TIA yaboresha mitaala kukidhi soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia

Morogoro. Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) imeendelea kuimarisha ubora wa mafunzo kwa kuboresha miundombinu ya ufundishaji na kufanya mapitio ya mitaala, hatua inayolenga kuzalisha wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

Akizungumza leo Machi 20, 2026 mjini Morogoro katika kikao cha tatu cha Baraza Kuu la tano la wafanyakazi wa TIA, Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa William Amos Pallangyo, amesema juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa taasisi kuhakikisha elimu inayotolewa inaleta tija kwa mhitimu na taifa kwa ujumla.

“Tumekuwa tukiboresha utoaji wa elimu katika taaluma mbalimbali kwa kufanya mapitio ya mitaala na kuanzisha kozi mpya zinazokwenda sambamba na mahitaji ya soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia. Hii imetuwezesha kufikia zaidi ya wanafunzi 37,000 katika kampasi zetu zote,” amesema Profesa Pallangyo.

Ameongeza kuwa TIA itaendelea kushirikiana na wadau wa elimu na sekta ya ajira ili kuhakikisha wahitimu wake wanakuwa na ujuzi unaotakiwa katika mazingira halisi ya kazi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa William Amos Pallangyo akizungumza katika kikao hicho mjini Morogoro. Picha na Juma Mtanda

Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Dk Hassanal Issaya, amesema maboresho ya mitaala yanafanywa kwa mfumo shirikishi unaowahusisha wadau mbalimbali ili kuondoa pengo la ujuzi kwa wahitimu.

“Hatutengenezi mitaala kwa kuiga, bali tunashirikisha wadau wote muhimu wakiwemo wafundishaji, wanafunzi na wadau kutoka viwandani na mashirika mbalimbali ili kuelewa ni aina gani ya mhitimu anayehitajika katika soko la ajira,” amesema Dk Issaya.

Baadhi ya wajumbe wa baraza hilo wamesema kikao hicho ni jukwaa muhimu la kujadili mwelekeo wa taasisi na namna ya kuimarisha mafanikio yake kwa manufaa ya jamii na sekta mbalimbali za uchumi.

Joyce Ntana, mmoja wa wajumbe, amesema ushirikishwaji unaofanywa na menejimenti ya TIA katika ngazi zote unasaidia kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo.

Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Wafanyakazi, Daud Mashauri, amesema kikao hicho pia kinatimiza matakwa ya kisheria yanayotaka taasisi kuwa na mabaraza ya wafanyakazi kwa ajili ya kutoa ushauri na kufanya mapitio ya bajeti.

“Baraza la wafanyakazi ni chombo muhimu kinachosaidia kushauri menejimenti na kufanya mapitio ya mipango na bajeti za taasisi, hivyo ni nguzo muhimu katika uendeshaji wa taasisi,” amesema Mashauri.