TANZANIA YATAKIWA KUWEKA VIWANGO VYA UBORA WA HUDUMA ZA RADIOLOJIA KWA KIWANGO CHA KIMATAIFA

…………..

Wataalamu wa huduma za mionzi tiba na uchunguzi kutoka Taasisi za dini, Hospitali ya Taifa, Kanda, Maalum pamoja na zile binafsi wametakiwa kuhakikisha wanaweka na kuzingatia viwango vya ubora wa huduma vinavyokubalika kimataifa ili kuongeza tija na ufanisi katika utoaji wa huduma hizo.

Wito huo umetolewa na Mratibu wa Huduma za Radiografia kutoka Wizara ya Afya, Gerald Mrema, Machi 19, 2026, wakati akifungua warsha ya siku moja kwa wasimamizi na watoa huduma za mionzi tiba na uchunguzi kutoka taasisi mbalimbali nchini zinazojihusisha na utoaji wa huduma za radiolojia.

 Mrema amesema hayo kufuatia kukamilika kwa mapitio na maboresho ya mwongozo wa utoaji wa huduma za radiolojia, ambao umeboreshwa ili kuendana na viwango vya kimataifa na kuhakikisha huduma zinakuwa salama, bora na zenye kuaminika.

“Lengo kuu la Quality Manual ni kuhakikisha utoaji wa huduma unaendana na ubora unaotambulika kimataifa, Ili kupata ithibati (accreditation) ni lazima kuwa na mwongozo utakaoweka na kusimamia viwango vinavyotakiwa katika utoaji wa huduma za mionzi,” amesema Mrema.

Ameongeza kuwa upatikanaji wa ithibati utategemea utekelezaji madhubuti wa miongozo hiyo katika ngazi zote, ikiwemo menejimenti, rasilimali watu, matumizi sahihi ya vifaa pamoja na mifumo ya ukaguzi na ufuatiliaji wa huduma kuanzia hatua ya awali hadi mwisho.

Ameeleza kuwa wagonjwa wanapochagua hospitali kama Aga Khan au nyingine zenye hadhi ya juu, hufanya hivyo kutokana na kuamini ubora na viwango vya huduma vinavyotolewa.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki, mwakilishi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Dkt. Salehe Abdallah, amesema wataalamu wa radiolojia wana nafasi muhimu katika sekta ya afya kwani majibu wanayoyatoa husaidia madaktari wengine kufanya maamuzi sahihi ya matibabu kwa wakati.

Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia mradi wa Pandemic Fund, inaendelea kuboresha na kusimamia utekelezaji wa mwongozo wa ubora wa huduma za radiolojia katika ngazi zote, hatua inayolenga kuimarisha mfumo wa huduma za afya nchini na kuongeza ufanisi wa sekta hiyo.