Dar es Salaam. Wakati sekta ya Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala (ADR) ikiendelea kukua kwa kasi duniani ikiwemo Tanzania, wadau wamewataka wanawake kujitokeza na kuchangamkia fursa hiyo kwani bado inatawaliwa zaidi na wanaume.
Kwa mujibu wa takwimu za tafiti mbalimbali barani Afrika, asilimia 72 ya wasuluhishi ni wanaume huku wanawake wakiwa ni asilimia 28 pekee. Katika taasisi kubwa za kimataifa, wanawake huchangia kati ya asilimia 29 hadi 34 ya uteuzi wa wasuluhishi.
Wito huo umetolewa leo Alhamis Machi 19, 2026, jijini Dar es Salaam katika mkutano na vyombo vya habari ulioandaliwa kuelekea kongamano wiki moja la Njia Mbadala za Utatuzi Migogoro litakaloanza Machi 27, 2026.
Kongamano hilo litakalowakutanisha watunga sera, wanasheria na viongozi wa biashara limeandaliwa na Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro Tanzania (TIAC), kwa kushirikiana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria. Kikiongozwa na Kaulimbiu “Kutoka Majadiliano hadi Hatua: Kuendeleza Ushirikishwaji wa Wanawake katika Utatuzi Migogoro kwa Njia Mbadala.”
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya TIAC, Wakili Godson Nyange amesema ukuaji wa sekta ya ADR unachangiwa na kuongezeka kwa shughuli za kibiashara na migogoro ya uwekezaji, hivyo kuwepo kwa haja kubwa ya kuongeza ushiriki wa wanawake hususan katika nafasi za juu za uamuzi.
“Lengo la kongamano hili ni kutoa elimu na kuhamasisha wanawake ili kupunguza pengo lililopo kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza ushiriki wao katika utatuzi wa migogoro,” amesema.
Amesema jukwaa hilo litatoa nafasi kwa wadau kutoka sekta binafsi na umma kujadiliana namna bora ya kuimarisha ushiriki wa wanawake, sambamba na kuunga mkono jitihada za serikali za kukuza usawa wa kijinsia na mifumo jumuishi ya utatuzi wa migogoro.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TIAC, Magreth Magoma amesema changamoto zinazowakwamisha wanawake kuingia katika sekta hiyo ni pamoja na ukosefu wa ujasiri, utayari pamoja na mila na desturi.
Amesema ili kuwa msuluhishi, mtu anatakiwa kupata mafunzo maalum na cheti cha ithibati kinachotolewa na Wizara ya Katiba na Sheria, ambayo pia husimamia orodha ya wataalamu wenye sifa hiyo.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Udhibiti Ubora kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Mercy Kyamba, amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika matumizi ya usuluhishi hasa kwenye migogoro ya kibiashara na kiraia, bado ushiriki wa wanawake hauridhishi.
“Tunatarajia kongamano hili litasaidia kuziba pengo hilo kwa kutoa jukwaa la majadiliano, ushirikiano na kubadilishana uzoefu,” amesema.
Amesema usuluhishi umeleta mafanikio makubwa hususan katika sekta ya ujenzi wa miradi na uwekezaji kati ya wawekezaji na serikali, huku maeneo ambayo bado yana changamoto yakitumika kama fursa ya kujifunza na kuboresha zaidi sekta hiyo.
Kongamano hilo litafanyika katika Ukumbi wa Wakili House jijini Dar es Salaam, likitanguliwa na mafunzo ya ana kwa ana ya siku tatu kuanzia Machi 24 hadi 26, 2026.
