Simba yabanwa Kirumba, Azam Lake Tanganyika

WAKATI jana mashabiki wa Simba wakifurahia sare ya mchezo wa TRA United dhidi ya Yanga, leo Alhamisi ikawa zamu ya wenzao kushangilia baada ya wekundu hao kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Pamba Jiji kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Simba ilitumia dakika tatu pekee kufurahia bao lake lililofungwa dakika ya 33 na Anicent Oura, kisha Pamba Jiji ikaweka mzani sawa dakika ya 36 kupitia James Mwashinga.

Sare hiyo ilikuwa ya tatu katika mechi nne zilizopita za Simba na kuifanya timu hiyo kufikisha pointi 28 katika nafasi ya tatu, ipo nyuma kwa pointi moja dhidi ya Azam FC (29) ambayo nayo imetoa sare leo dhidi ya Mashujaa huko Kigoma kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika.

Simba ilianza dakika 45 za kipindi cha kwanza kwa nguvu ya kusaka bao la mapema huku kwa mara ya kwanza katika ligi kocha wa kikosi hicho, Steve Barker akiwaanzisha kwa pamoja Elie Mpanzu, Anicent Oura na Libasse Gueye.

Mpanzu alisimama kama mshambuliaji wa mwisho huku Oura na Gueye wakicheza katika maeneo ya pembeni ambayo wamezoeleka kutumika huku nyuma yao kukiwa na Clatous Chama.

Hesabu za Barker kumuanzisha Mpanzu zilijipa katika dakika 33 kufuatia shambulizi la kushtukiza ambapo Mkongomani huyo alitoa pasi ya mwisho kwa Oura aliyewapa furaha mashabiki wa Simba kwenye uwanja huo.

Wakati bado mashabiki wa Simba wakifurahia bao hilo, Pamba Jiji ilijibu mapigo kwa kusawazisha kwa faulo dakika tatu baadae kupitia James Mwashinga ambaye aliachia mkwaju mkali uliomshinda kipa wa Simba, Mahamadou Kassali na kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Simba ilirejea kipindi cha pili na kujaribu kutafuta bao la pili lakini Pamba Jiji ilionekana kuwa bora katika kujilinda huku ikiwa na idadi kubwa ya wachezaji kitu ambacho kiliwapa wakati mgumu Simba.

Dakika ya 74, Simba ilifanya mabadiliko ya kwanza kwa kumtoa Alassane Kante na kuingia Morice Abraham kwa lengo kuongeza nguvu kwenye eneo la kati, hata hivyo mabadiliko hayakuzaa matunda na kufanya mchezo huo kumalizika kwa sare kama ilivyokuwa kwa watani zao Yanga dhidi ya TRA.

Pamba Jiji imeendelea kulinda heshima ya nyumbani kwani katika msimamo wa ligi msimu huu, ni timu ya pili iliyokusanya pointi nyingi ikiwa kwake nyuma ya Yanga.

Pamba Jiji imekusanya pointi 19 nyumbani kwa kushinda mechi tano dhidi ya Namungo (1-0), Coastal Union (3-0), KMC (3-0), Fountain Gate (1-0) na Mashujaa (2-1).

Mechi ambazo imetoa sare ni dhidi ya TRA United (0-0), Singida Black Stars (1-1), Azam (2-2) na Simba (1-1). Katika mechi tisa ambazo imecheza nyumbani, Pamba Jiji imefunga jumla ya mabao 14 huku ikiruhusu matano.

Yanga ndio timu iliyokusanya pointi nyingi zaidi nyumbani, imeshinda saba na kutoa sare moja, hivyo imekusanya pointi 22 katika mechi hizo, wanaofuata nyuma mbali na Dodoma Jiji ni Mtibwa Sugar yenye pointi 17, Azam nafasi ya nne na pointi 15, Simba ipo nafasi ya saba ikiwa na pointi 13 huku ikicheza mechi sita tu nyumbani.

Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, Kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ aliiongoza Mashujaa kuikazia Azam katika mwendelezo wa ligi hiyo, ikiwa ni mechi ya tatu kwake tangu akabidhiwe kikosi hicho akianza na ushindi wa 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, sare ya 1-1 dhidi ya Fountain Gate na jana 0-0 mbele ya Azam.

Hata hivyo, Mashujaa imeendelea kuwa na rekodi mbaya mbele ya Azam kwani katika mechi tano za ligi kukutana kwao tangu msimu wa 2024-2025, haijashinda wala kufunga bao, ikipoteza mbili na sare tatu. Ilianza kufungwa 3-0, kisha 2-0, huku mechi zingine tatu zikimalizika kwa matokeo ya 0-0.