Katika sehemu ya kwanza ya simulizi ya tukio la baba kumuua mtoto wake mwenye umri wa miaka 4 na miezi 6 kisha kumkata vipande vipande na kuvitumbukiza chooni, tuliishia ushahidi wa mama wa mtoto, alivyosimulia hatua kwa hatua juu ya tukio hilo.
Tuliona pia mama huyo, Daima Hongoli alivyoitwa na polisi katika nyumba aliyokuwa akiishi mzazi mwenzake, Joseph Mhulula ambaye amehukumiwa adhabu ya kifo, na kushuhudia vipande vya mwili wa mwanae vikiopolewa chooni.
Leo tunakuletea sehemu ya pili ya simulizi hii ya mauaji ya Timotheo Mhulila, tukiangazia na mshtakiwa alivyomuita askari mmoja wakati akiwa mahabusu na kumweleza kuwa anataka kueleza ukweli juu ya mauaji hayo.
Shahidi namba 2 wa Jamhuri, Inspekta Elijah Bundala, aliieleza Mahakama alivyompokea Daima Hongoli na jinsi alivyomweleza kuwa mtoto wake amepotea, na alipomhoji na mazingira ya kupotea, shahidi huyo alimshuku mzazi mwenzake kuhusika.
Inspekta Bundala alipata namba ya Mhulila kupitia kwa mzazi mwenzake na kuipiga lakini ilikuwa haipatikani hewani, na ndipo alitafuta namba ya mwenyekiti wa mtaa na kumtaka amwambie mshukiwa huyo kuripoti kituo cha polisi.
Mhulila aliitikia wito huo na kufika kituo cha Polisi, Dawati la Jinsia na kuanza kumdodosa juu ya kupotea kwa mtoto, akawa anajibu lakini huku anatetemeka na kuelezea kuwa mtoto alipotelea eneo la Hoteli ya Kani, alipokua amemwacha nje.
Alimweleza askari huyo (shahidi) kuwa alitoka nje ya hoteli hakumkuta mtoto, ndipo shahidi huyo akafungua jalada la uchunguzi la utekaji au kupotea kwa mtoto na hapo hapo alimkamata Mhulila na kumjulisha kuwa anatuhumiwa kwa kosa hilo.
Mshtakiwa aomba kukiri kosa
Shahidi wa 5 wa Jamhuri, Ofisa wa Polisi H.4712 Koplo Antony, katika ushahidi wake alisema Mei 6, 2025 saa 2:00 asubuhi akiwa Kituo cha Kikuu cha Polisi Iringa, kuna mtu mmoja aliyekuwa mahabusu kituoni hapo alimwita ili amweleze jambo.
Mtu huyo alikuwa ni mshitakiwa Mhulila na alikuwa akimfahamu kuwa ni dereva bodaboda na huko nyuma aliwahi kumkodi na kutumia usafiri wake.
Alipomsogelea mshtakiwa huyo, alimweleza kuwa amekaa mahabusu kwa muda mrefu, hivyo alitaka amweleze ukweli wa nini hasa kilitokea, ndipo naye akamjulisha mkuu wake wa kazi, kisha baadaye alimtoa mahabusu ili kumsikiliza.
Alimpeleka kwa Inspekta Lazaro Ngoko ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OC-CID) na shahidi namba 8 na wakiwa hapo yeye (Koplo Antony) alimtaka mtuhumiwa awe huru kumweleza bosi wake Inspekta Ngoko ukweli wote anaoujua.
Anasema mshitakiwa alimweleza OC-CID kuwa amemuua Timoth Mhulila ambaye ni mtoto wake, na kukata mwili wake vipande vipande na kuvitumbukiza chooni na walipomuuliza sababu za kufanya hivyo, alidai alifanya hivyo kwa tamaa ya utajiri.
Awapeleka polisi eneo la tukio
Baada ya maelezo hayo, Inspekta Ngoko ambaye ni shahidi wa 8 wa Jamhuri, aliandaa timu ya makachero na kumtaka mshitakiwa awaongoze hadi eneo la tukio nyumbani kwake Mtaa wa Lukosi ambapo alikuwa akiishi kipindi chote.
Makachero hao waligonga lango kuu la nyumba hiyo na kufunguliwa na mmiliki wa nyumba hiyo, Maximilian Luhwago aliyekuwa shahidi namba 4 wa Jamhuri, ambayo alimtambua mshitakiwa kuwa ni mpangaji wake tangu 2021.
Baada ya kuitwa viongozi wa mtaa, shahidi namba 8 na 5 walimtaka mshitakiwa awaambie viongozi hao kile alichowaeleza walipokuwa kituo cha Polisi ambapo alirudia kueleza jinsi alivyomuua mtoto wake.
Pia aliwaeleza kuwa baada ya kumuua, alimkata vipande vipande na kuvitumbukiza chooni na alimwaga maji kuhakikisha vinatumbukia vyote na hapo ndipo shahidi wa 4 (mwenye nyumba) alipowaruhusu polisi kufungua choo kutoa vipande hivyo.
Polisi na viongozi wa mtaa waliokuwepo, waliomba usaidizi kutoka Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji ambapo Inspekta Msaidizi aitwaye Banzi aliyekuwa shahidi wa sita alifika eneo hilo akiwa na maofisa wengine wa kikosi hicho.
