Simiyu. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Itilima, mkoani Simiyu, Mhuli Ngeleja amefariki Machi 18, 2026 huku CCM ikimtaja kama kiongozi shupavu na mwadilifu.
Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Machi 20, 2026 na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, imeeleza kuwa chama kimepoteza kiongozi shupavu, mwadilifu na aliyejitolea kwa dhati kukitumikia chama na wananchi.
“Tumejawa na huzuni kuu kwa kupoteza nguzo muhimu ndani ya chama, aliyejipambanua kwa uchapakazi na uzalendo wa hali ya juu,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa marehemu Ngeleja alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha umoja wa wanachama, pamoja na kusukuma mbele maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Wilaya ya Itilima na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed, amesema kuwa chama kipo katika maandalizi ya taratibu za mazishi huku akiahidi kutoa taarifa kamili baadaye.
CCM pia imetoa pole za dhati kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na wanachama wote wa CCM Wilaya ya Itilima na Mkoa wa Simiyu kwa msiba huo mkubwa.
Mwanachama wa CCM wilaya ya Itilima, John Shija amesema kifo cha Ngeleja ni pigo kubwa kwa chama na jamii.
“Tumepoteza kiongozi aliyekuwa karibu na wananchi, msikivu na mwenye moyo wa kusaidia. Ni pengo kubwa ambalo halitakuwa rahisi kuzibika,” amesema Shija.
Naye mwanachama mwingine, Maria Kija, ameongeza kuwa marehemu alikuwa chachu ya maendeleo katika wilaya hiyo.
“Mzee Ngeleja alikuwa mstari wa mbele kuhamasisha maendeleo na mshikamano. Kifo chake kimetuumiza sana sisi wanachama na wananchi wote wa Itilima,” amesema Kija.
