Na Ashrack Miraji Torch Media
Wakulima wa kahawa katika Kata za Kilema Kati na Kilema Kaskazini, wilayani Moshi, wamepongeza juhudi za Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Enock Koola, kwa kuwezesha upatikanaji wa miche laki tano ya kahawa ili kufufua zao hilo muhimu kiuchumi.
Pongezi hizo zimetolewa Machi 19, 2026 wakati wa ziara ya siku ya pili iliyoandaliwa na mbunge huyo, ambapo Katibu wake, Iddy Mfinanga, aliwakilisha dhamira ya mbunge ya kushirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha kilimo cha kahawa katika jimbo hilo.
Katika ziara hiyo, ilielezwa kuwa lengo kuu la mpango huo ni kuongeza tija ya uzalishaji, kuboresha kipato cha wakulima na kukuza mchango wa zao la kahawa katika uchumi wa eneo la Vunjo.
Maafisa kilimo kutoka halmashauri ya wilaya walitumia fursa hiyo kutoa elimu ya kitaalamu kwa wakulima kuhusu mbinu bora za kuandaa mashamba, kutunza kahawa na kuongeza uzalishaji kwa kutumia teknolojia sahihi za kilimo.
Aidha, wakulima walihimizwa kupima afya ya udongo ili kubaini mahitaji ya virutubisho, huku wakielezwa kuwa huduma hiyo inatolewa bure kupitia wataalamu wa halmashauri.
Kwa upande mwingine, maafisa kutoka TAKUKURU walisisitiza umuhimu wa uadilifu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo, wakitoa rai kwa viongozi na wananchi kuhakikisha uwajibikaji unazingatiwa ili rasilimali ziwanufaishe wote kwa usawa.
Katika kukuza soko la zao hilo, wadau kutoka J.S Premium Product walitoa uhakika wa soko la kahawa kimataifa, wakibainisha kuwapo kwa mahitaji makubwa hasa nchini Japan, hususan kwa kahawa ya kilimo hai inayolimwa kwa wingi Vunjo.
Walieleza kuwa kampuni hiyo iko tayari kununua kahawa kwa bei yenye ushindani kutokana na uhitaji mkubwa uliopo katika soko la dunia.
Wananchi wa kata hizo walieleza kuwa ziara hiyo imeongeza uelewa na kuamsha ari mpya ya kufufua zao la kahawa, huku wakisisitiza kuwa upatikanaji wa miche hiyo utasaidia kuongeza uzalishaji katika miaka ijayo.

