TWCA yagawa vitabu kuhamasisha masomo ya biashara

Dodoma. Katika juhudi za kuimarisha elimu na kuwajengea wanafunzi msingi imara wa taaluma za biashara, Chama cha Wanawake Wahasibu Tanzania (TWCA) kimetoa msaada wa vitabu 310 vya masomo ya biashara kwa Shule ya Sekondari Chinangali.

Hatua hiyo imekuja kama mwanga mpya kwa wanafunzi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya uhaba wa vitabu, hali iliyokuwa ikiathiri uelewa wao darasani na hata kuwapunguzia motisha ya kujifunza.

Vitabu vilivyotolewa vinahusisha masomo ya hisabati, Book Keeping na Business Study kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza, pili na nne, masomo ambayo ni mhimili muhimu katika kujenga taaluma za biashara na uhasibu.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo leo Alhamisi Machi 19, 2026, Mwenyekiti wa TWCA, Mary Mabiti amesema kuwa msaada huo ni sehemu ya kurudisha kwa jamii sambamba na maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Machi 8, 2026.

Mkuu wa shule ya Sekondari Chinangali iliyopi Jijini Dodoma, Victor Salisali akizungumza na wanafunzi kuhusu utaratibu wa kupokea vitabu kutoka chama cha wahasibu wanawake Tanzania (TWCA) Machi 19, 2026 shuleni hapo Chinangali Jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa moja ya changamoto kubwa kwa wanafunzi, hasa wa kike, ni hofu ya masomo yanayohusiana na hesabu. Hofu hiyo imekuwa kikwazo cha wao kushiriki kikamilifu katika masomo ya biashara, licha ya umuhimu wake mkubwa katika maisha ya baadaye.

“Hii ni sehemu ya kurudisha kwa jamii ambapo kila mwaka huwa tunatoa msaada. Tumeshatoa msaada kwenye shule mbalimbali katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Lindi, Mtwara, Kigoma na Dodoma,” amesema Mabiti.

Ameongeza kuwa lengo kuu ni kuwawezesha wanafunzi kuona kuwa masomo ya biashara yanawezekana na yana nafasi kubwa katika kufungua fursa za ajira na ujasiriamali.

“Kwa mwaka huu tumeona tuje hapa Chinangali Sekondari kuleta vitabu kama sehemu ya maadhimisho ya mwaka huu ya wanawake duniani. Tumekuja pia kuwatia moyo wanafunzi waone kuwa masomo haya si magumu bali yanahitaji juhudi na nyenzo sahihi kama vitabu,” ameongeza.

Mabiti amesisitiza kuwa licha ya chama hicho kuwa cha wanawake, msaada huo unawanufaisha wanafunzi wote bila kujali jinsia, akieleza kuwa elimu ni haki ya kila mtoto na ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake, mmoja wa waanzilishi wa chama hicho, Grace Lesilwa amesema kuanzishwa kwa TWCA kulilenga kuongeza idadi ya wanawake katika taaluma za uhasibu na ukaguzi, ambazo bado zinaongozwa na wanaume katika soko la ajira.

Baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari ya Chinangali Jijini Dodoma.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Chinangali, Victor Salisali amesema msaada huo umefika kwa wakati muafaka kwani shule ilikuwa na upungufu mkubwa wa vitabu vya masomo ya biashara.

“Vitabu hivi vitawasaidia wanafunzi wetu kuelewa masomo kwa undani zaidi na kufanya vizuri kwenye mitihani yao,” amesema Salisali.

Wanafunzi pia wameelezea furaha yao, wakisema kuwa upatikanaji wa vitabu utawasaidia kufanya mazoezi, kufuatilia masomo darasani na kuongeza uelewa wao.

Lulu Lubeleje amesema hapo awali walikuwa wanapata ugumu kuelewa masomo kutokana na kukosa vitabu, hali iliyokuwa ikiwafanya wabaki nyuma darasani.

“Mwalimu alikuwa anasema tutajifunza sura fulani lakini kwa kuwa hatukuwa na vitabu tulikuwa hatuelewi. Sasa tutakuwa tunakwenda sawa na mwalimu, tutaelewa na kufaulu vizuri masomo yetu,” amesema Lubeleje.

Naye Jeremia Matereka amesema msaada huo unaonyesha wazi kuwa vitabu si tu nyenzo za kujifunzia bali ni daraja la mafanikio kwa wanafunzi hasa katika masomo ya biashara ambayo yanahitaji mazoezi, ufahamu wa kina na kujifunza kwa vitendo.

Amesema upatikanaji wa vitabu hivyo unatarajiwa kuwa chachu ya kuinua kiwango cha elimu na kuandaa kizazi chenye ujuzi na uwezo wa kushindana katika dunia ya biashara.