Global Publishers
March 20, 2026
0 Comments
Simulizi ya kusikitisha imeibuka kufuatia kifo cha Muongozaji wa filamu, Athumani Nyanza, ambapo familia yake imeeleza kuwa tukio hilo lina utata mkubwa na linaashiria mauaji ya kikatili.
Akizungumza kwa uchungu, baba mdogo wa marehemu amesema kuwa tangu mwanzo kulikuwa na viashiria visivyo vya kawaida hadi walipofuatilia kwa kina na kugundua ukweli wa tukio hilo. Ameeleza kuwa familia ilipata taarifa tofauti kuhusu kutoweka kwa marehemu kabla ya hatimaye kubaini kilichotokea.
Kwa mujibu wa maelezo yake, inadaiwa kuwa marehemu aliuawa na mwanamke anayetajwa kuwa mama wa mtoto wake, kisha mwili wake kufukiwa karibu na nyumba yake iliyopo Mtaa wa Kimyakimya, eneo la Chanika jijini Dar es Salaam.
Simulizi hiyo imeacha maswali mengi kwa umma, huku familia ikilitaja pia suala la uwepo wa baadhi ya maafisa wa usalama, akiwemo afande pamoja na mkuu wa upelelezi, ambao wanadaiwa kujitokeza katika mchakato wa uchunguzi wa tukio hilo.
Familia imeitaka mamlaka husika kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha haki inatendeka kwa marehemu, huku wakisisitiza kuwa kifo hicho hakiwezi kuachwa bila majibu.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro leo Machi 20, 2026 amesema jeshi la polisi limefanikiwa kuwakamata watu wawili akiwemo Rehema Maulidi (42), kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya hayo.