Sababu radi kupiga Dar, jinsi ya kujikinga

Dar es Salaam. Katika kipindi hiki cha mvua, ili kujikinga na radi unapaswa kuepuka kukaa chini ya miti. Epuka kukaa katika eneo la wazi kama ufukweni au uwanjani, kwa sababu radi ikipiga huwa inatafuta kitu kirefu; kwa hiyo kama uko uwanjani wewe ndiyo unakuwa mlengwa.

Vilevile, kama upo ndani ya nyumba jiepushe kukaa karibu na madirisha au milango iliyo wazi; unatakiwa ukae sehemu iliyojificha. Lakini pia kama radi zinapiga sana unapaswa kuzima vitu vya umeme ambavyo kimsingi vina asili ya chuma.

Kitaalamu, radi ni mlipuko mkubwa wa nishati ya umeme unaotokea angani. Katika mawingu ya mvua kuna vipande vya barafu na matone ya maji vinavyogongana. Msuguano huo unatengeneza chaji chanya (+) juu ya wingu na chaji hasi (-) chini ya wingu.

Ardhi yetu ina chaji chanya (+). Wakati mvutano unapozidi, umeme unaruka kutoka kwenye wingu kuja ardhini ili kujisawazisha. Huo ndiyo mwangaza na kishindo tunachokiona.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Machi 19, 2026, Ramadhan Omary kutoka Ofisi Kuu ya Utabiri, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), amesema kwanza radi inaweza kujitengeneza katika eneo lolote, huku akisema kutokea kwake lazima kuwe na mawingu yanayosababisha.

Mvutano hasi na chanya kati ya wingu na ardhi ndio unaotengeneza umeme; ndiyo maana unaona radi imepiga mahali.

“Ikipiga ndipo unasikia muungurumo. Sasa hapa kuiona mwanga na muungurumo vimekaribiana ndani ya sekunde tatu, basi ujue radi hiyo iko karibu. Lakini ukiona mwanga halafu ukasikia muungurumo baada ya sekunde kumi, basi ujue iko mbali kama kilomita tatu hivi,” amefafanua.

Omary anasema radi ni umeme na ina kiwango kikubwa sana cha joto; ndiyo maana ikimpiga mtu anakuwa kama ameungua kwa sababu ya joto lililopo ndani yake.

Ni nadra sana radi kupiga mara mbili katika eneo moja; mara nyingi hupiga mara moja.

Kwanini Dar/Ukanda wa Pwani

Kimsingi, kutokea kwa radi kunahitaji hewa yenye unyevunyevu mwingi na joto ili kutengeneza mawingu mazito. Maeneo ya Pwani yana unyevunyevu mkubwa kutokana na Bahari ya Hindi, hivyo joto linapoongezeka mawingu yanakuwa na nguvu kubwa ya umeme.

Ukiangalia Dar es Salaam na mikoa ya Pwani ikiwemo Tanga, Lindi na Mtwara, iko karibu na bahari; kwa maana hiyo lazima kuwe na kiwango kikubwa cha mawingu.

Pia, hewa ya Pwani ina chembechembe za chumvi kutoka baharini. Chumvi ni kipitisha kizuri ya umeme. Hii inarahisisha radi kusafiri kutoka mawinguni kuelekea ardhini kwa urahisi zaidi.

“Ikumbukwe radi ni umeme, na zipo radi zinazofanyika ndani ya wingu lenyewe; zipo zinazofanyika kati ya wingu na wingu; na nyingine inayofanyika kutoka kwenye wingu kuja ardhini, ambayo ndiyo hatari zaidi.”

Kuhusu kujikinga, amesema kwa Dar es Salaam kuna baadhi ya majengo marefu ambayo yamewekwa vifaa vya kuzuia radi, hivyo huzuia radi.

Akielezea kuhusu vifaa vya umeme amesema kimsingi vimeundwa kwa asili ya chuma au bati ambavyo ni vipitishaji vya umeme na joto, hivyo vina uwezo wa kusababisha athari.

Radi inaweza kupiga kwenye mifumo ya umeme; sasa ikipiga ikakuta kifaa chako umechomeka, maana yake kitaathiriwa.

“Unapaswa kuzima, na kama kuna uwezekano unaweza ukachomoa kwenye swichi yako ili kujikinga. Lakini pia inapopiga radi hushauriwi kushika vitu vya chuma,” amesema.

Ikumbukwe jana Jumatano, Machi 18, 2026, wanafunzi watatu wa Shule ya Msingi Msongola, iliyopo wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam, walifariki dunia kutokana na kupigwa na radi wakati wakicheza shuleni.

Kulingana na mfumo wa radi ulivyo, huwa inatafuta njia fupi zaidi ya kufika ardhini. Mara nyingi hupiga vitu virefu vilivyojitokeza kama miti. Aidha, katika maeneo ya wazi, ikiwa mtu yupo katikati ya uwanja wa michezo, yeye ndiye anakuwa kitu kirefu zaidi katika eneo hilo, hivyo anavutia radi.

Zamani watu waliamini radi hupiga tu mikoa kama Tabora au Kigoma kwa sababu ina miti mingi na milima.