Hatua iliyofuata iliwalazimu maofisa hao kuvunja shimo la majitaka la choo ambapo askari wa Zimamoto walizama ndani na kuopoa vipande vya mwili wa binadamu vilivyokuwa vikielea.
Kwa kuwa shimo hilo lilikuwa na majitaka, maofisa hao waliomba msaada kutoka Mamlaka ya Majisafi na Taka Iringa (Iruwasa), ili kunyonya maji ambapo shahidi wa saba wa Jamhuri alifika na gari mahsusi na kufanya kazi hiyo.
Baada ya kuondoa majitaka, vipande vya mwili wa mwanadamu vilipatikana na vyote vilikabidhiwa kwa shahidi wa tisa, Inspekta Mshanga Lucas ambaye ni Ofisa aliyetangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) kama mtaalamu wa uchunguzi wa kisayansi.
Zoezi hilo lilichukua takribani saa 6 hadi saa 9:45 alasiri na baada ya shughuli hiyo kukamilika, maofisa wa Polisi walirejea kituoni na mshitakiwa pamoja na vielelezo.
Akijibu maswali ya dodoso, shahidi huyo wa tano alieleza kuwa vipande vya mabaki ya mwanadamu, vilikuwa vidogo chini ya inchi 4, hivyo ilikuwa ni rahisi kuingia kwenye choo cha kuflush na mshitakiwa alivikata kwa kutumia kisu.
Shahidi huyo alieleza kuwa mshitakiwa alimweleza kuwa kwa ile mifupa mikubwa kama fuvu, alitumia jiwe kuivunja vunja katika vipande vidogo vidogo.
Mashahidi namba 6, 7 na 8, walielezea mazingira ya shimo la choo lilivyokuwa na kwamba ni mshitakiwa mwenyewe ndiye aliyewajulisha amefanya mauaji hayo Aprili 12, 2025 na kuukata mwili vipande vipande.
Aliyeandika maelezo ya kukiri
Shahidi namba 12, H.2526 Koplo Juma ndiye aliyepewa jukumu la kuandika maelezo ya onyo ya mshitakiwa ambapo amesema alimweleza haki zake ikiwamo kuita ndugu, rafiki, wakili wake au mtu yeyote kushuhudia akitoa maelezo yake.
Mshitakiwa aliamua kutoa maelezo yake pasipokuwepo yeyote kati ya watu hao na shahidi aliandika maelezo hayo yaliyopokelewa mahakamani kama kielelezo P2 na baada ya kumaliza kuandika, alimpa mshitakiwa kuyasoma akasema yako sawa.
Shahidi huyo alisema wakati anaandika maelezo hayo, mshitakiwa alimweleza kuwa alimuua mtoto wake kwa kuwa alikuwa na tamaa ya kuwa tajiri na kwamba alimkatakata katika vipande vidogo. Aliamini mshitakiwa alikuwa anasema kweli kwa kuwa alitoa maelezo yake kwa hiyari.
Vipimo vya DNA vikafanyika
Shahidi wa 9 na wa 10 wa Jamhuri, ushahidi wao ulikuwa ni namna walivyosimamia uchukuaji wa sampuli kwa ajili ya DNA na kuzisafirisha hadi Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Jijini Dar es Salaam kwa uchunguzi.
Shahidi wa 13, Rajabu Mohamed ambaye ni mkemia wa Serikali daraja la kwanza katika ofisi ya mkemia mkuu alieleza namna alivyopokea sampuli kutoka kwa Ofisa wa Polisi aliyetumwa kutoka Iringa kwa ajili ya kuzifanyia uchunguzi wa DNA.
Baada ya kukagua sampuli hizo, aligundua ni mifupa ya binadamu, mate na damu kutoka kwa shahidi wa kwanza ambaye ni mama mzazi wa marehemu na mate na damu kutoka kwa mshitakiwa na kwamba sampuli zilikuwa katika hali njema.
Kulingana na ushahidi wake ni kwamba sehemu 15 za sampuli za mshitakiwa zilioana na sampuli A1 hadi A9 na kwamba sampuli zote 15 zilizochukuliwa kwa shahidi wa kwanza wa Jamhuri (mama) zilioana na marehemu.
Shahidi huyo alisema uwezekano kuwa mshitakiwa ni baba mzazi wa marehemu ulikuwa ni asilimia 99.99 na pia uwezekano kuwa Daima ni mama mzazi wa marehemu pia ulikuwa ni asilimia 99.99 kutokana na mifupa iliyochunguzwa.
Akijibu maswali ya dodoso, shahidi huyo alisema hakushuhudia sampuli hizo zikichukuliwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa bali alipokea bahasha kubwa ambayo ndani yake kulikuwa na bahasha ndogo ikiwa na sampuli hizo.
Alisema pia kuwa halikuwa jukumu lake kama mtaalamu wa maabara kutafuta kama mifupa ile ilikuwa ni ya mtu aliye hai au aliyekufa na kwamba kimantiki, sio rahisi kuchukua mifupa 15 kutoka kwa mtu ambaye yuko hai.
Alieleza pia kuwa sampuli zote hizo ziliteketezwa baada ya miezi sita kulingana na sheria za utunzaji wa sampuli na kwamba sheria inatambua ofisa wa Polisi mwenye cheo cha Inspekta kama ni ofisa anayeweza kuchukua sampuli.
Usikose mfululizo wa simulizi hii kesho ambapo tutakuletea utetezi wa mshitakiwa ili ujue nini alikisema mahakamani kabla ya uamuzi.