Dar/Geita. Waislamu nchini na duniani kote kesho wataadhimisha Sikukuu ya Eid El-Fitri, huku Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) likisema Rais, Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi katika Baraza la Eid litakalofanyika kitaifa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa awali na Katibu Mkuu wa Bakwata, Alhaj Nuhu Mruma, sherehe hizo zitafanyika katika Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), kuanzia saa 9:00 alasiri.
Wakati huohuo, viongozi wa dini mkoani Geita wamewataka waumini wa Kiislamu kuendeleza maadili waliyojifunza wakati wa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, wakisisitiza umuhimu wa kumtegemea Mungu katika maisha yao ya kila siku.
Akizungumza wakati wa swala ya Eid iliyofanyika leo Ijumaa Machi 20, 2025 katika Msikiti wa Al-Mtakuja mjini Geita, Sheikh Dauda Bushumbilo wa Taasisi ya Ansari amesema Ramadhani imewafundisha Waislamu umuhimu wa toba, ibada na kumtegemea Mwenyezi Mungu.
Amesema swaumu ni ibada binafsi kati ya mwanadamu na muumba wake, hivyo kila muumini anapaswa kuendeleza ucha Mungu hata baada ya kumalizika kwa mwezi huo mtukufu.
“Tunapomaliza swaumu, Mwenyezi Mungu haondoki; kinachoondoka ni Ramadhani. Ni wajibu wetu kuendelea kushikamana na ucha Mungu ili kufikia malengo ya swaumu,” amesema Sheikh Bushumbilo.
Aidha, amewataka wanawake kuendeleza maadili ya kujisitiri kama walivyofanya wakati wa mfungo, huku akiwahimiza wanaume kutokuwa kikwazo katika kudumisha maadili hayo.
Kwa upande wao, baadhi ya waumini wameeleza umuhimu wa kuendeleza ibada na kudumisha amani nchini.
Muumini Abdulrahman Yassin amesema ni muhimu kwa Waislamu kuendelea kumcha Mungu wakati wote, si tu katika kipindi cha Ramadhani.
Naye Kassim Abdallah ameishukuru Serikali kwa kuendelea kulinda amani nchini, akiwataka wananchi wote bila kujali dini zao kushirikiana katika kudumisha utulivu huo.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutuwezesha kuishi kwa amani. Ni wajibu wetu sote kuilinda ili nchi iendelee kuwa salama,” amesema.
Maadhimisho ya Eid El-Fitri huchukuliwa kuwa fursa muhimu ya kuimarisha umoja, kusherehekea mafanikio ya kiroho baada ya mwezi wa Ramadhani na kuendeleza mshikamano miongoni mwa Waislamu nchini.
Akizungumzia sherehe zitakazofanyika kesho, Alhaj Mruma amesema zitaanza kwa Swala ya Eid itakayofanyika katika Msikiti wa Mfalme Mohamed VI, uliopo Makao Makuu ya Bakwata, Kinondoni, kuanzia saa 1:30 asubuhi.
Amefafanua kuwa baada ya swala hiyo, Waislamu watakusanyika katika Ukumbi wa JNICC kwa ajili ya Baraza la Eid litakaloanza saa 9:00 alasiri, na kutoa wito kwa waumini kuhudhuria kwa wingi na kwa wakati.
Alhaj Mruma amesema uwepo wa Rais Samia katika sherehe hizo unaashiria mshikamano wa kitaifa na kuthamini nafasi ya Waislamu katika jamii.
Katika ujumbe wake, Katibu Mkuu huyo pia amewatakia Waislamu na Watanzania wote kwa ujumla sikukuu njema huku akihimiza kuimarisha amani na mshikamano.
