Rais Mwinyi Awasisitiza Waumini Kuendeleza Maadili Mema Baada Ya Ramadhani

Global Publishers
March 20, 2026
0 Comments

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasisitiza waumini wa dini ya Kiislamu kuyaendeleza mambo yote mazuri waliyokuwa wakiyatekeleza wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 20 Machi 2026, alipojumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika ibada ya Sala ya Ijumaa iliyosaliwa katika Msikiti wa Ijumaa Maisara, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Aidha, ameeleza kuwa kumalizika kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kusiwe sababu ya watu kurejea katika matendo maovu na yasiyompendeza Mwenyezi Mungu, bali iwe ni fursa ya kuendeleza ibada na maadili mema.

Alhaj Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwapa pole waumini wa msikiti huo kufuatia kifo cha Imam wao, Sheikh Saleh Ameir, aliyefariki tarehe 19 Machi 2026.

Rais Dkt. Mwinyi amewatakia waumini wa dini ya Kiislamu kila la heri na furaha katika kusherehekea Sikukuu ya Idd el-Fitri, kesho baada ya kukamilika kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.