KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars, Mkenya, David Ouma amesema kukosekana kwa kiungo mshambuliaji wa kikosi hicho, Marouf Tchakei, ni pigo kubwa kwa timu hiyo, ingawa ni nafasi pia nyingine kwa wachezaji wengine kucheza na kuziba pengo lake.
Nyota huyo raia wa Togo, aliyehusishwa kujiunga na Yanga katika dirisha dogo la usajili Januari 2026, kisha dili hilo kutibuka mwishoni, atakuwa nje ya uwanja hadi mwisho wa msimu wa 2025-2026 baada ya kupata majeraha ya misuli akiwa mazoezini.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma alisema ni pigo kwa timu hiyo kutokana na umuhimu wa mchezaji huyo, ingawa ukubwa wa kikosi hicho na wachezaji wengine bora waliopo, unatoa pia fursa kucheza katika michuano mbalimbali iliyobaki.
“Unapokuwa na wachezaji zaidi ya wawili wanaocheza nafasi moja tena kwa ufasaha inaweza isiwe tabu kwa benchi la ufundi, lakini tunapaswa kutambua kila mmoja ana aina yake ya uchezaji, hivyo tunamtakia kila la heri,” alisema Ouma.
Ouma alisema mbali na Tchakei, kiungo mwingine, Idriss Diomande, aliyeumia tangu Februari 8, 2026, katika mechi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria, anakaribia kurejea.
Tchakei aliyetua Tanzania, Julai 1, 2023, msimu wake wa kwanza wa 2023-2024, alionyesha kiwango bora, baada ya kufunga mabao tisa ya Ligi Kuu Bara, ingawa kwa msimu 2024-2025, alifunga mabao sita, huku 2025-2026, akiwa amefunga bao moja katika Ligi Kuu Bara, ikiwa ni mechi iliyomalizika kwa sare ya 1-1 dhidi ya Dodoma Jiji, Januari 16, 2026.
