Bakari Mahundu
March 19, 2026
0 Comments
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ameshiriki Mkutano wa Kimataifa wa Masuala ya Uchukuzi (NCT) uliofanyika katika Ukumbi wa Gallagher Estate, Johannesburg, Afrika Kusini. Mkutano huo ulifunguliwa na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa.
Sambamba na ushiriki huo, Naibu Waziri pia amehudhuria Mjadala wa Mawaziri wa Uchukuzi ukiwa na mada isemayo: “Leadership and Governance in the Implementation of an Integrated, Sustainable and Safe Transport System that Promotes Inclusive Economic Growth, Job Retention and Social Development in Southern Africa.”
Wakati wa mjadala huo, Naibu Waziri alieleza hatua mbalimbali zilizofikiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza miundombinu, ikiwemo uwekezaji mkubwa katika Reli ya Kisasa (SGR), maboresho ya bandari, viwanja vya ndege, na miundombinu ya barabara.
Aidha, alisisitiza kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na kuwakaribisha wawekezaji kushiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo ya sekta ya uchukuzi, kwa lengo la kuimarisha biashara, kuongeza ushindani wa kiuchumi, na kukuza maendeleo ya kikanda.
