Huwezi kuamini baba mzazi anaweza kufanya haya, lakini ushahidi uliotolewa umethibitisha hilo ni kuwa Joseph Mhulula, aliamua kumuua mwanawe mwenye umri wa miaka minne, kukatakata mwili wake vipande vidogo na kuvitumbukiza chooni kwa tamaa ya kupata utajiri.
Katika mfululizo wa simulizi ya mauaji haya, tutakuletea namna baba huyo alivyotekeleza tukio hilo kisha akamwaga maji ili chooni n vile vipande vitumbukie vizuri.
Mbali na hilo, tutaangazia ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri pamoja na utetezi wa mshitakiwa na jinsi jaji alivyoukataa utetezi wa mshtakiwa na kumtia hatiani, akisema ni yeye pekee aliyemuua mtoto na si mtu mwingine.
Ni simulizi ya mauaji ya kikatili ambayo inaweza kukutoa machozi, hasa ikizingatiwa aliyeyafanya ni baba wa damu wa mtoto, ajabu naye akawa anashiriki kumtafuta mwanaye.
Tukio hilo ambalo linaweza kuwa miongoni mwa matukio ya kutisha yanayoweza kuingia rekodi za dunia, lilitokea kati ya Aprili 9 na 12, 2025 huko mtaa wa Lukosi, kata ya Mkwawa katika wilaya ya Iringa.
Kama maandiko ya Biblia yasemayo, Mathayo 26:52, auaye kwa upanga naye atauawa kwa upanga, ndivyo Machi 17,2026 Jaji Angaza Mwipopo wa Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Iringa, alimhukumu Mhulula ambaye ni ambaye ni dereva bodaboda, adhabu ya kifo.
Hii ni baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi 13 wa mashitaka na ule wa utetezi wa mshitakiwa, kisha kuuchambua na kuona upande wa mashitaka, umeweza kuthibitisha shitaka la mauaji pasipo kuacha shaka yoyote.
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tito Mwakalinga akisaidiana na Wakili David Mwakiborwa, alisema Mhulula hana rekodi za uhalifu lakini akaomba mahakama impe adhabu anayostahili kulingana na kifungu 197 cha Kanuni ya adhabu. Kifungu hicho kinasema: “Mtu ambaye amepatikana na hatia ya kosa la kuuwa kwa kukusudia atahukumiwa adhabu ya kifo”.
Kwa upande wake, Wakili Geofrey aliyemtetea mshitakiwa alisema chini ya ibara ya 14 ya Katiba ya Tanzania, kila Mtanzania anayo haki ya kuishi, hivyo mahakama isimhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa kama sheria inavyoelekeza.
Wakili huyo alitoa kauli hiyo akizingatia mazingira ya kesi hiyo, ambayo yanaonyesha baba huyo alimuua mwanae kwa kuegemea imani za kishirikina, hivyo mahakama iangalie namna ya kumpa adhabu mbadala.
Katika hukumu yake, Jaji Mwipopo alisema ingawa wakili wake ameegemea ibara hiyo ya 14 ya Katiba kuomba mteja wake apunguziwe adhabu, haki hiyo si ya moja kwa moja kwani inasomwa pamoja na Ibara ya 30 ya Katiba hiyo hiyo.
Ibara hiyo pamoja na mambo mengine, inasema: “Kila mtu katika Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kufaidi haki za msingi za binadamu.”
Jaji alisema chini ya sheria iliyopo sasa, hakuna maombolezo ya kupunguziwa adhabu kwa mtu mzima aliyetiwa hatiani kwa mauaji ya kukusudia na kwa msingi huo, mikono yake imefungwa, hivyo Mhulula atanyongwa hadi kufa.
Licha ya hukumu hiyo, kiu ya wengi ni kujua namna tukio hilo la kikatili lilivyotokea, mashahidi wa Jamhuri waliyoyaeleza na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani na kumtia hatiani mshitakiwa hadi Jaji akaamua kumhukumu kifo.
Ushahidi uliotolewa unaonyesha kuwa Aprili 12,2025 saa 5:45 usiku, watu wawili, Joseph Mhulila ambaye ni baba wa mtoto na mzazi mwenzie, Daima Hongoli walitoa taarifa polisi kuhusu kupotea kwa mtoto wao, Timotheo Mhulila (miaka 4 na miezi 6).
Daima Hongoli ambaye alikuwa shahidi namba 1 wa Jamhuri, alieleza kuwa Joseph Mhulula ni baba wa mtoto na alikuwa akiishi Mtaa wa Mwalukosi na walikuwa hawajaoana, hivyo kila mmoja aliishi eneo tofauti.
