Global Publishers
March 20, 2026
0 Comments
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema jeshi la polisi limefanikiwa kuwakamata watu wawili akiwemo Rehema Maulidi (42), kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Athumani Nyanza.
Akizungumza na vyombo vya habari, Kamanda Muliro alisema kuwa mtuhumiwa huyo pamoja na mwenzake mmoja ambaye jina lake halikutajwa mara moja, wanashikiliwa na wanaendelea kuhojiwa ili kubaini ukweli wa tukio hilo.
Alieleza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea kufanyika ili kupata taarifa zaidi kuhusu mazingira ya tukio hilo pamoja na watu wengine wanaoweza kuhusika.
Jeshi la Polisi limewahakikishia wananchi kuwa linaendelea kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha haki inatendeka, huku likitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukamilisha uchunguzi.
Tukio hilo la mauaji limeibua hisia mbalimbali miongoni mwa wakazi wa Dar es Salaam, huku familia, ndugu na marafiki wa marehemu wakiendelea kuomboleza msiba huo.
