TMA yatoa tahadhari ya mvua kubwa, wananchi waonywa

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya tahadhari na angalizo la mvua kubwa kwa mikoa kadhaa, ikisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari stahiki ili kuepuka madhara yanayoweza kutokana na hali ya hewa mbaya.

Katika taarifa hiyo, TMA imetahadharisha kuwa Ijumaa ya  Machi 20, 2026, kunatarajiwa kuwa na mvua kubwa kwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia), Tanga, Kagera, Geita, Mwanza, Mara, Simiyu, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe, pamoja na visiwa vya Pemba na Unguja. 

Taarifa hiyo inaeleza kuwa uwezekano wa kutokea ni mkubwa ikibainisha kuwa athari mbaya zinazoweza kutokea kwa wastani, huku athari zinazotarajiwa zikibainisha mafuriko katika baadhi ya maeneo ni kuathirika kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi.

Kwa Jumamosi ya Machi 21, 2026, TMA imetoa angalizo la mvua kubwa kwa mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tabora, Singida na Tanga, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Aidha,   Mamlaka hiyo inasisitiza wananchi kuzingatia tahadhari na kujiandaa ipasavyo ili kuepuka madhara yanayoweza kuambatana na mvua hizo.
 Siku mbili mfululizo kuanzia Jumapili Machi 22 na Jumatatu yake, TMA imeonesha  kupungua kwa hatari ya mvua kubwa katika siku hizo.

Kwa taarifa hiyo, TMA inasisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuzingatia na kujilinda kwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa, kuepuka kuingia katika maeneo hatarishi kama mito na mabonde, na kuhakikisha familia zao ziko salama wakati wa mvua hizo zikiendelea kunyesha.

Angalizo la TMA limekuja wakati ambao baadhi ya maeneo yamekuwa yakikumbwa na mafuriko na kuathiri makazi ya watu na shughuli zao kutokana na mvua kubwa, jambo linaloonyesha umuhimu wa tahadhari zinazotolewa. 

Hali hii inakumbusha wananchi kwamba kuzingatia tahadhari zinazotolewa ma mamlaka za hali ya hewa, ni njia bora ya kuepuka madhara makubwa ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini.