Dar es Salaam. Alikuwa binti mwenye ndoto kubwa, lakini safari ya kuzifikia haikuwa nyepesi. Hakuwa na elimu ya juu wala ujuzi wa kutosha, zaidi hakukuwa na mazingira rafiki ya kumwezesha kufikia alichokuwa anakitamani maishani.
Katika harakati za kujitafuta, alianza kama msaidizi wa wasusi katika moja ya saluni jijini Dar es Salaam. Akiwa katika mazingira hayo, alijifunza hatua kwa hatua mbinu za ususi, akijijengea uwezo kwa vitendo.
Baadaye, alipoanza kujiamini, alianza kutafuta wateja wake binafsi, wakati mwingine akiwafuata hadi nyumbani ili kuwahudumia.
Hivyo ndivyo safari ya Lucy Oisso ilivyoanza, safari ya kupambana na hali yake ili kujenga mafanikio na kufikia uhuru wa kiuchumi. Hakuwa na hakika kuwa changamoto alizopitia ndizo zingekuwa daraja la kumfikisha kwenye mafanikio makubwa anayojivunia leo.
Hakuwahi kukata tamaa. Kila siku alikuwa akitafuta fursa mpya, akiamini ipo siku angefanikiwa na kuwa na kile alichokuwa anakitamani. Leo hii, juhudi hizo zimemfanya ajulikane kwa jina la Lucy Bridal Solution.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Lucy anasema safari yake ya mafanikio ilianza katika saluni aliyokuwa akifanya kazi kama msusi.
Hata hivyo, alitamani kuongeza ujuzi wake, na mwaka 2016 alijiunga na mafunzo ya upambaji (make-up). Ndoto hiyo ilikwama njiani kutokana na kushindwa kumudu ada.
Licha ya kushindwa kukamilisha mafunzo, hakutoka mikono mitupu. Ujuzi alioupata ulimwezesha kuanza kuwahudumia baadhi ya wateja, na mwaka huohuo alifanikiwa kumpamba bibi harusi wake wa kwanza, hatua iliyokuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa.
Akiendelea kusuka na kupamba wateja mbalimbali, Lucy aliweza kuweka akiba ndogo ya fedha. Mwaka 2017, akafungua saluni yake ya kwanza, ikiwa na vifaa vya msingi tu, yaani kioo kimoja na mashine ya kukaushia nywele moja, wengi wanaita ‘drayer.’
“Sikuwa na kiti. Mteja akija, nililazimika kuazima kiti kutoka kwa jirani ili nimhudumie,” anasimulia.
Kutokana na changamoto za mwanzo, alipokosa wateja, alibuni njia mbadala ya kuongeza kipato kwa kutengeneza vibanio vya nywele vya aina mbalimbali na kuviuza kwa wateja wake.
Kadiri biashara ilivyokuwa ikikua, alipata wazo la ubunifu zaidi, kuwaomba maharusi wamwachie magauni yao baada ya harusi ili ayakodishe kwa wengine, kisha wagawane mapato. Wazo hilo lilizaa matunda.
“Mwaka 2018 nilihamia Mbezi. Niliendelea na kazi ya kusuka, kupaka rangi kucha na kukodisha magauni ya harusi, ingawa wakati huo hayakuzidi manne,” anasema.
Biashara iliendelea kukua, na mwaka mmoja baadaye Lucy anasema alihamia katika eneo kubwa zaidi lenye fremu mbili, moja kwa huduma za nywele na nyingine kwa biashara ya magauni ya harusi.
Hata hivyo, mafanikio yalipozidi kuongezeka, mwaka 2022 alilazimika tena kuhamisha ofisi zake kutokana na eneo kuwa dogo.
Lucy anasema anakumbuka siku moja alipokuwa akimhudumia mteja wake, alipewa wazo la kuagiza magauni kutoka China. Hakusita, alilifanyia kazi wazo hilo.
“Nikaona ni wazo zuri litakalokuza biashara yangu. Kila nilipopata fedha, nilimtumia mtu wangu aliyekuwa China, naye aliniagizia magauni,” anasema.
