Wazawa wajitosa kuendesha taksi mtandao baada ya Uber kuondoka

Dar es Salaam. Ikiwa ni takribani miezi miwili sasa tangu kampuni ya kimataifa ya taksi mtandao ya Uber kufunga shughuli zake nchini, wazawa wameibuka na jukwaa kama hilo wakisema muundo wake umezingatia matakwa na mahitaji ya Watanzania.

Jukwaa jipya la Izze limetambulishwa sokoni jana Machi 18, 2026 na linatarajiwa kuongeza ushindani katika soko la Tanzania ambao kwa muda mrefu limetawaliwa na watoa huduma wa kigeni, miongoni mwao akiwa ni Uber (mwanzilishi wa huduma hizo hapa nchini).

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutambulisha jukwaa hilo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara na Masoko, Fredrick Silaa anasema Izze imeundwa kwa kuzingatia changamoto zote ambazo wadau waliokuwa wanazilalamikia kutoka kwa watoa huduma wengine.

“Sisi tunasema ya kwetu kivyetu, tunaunganisha madereva na abiria huku tukizingatia usalama wa hali ya juu. Kila dereva wa jukwaani kwetu ataunganishwa na bima ya afya na mfuko wa hifadhi ya jamii NSSF kwa ajili ya mpango wa ulinzi wa jamii na kuunga mkono ajenda ya Serikali ya bima ya afya kwa wote,” anasema Silaa.

Kwa upande wa makato ya dereva, Silaa anasema Izze itakata asilimia 19 tu, kiwango anachosema kwa sasa ni kidogo zaidi sokoni wakati mamlaka zikitaka watoa huduma kukata kati ya asilimia 10 hadi 25.

Kadhalika, Silaa anasema jukwaa hilo linatoa fursa kwa madereva wasio na vyombo kukutana na wenye vyombo wanaohitaji madereva, pia akisema hata mtu anapohitaji dereva wa kumwendesha kwa masaa mawili atampata.

“Tunataka kurasimisha ‘day worker’ (deiwaka); mtu mwenye gari akiwa mgonjwa au amechoka aweze kutafuta dereva wa kumwendesha, na dereva atalipwa kwa muda na umbali aliotembea. Hata kama umelewa huwezi kuendesha, unaita tu dereva kupitia Izze,” anasema Silaa.

Kwa upande wao, CRDB ambao ni washirika wa kifedha wa Izze walisema ni heshima kwao kuunga mkono ujasiriamali nchini, wakisema kukua kwao kuna manufaa makubwa katika ukuaji wa benki lakini pia uchumi wa nchi kwa ujumla.

“Jukwaa kama hili lina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi, ikiwemo kutoa fursa za ajira kwa vijana,” anasema Catherine Rutenge ambaye ni Mkuu wa Huduma za Benki Kidijitali katika Benki ya CRDB Tanzania.