa wanayokutana nayo ni uagizaji wa miche kutoka mataifa ya India, Misri na Falme za Kiarabu, ambapo taratibu zake huchukua muda mrefu licha ya wakulima kuwa tayari wameshaandaa mashamba yao.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa kilimo, Tabu Likoko, amesema kuwa dunia ina jumla ya mataifa 38 yanayolima tende, huku asili ya zao hilo ikitajwa kuwa Iraq.

Ameongeza kuwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kenyandiyo nchi pekee yenye mashamba makubwa ya tende.