Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Kamishna wa Polisi (CP) Suzan Kaganda, ametembelea ofisi za Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA) zilizopo mjini Harare na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa TPA nchini humo, Bi. Kulthum Boma kuhusu namna ya kuimarisha huduma na kuongeza ufanisi katika usafirishaji wa mizigo kupitia bandari za Tanzania.
Ziara ya Mheshimiwa Balozi Kaganda ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Diplomasia ya Uchumi, ikiwa na lengo la kutambua na kuendeleza mchango wa TPA katika usafirishaji wa mizigo kutoka bandari za Tanzania kwenda nchi za Kusini mwa Afrika, ikiwemo Zimbabwe.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bi. Kulthum Boma alieleza kuwa ofisi hiyo, yenye jukumu la masoko na huduma kwa wateja, imekuwa na mchango chanya katika kuongeza shehena ya mizigo inayoingia Zimbabwe kupitia bandari za Tanzania tangu kufunguliwa kwake rasmi mwaka 2023.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi Kaganda amepongeza mafanikio hayo na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya ofisi ya TPA na Ubalozi.
Vilevile ameshauri kuandaliwa kwa mikutano na wadau pamoja na wafanyabiashara nchini Zimbabwe ili kutumia majukwaa hayo kutoa elimu na kuongeza uelewa kuhusu matumizi ya bandari za Tanzania.
Hatua hiyo inatarajiwa kuchangia zaidi katika kukuza biashara na kuongeza pato la Taifa.

.jpeg)
.jpeg)