Mawakala wa forodha kutumia mifumo ya malipo kidigitali, Serikali kuvuna kodi

Dar es Salaam. Mawakala wa forodha Tanzania wamesema mfumo wa malipo ya kidigitali wa Capital Pay utawawezesha kupata malipo rafiki ya huduma wanayotoa pamoja na Serikali kupata kodi yake halali.

Mawakala hao wamesema tayari wamejiandaa kutumia mifumo ya kidigitali, baada ya kuwasilisha serikalini kima cha chini cha gharama za utoaji huduma zao ili kitangazwe katika gazeti la Serikali.

Wamesema hatua zote za kukamilisha mchakato wa kupata gharama nafuu za utoaji wa huduma za uwakala wa forodha ulifuatwa na sasa Serikali ipo hatua ya mwisho kutangaza gharama hizo kwenye gazeti la Serikali.

Kauli hiyo imetolewa Machi 18, 2026 na Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha (Taffa), Edward Urio katika hafla maalumu ya kuingia makubaliano ya kutoa huduma za huduma za kidigitali na kampuni ya Capital Pay.

Capital Pay ni mfumo unaowezesha kutuma na kupokea fedha, kulipa bili, kufanya malipo ya huduma au bidhaa, kuunganisha njia tofauti za malipo.

Urio amesema tangazo la Serikali litakapotoka kuwaruhusu kuwa na kima cha chini ya gharama za utoaji huduma utawaongoza kuwa na mfumo utakaokwenda kuoana na mifumo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuonyesha manufaa ya Serikali katika sekta hiyo pamoja na wawekezaji.

“Capital Pay itatusaidia kutengeneza mifumo ambayo ni rafiki itakayotusaidia kukusanya tozo hizi na kulinda kodi za Serikali, ukiangalia sekta ya ugomboaji wa mizigo imekuwa miongoni mwa sekta tatu za juu Serikali inapata Forex (biashara ya kubadilishana fedha)” amesema.

Akizungumzia mwongozo wa gharama za utoaji wa huduma kwa mawakala wa forodha, amesema ni kiu yao ya muda mrefu kupata mwongozo wa gharama baada ya kutoa huduma.

Kukosekana kwa mwongozo huo, amesema wameharibu soko kwa kila mtu kupambania bei ya huduma yake sokoni tofauti na majukumu wanayotekeleza.

“Jukumu letu kubwa ni kusaidia Serikali kukusanya kodi na sisi ni kiungo muhimu wa Serikali katika ugombiaji wa mizigo, mawakala wa forodha ndio watu pekee wanakutana na idara zote za Serikali na sekta binafsi”amesema.

Urio amesema kiu ya kuwa na gharama inayotambulika kwenye ugomboaji wa mizigo ilianza muda mrefu kwa kuwashawishi Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) kuitishi kikao na wadau kitisha maoni ya gharama za chini juu ya utoaji wa huduma kwa watoa huduma hao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (Tacas), Efrahim Mwankuse amesema kupitia mfumo wa Capital Pay watatatua tatizo la ukusanyaji wa mapato kwa kutumia bei elekezi itakayotolewa na Tasac katika ugomboaji wa mizigo.

“Mfumo huu wa Capital Pay utatusaidia sisi tunaofikiri kufanya kazi katika masoko ya ushindani wapo mawakala wanafanya kazi kwa gharama ndogo, pili mfumo huu utatusaidia bei ya mzigo kutokuwa juu kwa kuwa gharama zote zitakuwa mtandaoni,” amesema.

Amesema unaweka ajira kwa Watanzania akiwaomba mawakala wa forodha kujivunia mfumo wa Capital Pay kwani unakwenda kuwaondoa kwenye umasikini.

Meneja Usajili wa Leseni na Forodha wa TRA, Tuntule Nkyandwale amesema mfumo wa Capital Pay utasaidia kuongeza ukadiriaji wa mapato ya ndani kwa mawakala wa forodha nchini.

“Makadirio ya Mapato kwa mawakala ni tofauti kulingana na mazingira kwahiyo mfumo huu kwetu unakwenda kuongeza ufanisi zaidi kwa kufahamu uhalisia wa mapato ya kila mmoja,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Capital Pay, Garang Malek amesema mfumo huo upo Tanzania, Zimbabwe, Rwanda na unakwenda kutibu changamoto ya upatikanaji wa mapato baina ya mawakala wa forodha na TRA.

“Kupita mfumo huu Serikali itakusanya mapato mengi na itawezesha kukusaidia utekelezaji wake ikiwemo miundombinu ya mawakala wa forodha,” amesema.