Dar es Salaam. Sikukuu ya Eid ni miongoni mwa siku muhimu zaidi kwa Waislamu duniani, ikiwa ni hitimisho la ibada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Siku hiyo huadhimishwa kwa furaha, ibada na mshikamano wa kijamii.
Hata hivyo, mbali na sherehe, kuna mambo kadhaa ya msingi ambayo Muislam anapaswa kuyazingatia ili kuifanya siku hiyo kuwa yenye baraka na manufaa zaidi.
Kwanza, ni Sunna kwa Muislam kuanza siku ya Eid kwa kula kitu kidogo kabla ya kuelekea msikitini kwa ajili ya Swala ya Eid, ikiwa ni ishara ya kumalizika kwa mfungo wa Ramadhani.
Pili, siku ya Eid ni ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya uhai na uwezo wa kutekeleza ibada ya Saumu, hivyo Waislamu wanahimizwa kuongeza shukrani na dua.
Tatu, kabla ya kuswali Swala ya Eid, kila Muislam mwenye uwezo anatakiwa kutoa Zakatul-Fitr kwa ajili ya kuwasaidia wenye uhitaji, ili nao waweze kushiriki kikamilifu katika furaha ya siku hiyo.
Nne, usafi binafsi ni muhimu. Inapendekezwa kuoga, kuvaa nguo safi au mpya na kwa wanaume kujipaka manukato, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku hiyo kwa heshima.
Tano, Waislamu wanashauriwa kwenda msikitini pamoja na familia zao, wakiwemo wanawake na watoto, ili kushiriki kwa pamoja ibada ya Swala ya Eid.
Sita, kusoma Takbira ni sehemu muhimu ya maandalizi ya Eid, zikianza tangu usiku wa kuamkia Eid hadi muda wa Swala unapowadia.
Saba, baada ya Swala ya Eid, ni vyema kubaki na kusikiliza mawaidha ya Eid, ambayo hutoa maelekezo muhimu kwa jamii.
Nane, ni Sunna kubadilisha njia wakati wa kwenda na kurudi kutoka msikitini, jambo linaloashiria kueneza furaha na ujumbe wa Eid katika jamii.
Tisa, baada ya ibada, Waislamu husherehekea kwa kutembeleana na kubadilishana salamu na ndugu, marafiki na majirani, hali inayokuza mshikamano wa kijamii.
Kumi, kutoa sadaka na kusaidia wahitaji ni jambo la msingi siku ya Eid, ili kuhakikisha kila mmoja anapata nafasi ya kufurahia siku hiyo.