Hatua hiyo ilimpa msukumo wa kujitangaza zaidi kupitia mitandao ya kijamii, redio na televisheni ili kufikia wateja wengi zaidi.
Mwaka 2023, Lucy anasema alifanya safari yake ya kwanza kwenda China, ikiwa pia mara yake ya kwanza kupanda ndege na kusafiri nje ya nchi. Safari hiyo haikuwa ya utalii, bali ya biashara.
“Ilikuwa safari ya kwanza, lakini nilipata hasara kwa sababu baadhi ya mzigo haukuwa kama nilivyochagua. Hata hivyo, sikukata tamaa. Niliona kufika China ni mafanikio makubwa kwangu,” anasema Lucy.
Kadiri alivyoendelea kusafiri na kufanya biashara na wazalishaji wa nje, alianza kujenga uaminifu na kushirikiana na viwanda mbalimbali. Hapo ndipo ndoto yake ya kuwa mbunifu wa magauni ya harusi ilipoanza kuchukua sura mpya.
Sambamba na hilo, anasema alianza pia kuagiza maua na kutengeneza mapambo ya harusi kwa mitindo tofauti, akilenga kumpa mteja huduma zote sehemu pamoja.
Kwa sasa, Lucy anashona magauni anayoyabuni mwenyewe kwa kushirikiana na viwanda vya China na Uturuki. Amefanikiwa kupanua biashara yake, na sasa anamiliki maduka mawili ya nguo za harusi, moja likiwa Sinza, Dar es Salaam, na lingine jijini Mwanza.
Aidha, anamiliki duka la nguo za sherehe na saluni ya wanawake jijini Dar es Salaam.
Lucy pia anajivunia kuwahudumia wateja kutoka nje ya nchi, ama wanaokuja Tanzania moja kwa moja au kupitia mawakala wake waliopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Nigeria na Zambia, ambako huuza bidhaa kwa bei ya jumla.
“Niliona kufungua maduka katika nchi hizo kungekuwa na gharama kubwa, hivyo nikachagua kutumia mawakala wa huko kwa sababu wanaelewa soko lao na mahitaji ya wateja wao,” anasema.
Pamoja na mafanikio hayo, Lucy anatamani elimu kuhusu biashara hii ienee zaidi kwa vijana ili wachangamkie fursa zilizopo.
Anasema anaamini kadri wafanyabiashara wanavyoongezeka, ndivyo ushindani na ubunifu unavyoongezeka. “Hii inaweza hata kuchochea kuanzishwa kwa viwanda vya ndani, ili kuhudumia soko la ndani kwa bidhaa bora,” anasema.
Anasisitiza pia umuhimu wa kutambua mchango wa wafanyabiashara wa nguo za harusi, akisema mara nyingi hawapati nafasi sawa kama wabunifu wengine.
“Watu wa aina yangu, hata tukipata tuzo, ni mara chache sana. Tumesahaulika,” anasema.
Anatoa wito kwa jamii kuelimishwa kuhusu ubora wa nguo za kukodi au zilizo tayari, akieleza kuwa wengi bado wana mtazamo potofu.
“Watu wengi wanafikiri nguo za kukodi ni za bei nafuu au za kiwango cha chini, jambo ambalo si kweli. Sasa kuna nguo zilizoandaliwa kwa ubora wa hali ya juu, hata zaidi ya baadhi ya zinazoshonwa hapa,” anafafanua.
Anaongeza kuwa kutumia nguo zilizopo kunapunguza usumbufu na kuokoa muda, tofauti na kushona nguo mpya ambazo zinaweza kuleta changamoto zisizotarajiwa.
“Unapokuja kwetu, unaweza kupima nguo tofauti hadi upate inayokufaa vizuri kulingana na umbo lako. Hii inapunguza msongo wa mawazo, hasa katika maandalizi ya harusi,” anasema.
Licha ya mafanikio hayo yote, Lucy bado anaendelea kuota ndoto kubwa zaidi huku akiamini safari yake bado haijafika mwisho, akijipanga kufanya mambo makubwa zaidi katika siku zijazo.
