Radi ilivyowaua wanafunzi Dar, taratibu za mazishi…

Dar es Salaam. Hali ya huzuni imeendelea kutawala katika eneo la Msongola, wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam kufuatia vifo vya wanafunzi watatu wa Shule ya Msingi Msongola waliopoteza maisha kwa kupigwa na radi huku familia zao zikiendelea na maandalizi ya mazishi.

Taarifa zinaeleza miili ya wanafunzi wawili tayari imeanza kusafirishwa kwenda mikoani kwa ajili ya mazishi katika makazi ya familia zao, wakati mwanafunzi mmoja anatarajiwa kuagwa na kuzikwa kesho Ijumaa, Machi 20, 2026 katika eneo la Msongola.

Wanafunzi hao walifikwa na mauti jana Jumatano Machi 18, 2026, ambapo mvua zilizokuwa zikinyesha zilioambatana na radi zilisababisha vifo kwa wanafunzi hao huku wengine wawili wakijeruhiwa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alipozungumza na Mwananchi, alisema watoto hao walifikwa na mauti wakiwa eneo la shule chini ya mti.

Leo Alhamisi, Machi 19, 2026 Mwananchi limefika shuleni hapo na kuzungumza na baadhi ya wakazi na mashuhuda wa tukio hilo, limeelezwa radi hiyo ilipiga ghafla wakati wanafunzi walipokuwa katika muda wa mapumziko nje ya madarasa yao.

Kwa mujibu wa mashuhuda, kundi la wanafunzi lilikuwa limekusanyika chini ya mti mkubwa uliopo ndani ya eneo la shule hiyo wakijikinga na jua, ndipo radi ilipopiga kwa nguvu na kusababisha taharuki kubwa.

“Watoto walikuwa wamekaa pale chini ya mti wakati wa mapumziko, ghafla tukasikia mlio mkubwa na mwanga mkali sana. Baada ya hapo baadhi yao walianguka chini, ndipo tukagundua kuna waliopoteza maisha,” amesema mmoja wa mashuhuda aliyekuwepo eneo la tukio.

Shuhuda mwingine ameeleza juhudi za haraka zilifanyika kuwaokoa wanafunzi waliokuwa wamejeruhiwa kwa kuwapeleka hospitalini, huku waliopoteza maisha wakibainika kufariki papo hapo kutokana na athari za radi hiyo.

“Hali ilikuwa ya taharuki kubwa, walimu na wananchi walikimbia kuwasaidia watoto. Waliopata majeraha walipelekwa hospitali haraka,” amesema mkazi mmoja wa eneo hilo.

Kwa sasa (ilikuwa saa 8 mchana), shughuli za kawaida katika shule hiyo zimesitishwa kwa muda, huku walimu, wanafunzi na wazazi wakiwa katika majonzi wakijiandaa kushiriki taratibu za kuaga na kuzika miili ya marehemu.

Hata hivyo, jitihada za kumpata mwalimu mkuu wa shule hiyo ili kutoa maelezo zaidi kuhusu tukio hilo hazikufanikiwa, kutokana na kuwa katika majukumu ya kuratibu shughuli za msiba na maandalizi ya mazishi.

Katika tukio jingine linaloongeza uzito wa huzuni, imeelezwa kuwa mmoja wa viongozi wa kamati ya shule hiyo amefariki dunia jana kutokana na maradhi, hali inayozidisha majonzi kwa jamii ya shule hiyo.

Wakati taratibu za mazishi zikiendelea, jamii ya Msongola inaendelea kuomboleza vifo hivyo, huku wito ukitolewa kwa mamlaka kuongeza tahadhari dhidi ya majanga ya asili, hasa katika mazingira ya shule ili kulinda usalama wa wanafunzi.