Kipigo chamzindua Nsajigwa Prisons | Mwanaspoti

KIPIGO cha mabao 2-1 ilichokipata Tanzania Prisons dhidi ya Singida Black Stars juzi kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, kimemwibua kocha wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’, baada ya kukiri umakini ndiyo sababu ya kukosa ushindi.

Mechi hiyo iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini, Dodoma, Prisons ilitangulia kupata bao la penalti dakika ya tatu, kupitia George Mpole, kisha Ayoub Lyanga, akaisawazishia Singida dakika ya sita.

Hata hivyo, wakati mechi hiyo ikionekana inaenda kumalizika kwa timu hizo kugawana pointi mojamoja, Singida ilipata bao la pili lililopeleka kilio baada ya beki raia wa Ghana, Ibrahim Imoro, kupiga ‘Frii-Kii’ ya moja kwa moja dakika ya 90.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nsajigwa alisema ukosefu mzuri wa utulivu ulichangia kipigo hicho, ingawa sio muda wa kuanza kuangalia hilo kwa sasa, isipokuwa jambo kubwa wanalolifanya ni kuandaa mikakati mizuri kwa mechi zilizokuwa mbele yao.

“Unapocheza na timu zenye wachezaji bora ni lazima uongeze umakini katika kila hatua, tumeshindwa kupata pointi moja kwa sababu ya umakini mdogo katika eneo la kujilinda, bado tuna nafasi ya kuzirekebisha kasoro zilizopo,” alisema Nsajigwa.

Nsajigwa, aliyejiunga na timu hiyo Februari 27, 2026, akichukua nafasi ya Mkenya Zedekiah ‘Zico’ Otieno, aliyeondoka kwa makubaliano ya pande mbili, Februari 25, 2026, tangu ajiunge na kikosi hicho amekiongoza katika mechi tatu za Ligi Kuu.

Katika mechi tatu, Nsajigwa alianza na suluhu (0-0) dhidi ya Azam FC, Machi 5, 2026, kisha akachapwa na Yanga bao 1-1 (Machi 12, 2026), huku akipoteza mbele ya Singida kwa mabao 2-1 (Machi 18, 2026).

Kichapo hicho kwa Prisons, kimeifanya timu hiyo kuendelea kubaki nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu na pointi 13, baada ya kushinda mechi tatu, sare nne na kupoteza 10, kati ya 17 ilizocheza, ikifunga mabao tisa na kuruhusu 19.