WAAMUZI Hussein Katanga kutoka Tabora na Ally Mnyupe wa Morogoro, wamekumbana na adhabu za kufungiwa kutokana na makosa yaliyotokea kwenye michezo waliyochezesha.
Waamuzi hao wawili wamefungiwa kwa mizunguko mitatu kufuatia Kamati ya Usimamizi wa Ligi kuwakuta na hatia kutokana na kushindwa kufanya uamuzi sahihi kwenye matukio mawili tofauti yanahohusisha penalti, yaliyotokea kwenye michezo miwili tofauti.
Katanga aliyechezesha mechi kati ya Singida Black Stars iliyopoteza kwa mabao 1-2 dhidi ya Simba iliyochezwa Machi 11, 2026 mkoani Singida, amekutana na adhabu hiyo baada ya kipa wa Simba, Djibrilla Kassali kumuangusha mshambuliaji wa Singida Black Stars, Joseph Guede kwenye eneo la hatari, lakini haikuamuliwa kuwa penalti.
Aidha, Singida nayo imetozwa faini ya Sh5 milioni kwa kosa la meneja mkuu wa timu hiyo, Othmen Najjar kutovaa sare za timu kama maofisa wengine kwa mujibu wa kanuni ya 17:8ya ligi kuhusu utaratibu wa mavazi.
Wakati Katanga akikutana na mkasa huo, ukamkuta pia Mnyupe ambaye alifanya kosa kama hilo akishindwa kutafsiri vyema sheria baada ya beki wa Azam, Fuentes Mendoza kumuangusha mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube kwenye eneo la hatari, mchezo ambao ulimalizika kwa timu hizo kushindwa kufungana, Machi 15, 2026 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Yanga nao wamepigwa faini ya Sh5 milioni kwa kosa la mashabiki wake kuwarushia chupa za maji waamuzi wa mchezo wao dhidi ya Azam, wakati wakitoka uwanjani.
Aidha shabiki wa Yanga, Carlos Mayangura amefungiwa kwa miezi 12 kwakosa la kuongoza mashabiki na maofisa wengine wa ulinzi, kuvunja madirisha ya chumba cha kuvalia na kusababisha uharibifu kwenye uwanja wa Airtel, kwenye mchezo dhidi ya Singida Black Stars uliochezwa Machi 5, 2026 na Yanga kushinda 0-3 ugenini.
Kwenye tukio hilo, Yanga nayo imetozwa faini ya Sh5 milioni na kutakiwa kugharamia uharibifu huo na maeneo mengine uliofanywa na mashabiki hao.
ADHABU/ MAONYO KUTOKA TPLB
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Machi 17, 2026 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;
Mechi Namba 72: Singida BS FC 0-3 Young Africans SC
Shabiki wa klabu ya Young Africans aliyetambuliwa kwa jina la Carlos Leonard Mayangura, ambaye amekuwa akiambatana na walinzi wa klabu hiyo, amefungiwa miezi 12 kwa kosa la kuongoza mashabiki na maofisa wengine wa ulinzi, kuvunja madirisha ya chumba cha kuvalia na kusababisha uharibifu.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:2 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Klabu ya Young Africans imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) na kutakiwa kulipa (milioni tano) na kutak gharama za matengenezo ya madirisha na maeneo mengine ya chumba cha kuvalia yaliyo-haribiwa na mashabiki hao.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:(1 & 3) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mechi Namba 111: Singida BS FC 1-2 Simba SC
Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Katanga Hussein kutoka Tabora amefungiwa mizunguko mitatu (3) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu katika mchezo huo.
Mwamuzi huyo alishindwa kufanya maamuzi sahihi kwa mujibu wa sheria baada ya golikipa wa klabu ya Simba, Djibrilla Kassali kucheza rafu dhidi ya mchezaji wa Singida BS, Joseph Guede ndani ya eneo la penati.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.8) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.
Klabu ya Singida BS ya mkoani Singida imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la meneja wa timu hiyo, Othmen Najjar kutovaa sare za timu kama maofisa wengine wa timu, kwa mujibu wa kanuni ya 17:8 ya Ligi Kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 104: Azam FC 0-0 Young Africans SC
Klabu ya Azam imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la kukataa kutumia chumba rasmi cha kuvalia kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo walitumia njia ya kuingilia vyumbani (corridor) kwa shughuli hiyo kabla ya kuanza mchezo, kinyume cha matakwa ya kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Ally Mnyupe kutoka Morogoro amefungiwa mizunguko mitatu (3) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu katika mchezo huo.
Mwamuzi huyo alishindwa kufanya maamuzi sahihi kwa mujibu wa sheria baada ya mchezaji wa klabu ya Azam, Fuentes Mendoza kucheza rafu dhidi ya mchezaji wa Young Africans, Prince Dube ndani ya eneo la penati.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.8) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.
Klabu ya Young Africans imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la mashabiki wake ku-warushia chupa za maji waamuzi wa mchezo tajwa hapo juu wakati wakitoka kiwanjani baada ya ku-malizika kwa mchezo huo
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Ligi ya Championship ya NBC
Mechi Namba 161: Polisi Tanzania 1-0 Kagera Sugar FC
Klabu ya Kagera Sugar imepewa Onyo Kali kwa kosa la kuchelewa kuwasili kwenye kikao cha kitaalam cha maandalizi ya mchezo (MCM) kuelekea mchezo tajwa hapo juu kinyume cha matakwa ya kanuni ya 17:2 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Wachezaji David Luhende na Erasto Nyoni wa klabu ya Kagera Sugar wametozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kila mmoja kwa kosa la kuonekana wakimwaga kimiminika kiwanjani wakati timu hiyo ilipozuru uwanja dakika chache baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Ushirika, Kilimanjaro, kitendo kilichotafsiriwa kama imani za kishirikina.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5(5.5) ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Mchezaji Andrew Vicent wa klabu ya Kagera Sugar amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni) kwa kosa la kumpiga ngumi mchezaji Tunga Said wa Polisi Tanzania wakati mchezo tajwa hapo juu ukiendelea kwenye uwanja wa Ushirika, Kilimanjaro.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5(5.2) ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Mechi Namba 165: Stand United FC 0-1 B19 FC
Klabu ya Stand United imetozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili) kwa kosa la mashabiki wake ku-warushia mawe na kuwatolea lugha za vitisho waamuzi wa mchezo tajwa hapo juu, jambo lililosaba-bisha waamuzi hao kusimamisha mchezo na kuondoka kiwanjani kwa kuhofia usalama wao.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Mechi Namba 168: Barberian FC 0-0 Mbeya Kwanza FC
Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Haji Mtondohima kutoka. Mtwara amefungiwa mizun-guko mitatu (3) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu katika mchezo huo.
Mwamuzi huyo alishindwa kufanya maamuzi sahihi kwa mujibu wa sheria akitoa adhabu ya penati kwa klabu ya Barberian baada ya mchezaji wa Mbeya Kwanza kujiangusha ndani ya eneo la penati.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.8) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.