Dar es Salaam. Katika hatua inayotarajiwa kubadili mwelekeo wa ubora wa elimu nchini, Serikali inatarajia kuanza kuwapanga walimu wapya kulingana na viwango vyao vya elimu huku walimu wanaohitimu stashahada (diploma) wakielekezwa moja kwa moja kufundisha katika shule za msingi.
Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu ya mwaka 2014, toleo la mwaka 2023, unaolenga kuimarisha msingi wa elimu kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa imara tangu ngazi ya awali.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Machi 19, 2026, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi amesema mabadiliko hayo yanawahusu walimu wanaohitimu sasa na siyo waliopo kazini.
Hata hivyo, amesisitiza hakuna mwalimu yeyote atakayeshushwa daraja kwa kile alichoeleza kuwa mpango huo unalenga kupanga rasilimali watu wapya wanaoingia kwenye mfumo wa ajira.
“Huu ni utekelezaji wa sera iliyoboreshwa. Tunaanza na walimu wapya wanaohitimu sasa, na siyo kuwahamisha waliopo kazini. Tunataka kuwa na mpangilio sahihi wa walimu kuanzia ngazi ya chini,” amesema Profesa Mushi.
Amesema mageuzi hayo ni ya kimkakati na yanahitaji ushirikiano wa wadau wote ili kufanikisha lengo la kuinua ubora wa elimu nchini.
Naibu Katibu Mkuu huyo amesema hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji, hasa kwa kuimarisha elimu ya msingi ambayo imekuwa ikitajwa kuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya mwanafunzi katika ngazi zinazofuata.
“Haya ni mabadiliko ya muda mrefu. Tunataka kujenga mfumo imara wa elimu unaoanzia chini hadi juu. Ushirikiano wa kila mdau ni muhimu. Tunapowekeza nguvu katika elimu ya msingi, tunajenga msingi imara wa maarifa. Hii itasaidia wanafunzi kufanya vizuri zaidi wanapoendelea na masomo yao,” amesema Profesa Mushi.
Hatua hiyo imepokelewa kwa mitazamo tofauti kutoka kwa wadau wa elimu, huku baadhi wakiipongeza na wengine wakitaka maelezo ya kina zaidi kuhusu utekelezaji wake.
Rehema Mallya, ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi jijini Dar es Salaam, amesema mpango huo unaweza kuleta mabadiliko makubwa katika ubora wa elimu ya msingi.
“Kwa muda mrefu, tumekuwa tukihitaji walimu wenye ujuzi zaidi katika shule za msingi. Ikiwa walimu wa diploma wataanza kufundisha hapa, tunaweza kuona matokeo bora zaidi kwa wanafunzi,” amesema.
Mzazi na mdau wa elimu, John Mgaya, naye ameunga mkono hatua hiyo akieleza ni uwekezaji wa msingi kwa maendeleo ya taifa.
“Elimu bora inaanzia chini. Tukijenga msingi mzuri, hata sekondari zitapata wanafunzi wenye uwezo mkubwa zaidi wa kujifunza,” amesema.
Baadhi ya wachambuzi wa elimu waliozungumza na Mwananchi wameeleza hatua hiyo ina mantiki ya kitaaluma, lakini mafanikio yake yatategemea utekelezaji wake, huku wakisisitiza uwekezaji zaidi katika mazingira ya kufundishia ili mpango huo uweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
Mchambuzi wa sera za elimu, Dk Aika Kiwale, amesema ni muhimu kuhakikisha walimu wanaandaliwa kulingana na mahitaji ya ngazi ya msingi.
“Mbinu za kufundishia watoto wa shule za msingi ni tofauti na sekondari. Vyuo vya ualimu vinapaswa kuendana na mabadiliko haya ili kutoa walimu wanaokidhi mahitaji halisi,” amesema Dk Kiwale.
Mchambuzi huyo amesema mawasiliano ya wazi kwa wadau wote yatasaidia kuondoa hofu na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu sera hiyo.
Mhadhiri wa elimu, Profesa George Kahangwa, amesema tafiti zinaonyesha changamoto nyingi za ufaulu wa wanafunzi huanzia katika hatua za awali za elimu, hivyo kuwekeza walimu wenye sifa katika ngazi hiyo ni mkakati wa muda mrefu wa kuinua viwango vya elimu nchini.
“Kwa muda mrefu kulikuwa na mjadala kuhusu ubora wa elimu. Maboresho yamefanyika kwenye sera na mitaala, na mojawapo ya eneo lililoangaliwa ni elimu ya ualimu. Tumetoka mbali kwenye kuwapanga walimu; sasa tupo kwenye hatua nzuri.
Hata hivyo, mipango isipowekwa vyema, utekelezaji wake unaweza ukawa na shida. Ikumbukwe kwamba inaenda kuongeza bajeti kwa sababu huwezi kumlipa mwalimu wa diploma kile ulichokuwa unamlipa wa ngazi ya cheti,” amesema Profesa Kahangwa.
Mbali na hilo, mhadhiri huyo ameshauri Serikali kuwa na mpango madhubuti wa kuwapandisha walimu ambao wamejiendeleza kielimu ili wafanye kazi zinazoendana na ujuzi wao.
“Hawa wa diploma wanaenda shule za msingi, lakini huko pia wapo walimu waliojiendeleza, wengine hadi ngazi ya shahada ya uzamivu. Nafikiri kuna haja ya hawa watolewe wakafanye kazi kulingana na maarifa waliyokuwa nayo, ikiwemo kufanya utafiti au kufundisha ngazi za juu, siyo kuwaacha shule za msingi,” amesema Profesa Kahangwa.
Akijibu kuhusu hilo, Profesa Mushi amesema: “Ninachofahamu, upo utaratibu wa kuwapangia majukumu mapya wale waliojiendeleza kulingana na ujuzi waliopata; nafasi hiyo ipo.”
