Kazi: Namungo imenirejeshea kujiamini baada ya wakati mgumu Simba

DAKIKA 1530 katika mechi 17 za Ligi Kuu Bara msimu huu alizocheza beki wa kati wa Namungo FC, Hussein Kazi, amesema zimemwongezea kitu kikubwa, tofauti na msimu uliopita akiwa Simba na hakupata nafasi kubwa ya kucheza.

Msimu wa 2024-2025 wakati yupo Simba, Kazi alicheza mechi moja kwa dakika 10 dhidi ya KMC, jambo ambalo anasema lilimpunguzia kujiamini, tofauti na sasa ambapo anajiona kujiamini kwake kumeongezeka.

Kazi aliliambia Mwanaspoti namna ambavyo anajiona yupo fiti, anajiamini na anazidi kupambana kuhakikisha anaendelea kumshawishi Kocha Juma Mgunda kuendelea kumpa nafasi kucheza kikosi cha kwanza.

“Nimecheza dakika 90 mechi zote 17, natambua ushindani ni mkali unaonisaidia kujituma kwani najua mtu akikaa benchi anakuwa anatamani kucheza, hivyo akipata nafasi anaitumia kisawasawa,” alisema Kazi na kuongeza;

“Simba ilinisaidia kunipa uzoefu wa kutokukata tamaa licha ya kwamba nilikuwa sichezi, nilijengwa kujituma kwa bidii katika mazoezi binafsi, hivyo nilichokuwa nakihitaji zaidi ni kucheza na kwa sasa nacheza.”

Kuhusu Simba alisema kwa sasa ina mabadiliko na imerejea kwa uharaka kucheza kwa kuelewana licha ya kuacha wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza, hivyo anauona unaweza ukawa msimu wa kutimiza malengo iliyojiwekea klabu hiyo.

“Nawakubali mabeki wote Simba kwani ni wazuri, kwa wazawa Abdulrazack Hamza na Wilson Nangu ingawa wameumia, naamini watakaa sawa na wataendelea na mapambano,” alisema.