Dar es Salaam. Wakati Waislamu nchini wakijiandaa kusherehekea sikukuu ya Eid kati ya kesho Ijumaa au Jumamosi, Machi 21, 2026, mfumko wa bei kwenye vyakula na nguo za watoto umekuwa kikwazo katika shamrashamra hizo, baadhi wakilalamikia kupanda kwa bei za bidhaa hizo muhimu.
Wamesema hali hiyo imewalazimu wengi kubana matumizi na wengine kubadili mipango yao ya kusherehekea sikukuu hiyo muhimu ya kidini.
Hata hivyo, licha ya mfumko wa bei kulalamikiwa, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limewasisitiza waumini wanapojiandaa kusherehekea sikukuu hiyo wakumbuke kauli mbiu ya mwaka huu ya Eid ambayo ni amani na maadili katika ujenzi wa jamii bora.
Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Nuhu Mruma, akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Machi 19, 2026 amesema wakati waumini wakitarajia kusali sala ya Eid kati ya Machi 20 au 21 kutegemea mwandamo wa mwezi, wanapaswa kusimamia ujumbe wa Eid wa mwaka huu wa amani na maadili katika ujenzi wa jamii bora.
Amesema mwezi wa Ramadhani umekuwa kama chuo kilichowafanya waumini wawe na huruma, wapole na waliosaidiana katika heri na kujali wasiojiweza, yatima na wajane, hivyo wanapaswa kuyaishi yale yote waliyoyafanya katika mwezi huo hata baada ya kupita.
“Mwezi wa Ramadhani ndiyo unamalizika, lengo la kuwafanya kuwa wacha Mungu zaidi limetimia, lakini unapoelekea ukingoni tunasisitiza Waislamu wote kuendelea kuyaishi maisha hayo hata baada ya Ramadhani.
“Tunawaelekeza kwamba wajiandae vizuri kifamilia, wasubiri maelekezo ya viongozi. Kama mwezi utaonekana basi washiriki ibada ya Eid katika misikiti mbalimbali, na kikubwa zaidi wenye uwezo wawasaidie wasiokuwa na uwezo kwa kutoa Zakat al-Fitr,” amesema.
Wakati shamrashamra za maandalizi ya sikukuu zikiendelea, baadhi ya wananchi wamelalamikia mfumko wa bei kwenye bidhaa za vyakula na nguo za watoto.
Mwananchi iliyotembelea soko maarufu la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, ilishuhudia pilika na msongamano wa watu katika kufanya manunuzi, huku baadhi wakieleza namna nguo za watoto zilivyopanda bei kulinganisha na Eid ya mwaka jana.
“Mwaka huu nguo za watoto za Uturuki zinauzwa hadi Sh 50,000 kutoka Sh 35,000, zimekuwa juu sana,” amesema Asha Rashid.
Amina Rajabu amesema kuna unafuu katika nguo za wakubwa, akitolea mfano vazi la abaya, ambalo amesema katika kipindi kama hiki miaka ya nyuma lilifika hadi Sh70,000.
“Mwaka huu hadi Sh20,000 unapata. Changamoto ipo kwenye nguo za watoto, bei imepanda sana,” amesema.
Mmoja wa wafanyabiashara ambaye aliomba hifadhi ya jina amesema vita ya Israel na Marekani dhidi ya Iran inaweza kuwa imesababisha kupanda kwa bei, akieleza kwamba wafanyabiashara wengi hawakwenda kufuata mzigo.
“Mzigo unaouzwa mwingi ni ule ambao ulikuwa stoo. Wengi hatukusafiri, hivyo wale walio na mzigo wanatumia kama fursa na kupandisha bei,” amesema.
Mwananchi imetembelea masoko kadhaa ya Dar es Salaam ikiwamo la Mbezi, Mabibo na Buguruni ambako baadhi ya bidhaa kama nyanya, viazi mviringo na kuku zimepanda.
Vilevile, bei ya nyama katika mabucha yaliyopo kwenye machinjio ya Vingunguti nayo imepanda hadi kufika Sh 12,500 mpaka Sh 13,000 kwa kilo kutoka Sh 11,000.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa nyama Vingunguti, Joel Meshack amesema kutokana na bei hiyo ya Vingunguti, kuna uwezekano bei ikafika hadi Sh 15,000 katika mabucha mengine ya mitaani.
“Kipindi kama hiki wanunuaji wa nyama ni wengi, tofauti na kipindi cha Pasaka ambapo wengine huchinja majumbani na wengine huwa wamehifadhi nyama kwa muda kwenye majokofu,” amesema.
Amesema katika sikukuu za Eid historia inaonyesha wengi hutaka nyama ya siku hiyo hiyo, hivyo uhitaji wa wateja huwa mkubwa na gharama zinaongezeka.
Katika baadhi ya mabucha mtaani, hadi kufikia Machi 19, 2026 saa nne asubuhi, bei ya kilo moja ilikuwa Sh 14,000 kutoka Sh 12,000 ya awali.
Mwananchi ilishuhudia pia bei ya nyanya ikipanda hadi mara mbili, kutoka Sh 3,500 na Sh 4,000 kwa sado ndogo hadi Sh 6,000 mpaka Sh 8,000 katika baadhi ya masoko.
Sado ya viazi mviringo iliyokuwa ikiuzwa Sh 1,500 au Sh 2,000 imepanda na kuuzwa Sh 3,000, wakati kuku wa nyama akifikia hadi Sh 7,000 kutoka Sh 6,000 kwa mmoja katika soko la Shekilango na Buguruni.
Huduma ya kuchora hina pia imeshamiri, wajuzi wa kazi hiyo wakieleza kufanya kazi usiku na mchana tangu Machi 18, 2026 kutokana na wingi wa wateja.
Baadhi ya waumini wa Kiislamu wamesema wanachokifurahia katika kusherehekea sikukuu ya Eid ni kutoa Zakat al-Fitr na kugawa chakula kwa wahitaji.
“Mimi kuvaa kwangu sio lazima; wakivaa watoto inatosha. Lakini huwa sioni kama Eid yangu imeisha kama sijatoa Zakat al-Fitr na kugawa chakula,” amesema Mariam Shaban.
Awadh Juma amesema kwake kikubwa ni kushiriki sala ya Eid na kutoa Zakat al-Fitr.
