Global Publishers
March 20, 2026
0 Comments
Mkazi wa Dar es Salaam, Oswad Kimario (27), ambaye ni mzaliwa wa Moshi mkoani Kilimanjaro, amedai kutapeliwa kiasi cha shilingi milioni 2.7 baada ya kushawishiwa kuwekeza kwenye biashara ya viatu.
Akizungumza na waandishi wa habari Machi 19, 2026, Kimario amesema fedha hizo alizipata baada ya kuuza pikipiki yake pamoja na baadhi ya mali za ndani alipokuwa akifanya kazi ya usafirishaji maarufu kama bodaboda jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa maelezo yake, alishawishiwa na rafiki yake wa muda mrefu, Ally Mrangi, mkazi wa Arusha, ambaye alimueleza kuhusu fursa ya biashara ya viatu yenye faida kubwa.
Kimario anadai kuwa rafiki yake huyo alimshawishi kuwa watakuwa wakinunua viatu kutoka Nairobi, Nairobi kwa bei nafuu na kuviuza Arusha kwa faida.
Amesema alifika Arusha Machi 17, 2026 kwa ajili ya kuanza biashara hiyo, ambapo alikutana na rafiki yake na kuombwa kukabidhi fedha zote kiasi cha shilingi milioni 2.7 kwa ajili ya kununua mzigo.
Hata hivyo, baada ya kukabidhi fedha hizo, Kimario anadai kuwa rafiki yake alitoweka na hajulikani alipo hadi sasa. Juhudi za kumtafuta kupitia simu na mitandao ya kijamii zimeelezwa kushindikana.
Mwandishi wa habari pia alijaribu kumtafuta Ally Mrangi ili kupata upande wake wa maelezo, lakini hakupatikana.
Kutokana na tukio hilo, Kimario amesema anajutia uamuzi wake na kwa sasa amebaki bila mtaji, hali iliyomlazimu kuomba msaada kwa Watanzania ili aweze kurejea kwenye shughuli zake za awali za bodaboda.