Wiki za karibuni mstaafu wetu amekuwa akishangazwa na mfululizo wa matangazo kutoka hizi benki kadhaa za dotcom zikijinasibu kwamba zitakuwa zinawasaidia wastaafu ‘kwa kununua madeni ya mikopo yote tuliyojiingiza kwa shida zetu zisizoisha, halafu benki hizo zitatusaidia kwa kutukopesha mikopo mingine juu ya ile iliyo nunuliwa. Pole yetu.
Iko hivi. benki zinazodai kuwa ziko karibu na wananchi, wakiwemo wastaafu, miaka michache iliyopita zilisema zinatoa mikopo midogo kwa wastaafu ili kuwasaidia katika shida zao, hususan ile mikopo ya matibabu ya bure kwa wazee wenye umri kuanzia maka 60, ambao ndio umri rasmi wa kustaafu.
Ndio umri rasmi wa kustaafu, lakini cha kushangaza, tunajua kuwa wastaafu wote ni sawa lakini wastaafu wengine wanakuwa zaidi kuliko wastaafu wengine, chambilecho Muingereza George Orwell na Shamba lake la Wanyama.
Wastaafu hawa wanaokuwa zaidi ya wengine huwa hawastaafu na miaka 60 kama sheria inavyosema bali hufikisha hata miaka 70 mpaka 80 wakidunda mzigo na kila siku wakiteuliwa kuongoza ama tume hii au ile, ama taasisi hii au Ile; huku wasomi wetu wanaomaliza vyuo wakiishia kusaka ajira kwa tochi.
Haya, benki hizi zinazodai kuwa ni za wananchi zikatoa mikopo midogo kwa wastaafu na tukakubali kukatwa moja kwa moja rejesho na riba ya mikopo hiyo kutoka kwenye pensheni ya mwezi.
Tabu ikawa riba ya mikopo hiyo ikawa kama ile riba ya wafanyabiashara. Kwa maana kwamba wote walikuwa wakibamizwa riba moja, hakuna cha kupunguza riba ya mstaafu wala nini. Kila Mtu atajiju!
Taabu ya mikopo hiyo toka mwaka juzi ikawa ile wastaafu akina sisi wa kima cha chini tuliokuwa tukipata pensheni ya shiling laki moja na elfu tano, kwa miaka ishirini nyuma, tukaishia kupata pensheni ya shilingi elfu 48, baada ya riba na rejesho kufanya vitu vyake kilaaini kwenye mikopo tuliyokopa macho juu!
Inashangaza sana kwa pensheni ya shilingi elfu 48 kwa mwezi bado wastaafu waliendelea kuishi japo kwa mateso makubwa, na hakuna hata mwenye huruma aliyesikia kilio cha maumivu cha wastaafu wa Sh105,000 kwa mwezi, cha kutaka waongezwe pensheni yao ili angalau waweze kujihami na hali ngumu ya maisha iliyokuwa ikimkabili kila mtu, zaidi wastaafu.
Sio kujihami tu bali kuweza kukabiliana na mtihani wa ‘matibabu ya bure kwa wazee’ ambao uliishia kuwa maneno ya kanga tu, huku wazee wakiishia kununua, rudia kununua, panado tu kutibu kisukari na BP magonjwa ya wastaafu. yenye kawaida ya kuzuka na kushika kasi mtu anapostaafu na yale matibabu ya dezo aliyokuwa akipata ofisini kuwa ‘kwishine’!
Kwa nini magonjwa hayo yasishike kasi wakati mashine ya kupimia kisukari’ ni Sh50,000 na ile ya kupimia BP bei yake ni mara mbili ya pensheni ya mstaafu iliyobamizwa na riba huku benki ikitamba kabisa kuwa inawasaidia wastaafu!…labda kwa kuwahimiza kwenda Kinondoni fasta!
Tunaishukuru Siri-kali na kibubu viliposhituka na kuwapa nyongeza ya pensheni wastaafu wa kima cha chini, kama siyo cha chizi, kuwa shilingi Laki mbili na nusu kwa mwezi, inayosaidia angalau watoke kule kwenye elfu 48 kwa mwezi baada ya kukatwa riba na marejesho ya mikopo tuliyodhani itapunguza shida zetu, kumbe imeziongeza!
Angalia sasa, ghafla kumezuka matangazo kibao ya hizi benki zetu za dotcom yakitutangazia kuwa kama madeni yetu yameishafika nusu, basi ziko tayari kuyanunua madeni hayo na kisha kutupa mkopo mwingine katika kile wachodai ni kuwasaidia wastaafu’….kama sio kuwasaidia kumaliza haraka nyongeza ya pensheni ya laki mbili unusu waliyopewa!
Iko hivi. Kweli wanakulipia mkopo wako uliobaki na wanakukopesha mkopo mwingine, mathlani wa Shilingi milioni tatu lakini wanatoa ule mkopo unaodaiwa halafu ndio wanakupa zilizobaki. Yaani kama mkopo wa zamani ulikuwa umebaki Shilingi milioni moja unusu, wanachukua hizo milioni moja unusu walizokulipia, kisha wanakupa mkopo mpya wa shilingi …milioni moja nusu japo umeomba milioni tatu!
Kibaya zaidi sasa ni kuwa kama mkopo wako huo wa zamani ulikuwa umebakisha miezi 16 kwisha, hawaifuti hiyo miezi 16 bali wanaiongeza na miezi ya mkopo mpya. Inashangaza! Maana ulikuwa kama wamefuta deni la zamani walipaswa pia kufuta na umri wa deni la zamani na kuweka umri wa deni lao jipya! Wastaafu wengi wametoka kapa hapa, kama mimi nilivyotoka kapa!
Matokeo yake mstaafu unajikuta una mkopo mpya wa shilingi milioni tatu ambazo kiuhalisi umepata Shilingi milioni moja unusu keshi, lakini utakugharimu miaka 6 hadi mwaka 2029, kama hujakuwa tayari mkazi wa Kinondoni! Wastaafu wenzangu waichunguze vizuri mikopo ya kulipiwa kabla ya kuingia humo macho juu juu!
0755 340606 / 0784 340606