Hongoli alikuwa akiishi na mtoto wake, ambaye sasa ni marehemu katika Mtaa wa Mtwivila na mara kwa mara baba wa mtoto alikuwa na mazoea ya kwenda kumchukua Ijumaa na kumrejesha Jumapilli jioni.
Kulingana na ushahidi wake, Machi 28, 2025 kwenye muda wa saa 1:00 usiku, mshtakiwa alimchukua mtoto kwa ahadi angemrudisha Jumamosi jioni.
Jioni ya Machi 29, 2025, Hongoli anasema alikwenda nyumbani kwa mshitakiwa na alimkuta akiwa na Timotheo na siku hiyo mama huyo alilala huko na kuondoka siku iliyofuata, yaani Machi 30 saa 2:00 asubuhi.
Wakati anaondoka, alimwacha mshitakiwa akiwa na mtoto na ilipofika jioni, alimtaka mzazi mwenzake amrudishe mtoto, lakini alijibu kuwa alikuwa amempeleka mtoto wa wazazi wake (bibi na Babu), wanaoishi jirani na angemrudisha siku inayofuata.
Aprili 9, 2025 saa 8:00 mchana, Hongoli anasema alizungumza na mwanae kupitia simu ya mzazi mwenzake na baadaye siku hiyo hiyo saa 1:30 usiku, mshitakiwa alifika nyumbani kwake na kuchukua nguo za mtoto lakini hakusema sababu za kuchukua nguo hizo.
Katika simulizi yake, Hongoli alisema Aprili 10, 2025 saa 4:00 asubuhi, alimpigia simu mshitakiwa na kumuuliza kwa nini alichukua nguo za mtoto na akamjibu kuwa mtoto wao amesafiri kwenda Songea mkoani Ruvuma na Babu yake.
Anasema alimtaka mzazi mwenzake ampe namba ya mtu ambaye amesafiri na mtoto wao lakini alikataa akisema hawezi kumpa namba ya baba yake kwa vile hamfahamu.
Katika mtiririko huo, Aprili 11, 2025, mshitakiwa alitembelea nyumbani kwa mzazi mwenzake ambapo shahidi huyo alimuuliza mahali alipo mtoto na alimjibu kuwa yuko kwa wazazi wake (wazazi wa mume) na yeye alimwamini mzazi mwenzake.
Aprili 12 ,2025 saa 1:30 usiku, shahidi huyo anasema alipokea simu kutoka kwa mzazi mwenzake akimweleza kuwa ameshamchukua mtoto kutoka kwa wazazi na kuwa muda huo alikuwa anakwenda kwake (kwa mshitakiwa) kumchukulia sweta.
Lakini dakika chache baadaye, mshitakiwa alimpigia tena simu mzazi mwenzake na kumjulisha kuwa mtoto wao amepotea baada ya kumwacha kwenye pikipiki na yeye akawa ameingia ndani ya Hoteli ya Kani, iliyopo Mtaa wa Mwalukosi.
Baada ya kusikia hivyo, mama wa mtoto akafunga safani kwenda Hoteli ya Kani ili kujua nini kinaendelea na alipofika hapo hotelini alimkuta mshitakiwa akiwa na rafiki yake aitwaye Charles, wakashirikiana kumtafuta mtoto hadi saa 6:00 usiku wa kuamkia Aprili 13 bila mafanikio.
Walienda pamoja kituo cha polisi kutoa taarifa za kupotelewa na mtoto lakini wakaambiwa warejee baada ya saa 24 na siku iliyofuata, shahidi huyo alikwenda kituoni kufuatilia maendeleo ya kutoweka kwa mwanae.
Mshitakiwa ambaye ni alikuwa akiendelea kumtafuta mtoto kwa kushirikiana na madereva wenzake wa bodaboda, ambapo polisi walimtaka atoe maelezo yake na baadae walimpigia simu mzazi mwenzake ili afike polisi.
Kwenye saa 6:00 mchana wa Aprili 14, 2025, mshitakiwa alifika kituo cha polisi ambapo alihojiwa huku mama huyo akishuhudia mahojiano hayo ambapo mshitakiwa aliwaeleza polisi kuwa alimchukua mtoto Aprili 13, jambo ambalo lilikuwa uongo.
Baada ya mahojiano hayo, polisi waliamuru mwanamume huyo awekwe mahabusu kama mshukiwa na wakamtaka mama huyo aendelee na harakati za kumtafuta mtoto.
Usikose mfululizo wa simulizi ya mauaji haya kesho ambapo tutakuletea namna mama wa mtoto alivyopokea taarifa nzito na za kushtua kutoka kwa baba mkwe.